Bukobawadau

KAGERA WALIA NA OFISI YA MRAJISI WA VYAMA VYA USHIRIKA

Na Prudence Karugendo

MRAJISI  wa Vyama vya Ushirika ni msimamizi na mlezi wa ushirika nchini. Kwa nafasi yake hiyo tunategemea kuwaona wananchi wakiwa wameboresha maisha yao baadaya ya kuunganisha nguvu zao kwa mtindo wa ushirika kujiinua kiuchumi. Hali hiyo inajiweka wazi kutokana na kuwepo kwa ofisi ya Mrajis inayopaswa kutoa moungozo wa kitaalamu na kuhakikisha ushirika unakuwa imara na kutoa matunda yaliyokusudiwa.

Wananchi wanatarajia kuyaona maisha yao yakishamiri yakiwa ndiyo matunda ya ushirika. Sababu ushirika siyo mapambo, bali njia ya wananchi kuinuana kiuchumi, kujiondoa kwenye ufukara.

Lakini katika miaka ya karibuni ushirika nchini umeangukia pua. Vyama vingi vya ushirika, katika maeneo mbalimbali ya nchi,  vimezorota sana na vingine kufa kabisa. Tena cha kusikitisha, vinakufa vifo vya kulazimishwa kutokana na kuhujumiwa.

Swali linalojitokeza ni la kwa nini hali iwe hivyo ilhali ofisi iliyotengwa na serikali kwa ajili ya kuvisimamia na kuvilea vyama vya ushirika, Ofisi ya Mrajis wa Vyama vya Ushirika, inaendelea kufanya kazi? Kwa nini vyama vya ushirika vionekane yatima wakati mzazi na mlezi wake bado yuko hai?

Swali hilo linazidi kuwa tata na kuzidisha ugumu wa kujibika hasa pale zinapojitokeza dalili za kwamba Ofisi ya Mrajis wa Vyama vya Ushirika, kwa njia moja au nyingine, nayo inahusika na vitendo vya kudhoofisha shughuli za ushirika nchini.

Dalili hizo mbaya na za kushangaza zimeanza kujionyesha kupitia mkoani Kagera ambako wanaushirika, chini ya chama kikuu cha ushirika cha KCU (1990) Ltd., wanailalamikia Ofisi ya Mrajis kwa kushindwa kuchukua hatua muafaka kukinusuru chama chao cha ushirika.

Mbali na malalamiko kadhaa ambayo yameishamfikia hata Waziri wa Kilimo na Ushirika, hasa malalamiko ya kuhusu ukaribu husio na kheri kati ya Mrajis Msaidizi mkoani Kagera na uongozi wa KCU (1990) Ltd., yapo vilevile malalamiko mengine kuhusu Mrajis Msaidizi kupindisha mambo kinyume cha utaratibu katika uendeshaji wa Benki ya Wakulima, Kagera Farmers’ Co-operative Bank, ambayo KCU (1990) Ltd. ni mwanahisa.

Mwaka 2002 Bodi ya KCU (1990) Ltd. ilitoa wazo la kuanzisha Benki ya Wakulima kwa kuwatafuta wanahisa wengine ili kutimiza azima hiyo.  Wazo hilo lilipata Baraka za Mkutano Mkuu na hivyo Benki ya Wakulima, Kagera  Farmers’ Co-operative Bank (KFCB), ikawa imeanzishwa baada ya kupata leseni toka Benki Kuu ya Tanzania.

Wanahisa waanzilishi walikuwa ni KCU (1990) Ltd. yenyewe, Mfuko wa Mazao, na Vyama vya Msingi. Baadaye Saccos na Maihanika (saccos kwenye vyama vya msingi) nao wakapewa hisa.

Madhumuni ya kuanzisha Benki ya Wakulima, pamoja na mambo mengine, yalikuwa kwamba KCU (1990) Ltd. iweze kukopa kwenye benki hiyo ili kuepuka riba kubwa zinazotozwa na mabenki mengine. Vilevile riba ndogo iliyotarajiwa kutozwa na benki hiyo bado ilikuwa ni faida kwa wenye benki ambao ni pamoja na wakulima, wanaushirika.

Lakini ni jambo la kushangaza kwamba tangu kuanzishwa kwa KFCB, KCU (1990) Ltd. haijawahi kukopa kwenye benki hiyo kwa kiasi cha kuridhisha. Kisingizio mara zote kimekuwa kwamba benki hiyo haijawa na mtaji wa kutosheleza mahitaji ya KCU (1990) Ltd. Hata pale benki hiyo ilipopata pesa kutoka mfuko wa serikali kwa ajili ya kuwainua wakulima (AGIPF), bado KCU (1990) Ltd. iligoma kukopa kwenye benki hiyo na hivyo kuikosesha riba ndogo ambayo ingenufaika nayo kama faida, wakati chama hicho cha ushirika kikiendelea kukopa kwenye benki za CRDB na nyingine kwa riba kubwa!

Baada ya maswali kuwa mengi juu ya kwa nini aliyetarajiwa kuwa mteja mkubwa na wa kutumainiwa na KFCB, KCU (1990) Ltd., anagoma kuitumia benki hiyo, maswali na mshangao hasa vilivyokuwa vinatoka kwenye uongozi wa KFCB, ndipo ikaanza kufanyika mizengwe ya kuuondoa uongozi wa benki hiyo kusudi uwekwe uongozi unaotokana na KCU (1990) Ltd. kwa lengo la kuendelea kuidhoofisha benki hiyo kimyakimya.

Ni kweli kwamba KCU (1990) Ltd. ndiye mwanahisa mkubwa kuliko wote katika Benki ya Wakulima, lakini katika sheria za ushirika hakuna panaposemwa kwamba mwenye hisa kubwa ndiye awe kiongozi.

Kwahiyo ni wazi kwamba, mizengwe hiyo ambayo kwa sasa tayari imefanikiwa, ya KCU (1990) Ltd. kukamata uongozi wa KFCB, ililenga kuyazima maswali ya kwa nini chama hicho kikuu cha ushirika hakiitumii benki hiyo kama yalivyokuwa madhumuni ya uanzishwaji wake.

Jambo la kushangaza ni namna Mrajis Msaidizi alivyoidaka mizengwe hiyo, iliyoonekana tayari ilikuwa na Baraka zake,  na kuigeuza ya kwake kiasi cha kuitumia yeye mwenyewe dhidi ya uongozi wa KFCB uliokuwa unamaliza kipindi kimoja kabla ya kuendelea na kipindi kingine.

Mrajis Msaidizi aliingiza kinyemela kwenye masharti ya Bodi ya KFCB kipengere ambacho hakikuwa na Baraka za Bodi. Kipengere hicho kilichoingizwa kinyemela kinasema kwamba wajumbe wa Mkutano Mkuu wa KFCB ni sharti watoke kwenye Bodi za vyama vya msingi, kitu kinachowatenga baadhi ya wenye hisa, wenye mali, kwa kuwanyima fursa ya kugombea nafasi yoyote ya uongozi kwenye benki yao isipokuwa kupiga kura tu, tena kwenye vyama vyao vya msingi.

Kipengere hicho kilichochomekwa na Mrajis Msaidizi, moja kwa moja,  kinaubatilisha Mkutano Mkuu uliofanyika mwaka jana na kuuondoa madarakani uongozi wa KFCB kwa vile kilikuwa kimewafukuza wajumbe halali wa mkutano mkuu. Hivyo Mkutano Mkuu wa mwaka jana ulifanywa na wajumbe waliopatikana kinyemela kwa juhudi binafsi za Mrajis Msaidizi. Na mkutano huo ndio ukaja kutoa Baraka za marekebisho ya masharti hayo mapya yaliyoletwa na Mrajis Msaidizi na kuwafukuza wajumbe halali wa Bodi na Mkuatano Mkuu wa KFCB.

Kwa vielelezo vinavyoonyeshwa na wahusika ni kwamba masharti mapya hayakupitia kwenye mkutano wa Bodi ya KFCB wala Mkutano Mkuu, na hata Mrajis Msaidizi alikuwa hajayasaini, lakini cha kushangaza yakatumika kuendesha Mkutano Mkuu!

Wanaushirika wanasema kwamba Mrajis Msaidizi wa mkoa wa Kagera yupo kumsaidia Mrajis wa Vyama vya Ushirika nchini. Lakini eti badala yake anaonekana kumpotosha, sasa haieleweki kama huo upotoshaji ndio msaada unaotakiwa na mtu kutoka kwa msaidizi wake.

Eti Mrajis Msaidizi alimweleza Mrajis kwamba watu hawa, wajumbe wa Bodi ya KFCB, wamekaa kwa  muda mrefu wakati ukweli ni kwamba wajumbe hao wa Bodi walikuwa na kipindi kimoja na mmoja tu ndiye aliyekuwa na vipindi viwili. Wakati kanuni ya theluthi inaagiza mtu akae vipindi vitatu. Katika mkutano wa mwaka jana mtu mmoja ndiye aliyekuwa anaingia katika theluthi ya tatu wakati wengine walikuwa wanaingia theluthi ya pili.

Mbinu chafu za Mrajis Msaidizi. Wajumbe wa zamani waliotaka kugombea tena ujumbe wa Bodi ya KFCB, katika uchaguzi wa mwaka jana, ambao walikuwa hawabanwi na kipengere kipya cha Mrajis Msaidizi, walinyimwa fomu kwa hadaa kuwa fomu zao za zamani zilikuwepo, zinatosha. Lakini baadaye Mrajis Msaidizi akatangaza bila aibu kwamba wajumbe ambao hawakujaza fomu walikuwa wamejiondoa wenyewe kwenye kugombea. Matokeo yake Mrajis Msaidizi akashindwa kuwapata wagombeaji wa kutosha, mkutano ikabidi uahirishwe.

Wanaushirika wanasema kwamba hayo yote yamefanyika kwa shinikizo la KCU (1990) Ltd. kwa vile chama hicho kikuu cha ushirika hakikuwa katika mahusiano mazuri na mwenyekiti wa Bodi ya KFCB aliyeondolewa kinyemela.

Nilipomtafuta mwenyekiti huyo aliyeondolewa, Bw. Rweyongeza Bagyemu, kuona kama analo la kuongea juu ya sakata hilo, akasema kwa sasa amelazwa anaumwa. Hivyo hawezi kuongelea suala hilo kwa wakati huu. Ila akathibitisha kwamba niliyoelezwa yote yana ukweli uliokamilika. Na kuahidi kwamba akiwa mzima kuna mengine atayaongeza katika kuzidi kuliweka wazi suala hilo.

Kwa mwenendo huu Mrajis Msaidizi wa mkoa wa Kagera akiendelea kukalia nafasi yake hiyo masuala yote ya ushirika mkoani Kagera yatabaki tu kwenye masimulizi. Hiyo ni kutokana na Mrajis huyo Msaidizi kuonekana anatanguliza maslahi binafsi badala ya maslahi ya ushirika.

Linalopaswa kuzingatiwa ni kwamba wanaushirika wameamua kuanzisha benki. Ieleweke kwamba benki ni chombo kinachotakiwa kuendeshwa kwa weledi bila kufuata tu uwakilishi wa ilmaradi. Hicho ni chombo muhimu cha kiuchumi kinachohitaji watu wenye sifa zilizo katika taaluma hiyo. Kuichezea benki ni kuuchezea uchumi wa watu na hivyo kuyachezea maisha na uhai wao.

Pamoja na kwamba Mrajisi Msaidizi ndiye anayefanya mchujo wa mwisho wa wajumbe wa KFCB, anatakiwa kuzingatia kwamba benki hiyo imesimama kwenye mihimi miwili. Wa kwanza ni Ushirika na wa pili ni Benki Kuu ya Tanzania (BOT). Lakini ikiangaliwa itaonekana kwamba wajumbe wa KFCB waliopitishwa na Mrajis Msaidizi wengi wanakidhi vigezo vya mhimili mmoja tu, ushirika, wakati wako nje kabisa ya vigezo vya BOT. Hiyo ni kwa sababu wengi wao ni wa darasa la 7. Haitegemewi hata kidogo mhitimu wa darasa la saba awe na vigezo vya BOT.

Swali wanalojiuliza wanaushirika ni kwamba, hivi kweli Mrajis Msaidizi wa Kagera anayo dhamira ya dhati ya kuiona benki hiyo ya wakulima ikishamiri?

Mfano, Kamati ya Usimamizi inayotakiwa kuwa na wajumbe watatu mpaka sasa inasemekana inaye mjumbe mmoja tu. Hiyo imesababishwa na mizengwe ya Mrajis Msaidizi ya kupindisha masharti ya kuwapata wajumbe kwamba ni lazima watoke kwenye Bodi za vyama vya msingi, kitu ambacho hakimo katika sheria za ushirika, badala ya wanachama wote. Ni vigumu kuwapata wajumbe wenye vigezo vya BOT kwenye vyama vya msingi.

Pamoja na malalamiko ya wanaushirika mkoani Kagera juu ya utendaji usioridhisha wa Mrajis Msaidizi mkoani humo, bado wadau hao wa ushirika wanayo machache,  lakini muhimu, ya kuisemea ofisi ya Mrajis Msaidizi mkoani mwao.

Wanasema kwamba ofisi hiyo ni kama imetelekezwa na wahusika kitu kinachomlazimisha Mrajis Msaidizi ajipendekeze kwa Chama Kikuu cha Ushirika, KCU (1990) Ltd.,  ili kujinusuru kimaslahi. Ni katika hali hiyo ambamo Mrajis Msaidizi anajikuta chini ya usimamizi wa chama hicho cha ushirika kama mwajiriwa wake na hivyo kuuondoa uwezekano wa yeye kukisimamia chama hicho kama sheria ya vyama vya ushirika inavyoelekeza.


0784 989 512 
Next Post Previous Post
Bukobawadau