HOTUBA YA MSEMAJI MKUU WA KAMBI RASMI YA UPINZANI BUNGENI MH. PROF. KULIKOYELA KANALWANDA KAHIGI (MB) KUHUSU MAPITIO YA UTEKELEZAJI WA BAJETI YA 2012/2013 NA MAKADIRIO YA MAPATO NA MATUMIZI YA OFISI YA RAIS – MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA KWA MWAKA WA FEDHA 2013/2014
UTANGULIZI
Mheshimiwa Spika,
kwa mujibu wa Kanuni ya 99(9) ya Kanuni za Kudumu za Bunge, toleo la 2013,
naomba kuwasilisha maoni ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inayoongozwa na
CHADEMA, kuhusu mapitio ya utekelezaji wa Bajeti ya 2012/2013 na makadirio ya
mapato na matumizi ya Ofisi ya Rais – Menejimenti ya Utumishi wa Umma kwa mwaka
wa fedha 2013/2014.
Mheshimiwa Spika,
Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inayoongozwa na CHADEMA, kipindi hiki itajikita
katika mambo machache mahususi katika Ofisi ya Rais - katika Utawala bora,
Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Mahusiano na Uratibu - ambayo tunayaona ni
mapungufu. Lengo la kufanya hivyo ni kuitaka Serikali ama ichukue hatua ya
kuyatokomeza mapungufu hayo kwa kutangaza hadharani nia yake ya kuyakomesha, kisha
ichukue hatua mwafaka, au ijiuzulu kwa kushindwa kuongoza dola.
- UTAWALA BORA
2.1.
Idara
ya Usalama wa Taifa – Ikulu
Mheshimiwa Spika, kwa
muda mrefu sasa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inayoongozwa na CHADEMA
imeitaka Serikali kuwachukulia hatua maafisa wa Idara ya Usalama wa Taifa –
Ikulu ambao wanatuhumiwa kujihusisha na vitendo vya kihalifu vya utekaji na
utesaji kwa watu wanaoonekana kuikosoa Serikali, lakini mpaka sasa hakuna hatua
dhahiri zinazochukuliwa ilhali matukio
hayo ya utekaji na utesaji yanazidi kuongezeka katika nchi yetu.
Mheshimiwa Spika, aliyetajwa
na Gazeti la Mwanahalisi kuhusika na
kitendo cha kinyama cha kumteka na kumtesa Dkt. Ulimboka mwezi Juni, 2012 ni afisa
wa Usalama wa Taifa, Ramadhani Ighondu Abeid. Tulitarajia Serikali, kupitia
Jeshi la Polisi, ingemkamata na kumhoji mtu huyu ili kujiridhisha na tuhuma
dhidi yake na kuchukua hatua kwa mujibu wa sheria za nchi, lakini mpaka leo
hakuna chochote kilichofanyika kuhusu uhalifu dhidi ya binadamu aliofanyiwa
Dkt. Ulimboka, jambo ambalo linaashiria kwamba Serikali iliridhika na
kilichotokea. Lakini jambo baya zaidi ni kwamba Gazeti la Mwanahalisi lililosaidia kugundua uhalifu huo lilifungiwa kwa muda
usiojulikana.
Mheshimiwa Spika, mazingira
ya kuteswa kwa Mhariri wa Shirika la Habari,
ndugu Absalom Kibanda yanafanana sana na yale ya kutekwa na kuteswa kwa Dkt.
Ulimboka. Aidha, aina ya utesaji (mfano kung’olewa kucha, meno na kutobolewa jicho)
unafanana sana na aina ya mateso aliyopata Dkt. Ulimboka. Hivyo, ushahidi wa
kimazingira unaonesha kwamba waliomteka na kumtesa Dkt. Ulimboka yumkini ni
walewale waliomteka na kumtesa Absalom Kibanda au mawakala wao.
Mheshimiwa Spika, katika
sakata la Dkt. Ulimboka, jeshi la polisi lilidai kuwa limemkamata mtu mmoja
lililodai kuwa ni raia wa Kenya ambaye hatima ya kesi yake haijulikani mpaka
sasa. Kwa tukio la Absalom Kibanda hadi sasa hakuna taarifa rasmi ya watu
walioshtakiwa kuhusu uhalifu huu dhidi ya binadamu. Dkt. Ulimboka ambaye
angeweza kutoa msaada kwa Polisi kuwakamata waliohusika na uhalifu huo, hajahojiwa
mpaka leo ingawa katika kiapo chake alichokiandika mbele ya mwanasheria wake
alimtaja afisa wa Usalama wa Taifa - Ikulu kuwa alihusika kumteka na kumtesa.
Inashangaza sana kwa nini Serikali haijataka kutumia maelezo ya Dkt. Ulimboka
mwenyewe kuwakamata wahalifu. Jambo jingine la kusikitisha ni kwamba kuna dalili
za wazi kwamba suala la kutekwa na kujeruhiwa vibaya kwa Absalom Kibanda
limesahaulika kabisa.
Mheshimiwa Spika, kwa
mujibu wa Kanuni ya Adhabu ya Tanzania (Penal Code), kuteka na kutesa ni makosa
ya jinai. Ni aibu kwa Idara ya Usalama wa Taifa iliyokabidhiwa jukumu kubwa na
la heshima kubwa la kuulinda usalama na usitawi wa nchi kutuhumiwa kujihusisha
na vitendo vya kikatili kama hivi. Kitendo cha kuhisiwa tu kwamba chombo hiki
cha usalama kinajihusisha na vitendo vya kijinai moja kwa moja kinakikosesha
sifa ya kufanya kazi ya usalama wa taifa. Na kwa kuwa chombo hiki kiko chini ya
mamlaka ya Rais moja kwa moja tayari ni
doa kubwa kwa Rais mwenyewe, Serikali
yake na hata kwa chama chake.
Mheshimiwa Spika, kwa
mujibu wa Sheria ya Ujasusi na Usalama ya Tanzania (Tanzania Intelligence and
Security Services Act) ya 1996, Idara ya Usalama wa Taifa hairuhusiwi kufanya
upelelezi wa ufuatiliaji - “ushushushu”
kwa watu wanaoipinga Serikali kwa
misingi ya kisheria na kikatiba (kwa maana ya vyama vya siasa, vyombo vya
habari na wanaharakati). Ibara ya 5(2),
kipengele ‘a’ na ‘b’ inasomeka hivi:
“It shall not be
the function of the Service :
a) to
enforce measures for security or;
b) to
institute surveillance of any person or category of persons by reason only of his or their involvement in
lawful protest or dissent in respect of any matter affecting the constitution ,
the laws or the Government of Tanzania”.
Mheshimiwa
Spika, kwa tafsiri isiyo rasmi, sheria inasema hivi:
“Haitakuwa kazi ya Idara
kufanya yafuatayo:
a) kutekeleza
hatua za usalama, au
b) kufanya
upelelezi wa ufuatiliaji wa mtu yeyote au kundi lolote la watu kwa sababu tu ya
kuhusika na kupinga au kushiriki maandamano halali kuhusiana na jambo lolote la
kikatiba, sheria au Serikali ya Tanzania”.
Mheshimiwa
Spika, nimelazimika kunukuu sheria hii kwa kuwa Kambi Rasmi ya
Upinzani inayoongozwa na CHADEMA, inao ushahidi kwamba maafisa wa Usalama wa
Taifa wamekuwa wakifanya upelelezi wa ufuatiliaji (surveillance) kwa watu
wanaoipinga Serikali kwa misingi ya Katiba na sharia - jambo ambalo ni kinyume na sheria iliyopo.
Mheshimiwa
Spika,
ushahidi wenyewe ni kwamba baada ya Mkurugenzi wa Ulinzi na Usalama
wa CHADEMA kutuhumiwa kwamba anahusika na ugaidi na video yake
kurushwa
kwenye mitandao ya kijamii, Muhidin Issa Michuzi, ambaye ni mpiga picha
wa
Rais, Ikulu, aliandika barua-pepe kwa Salvator Rweyemamu, Prosper Mbena,
Hamis
Mwinyimvua, Liberatus Mulamula, Msafiri Marwa, Laurent Ndumbaro na
wengine
ambao ni watumishi wenzake wa Ofisi Binafsi ya Rais akiwapongeza kwa
kazi nzuri
na ya ziada waliyoifanya ya kutengeneza video ya Lwakatare, na kuwaeleza
kuwa hiyo ni kete kubwa kwao hivyo lazima waipigie kelele sana.
Mheshimiwa
Spika, kuna ushahidi mwingine kwamba baadhi ya maafisa wa Idara
ya Usalama wa Taifa (TISS) wanawahonga kwa kuwalipa fedha watumishi wa CHADEMA
ili watoe ushahidi wa uongo dhidi ya kesi inayomkabili Mkurugenzi wa Ulinzi na
usalama wa CHADEMA. Miongoni mwa maafisa hao ni Sinbard Mwagha. Huyu ni ni afisa usalama wa taifa anayefanya kazi makao makuu ya idara hiyo.
Taarifa zilizopo ni kwamba ndiye anayetumika kuendesha michezo ya kuhonga
wanasiasa wa CCM na upinzani, na kwamba ndiye anayehusika pia kuwapanga wabunge wa CCM waongee nini bungeni
wakati wa vikao vya bunge kwa maslahi ya CCM.