Bukobawadau

Maggid Mjengwa: Kuhusu mimi kumfahamu Ludovick

Ndugu zangu,
Ndugu yangu January Makamba alipata kuyasema haya, Desemba 9, 2012 pale Nkrumah Hall;
“ Msituone sisi wanasiasa tunakumbatiana mkadhani wote tunapendana. Tukivua mashati mkaangalia migongo yetu mtaona alama za mikuki!”- January Makamba

Nilikuwepo pale Nkrumah Hall, nilimsikia ndugu yangu January Makamba akiyatamka hayo. Kuna waliocheka, lakini kuna tuliobaki tukitafakari. Nitarudi kwenye tafsiri ya kauli hiyo ya January.
Lakini kwanza, nianze kwa kukiri kuwa nimechelewa kufuatilia mjadala huu hapa jukwaani juu ya ‘ Ludo kurubuniwa’ na mengineyo kuhusiana na sakata la Ludo kama anavyojulikana humu  na Lwakatare.
Ukweli nilikuwa mapumziko ya Pasaka mbugani Ruaha kwa siku kadhaa nikiwa na familia yangu. Hivyo, kuwa mbali na mitandao na habari nyingine za dunia.
 Ndugu yangu Zitto,
Umeandika yafuatayo kwenye jukwaa hili, nakunukuu;
“Nimeshtushwa sana na habari ninazoendelea kuzipata kuhusu bwana huyu. Nimesoma pia maandiko yake hapa na hasa maandiko dhidi yangu yenye maneno makali kweli. Kikweli sikujua kabisa kama bwana huyu alikuwa kitengo muhimu kama cha usalama kwenye chama changu ambacho mimi ni Naibu Katibu Mkuu.
Hata hivyo muhimu kuacha haki itendeke. Sio vema kumhukumu sasa mpaka ukweli wote ujidhihirishe.

Napenda kukumbusha kwamba Ukweli hautengenezwi, bali hutafutwa. Mwisho wa siku tutajua huyu bwana alikuwa anafanya kazi ya nani na kwa nini? Kwa nini yeye atekwe siku moja na Mhariri Kibanda na awe miongoni mwa watu wa mwanzo kufika hospitali kumwona Kibanda.

Ningependa pia ndugu yangu Maggid aweke wazi na kinaga ubaga mahusiano yake na bwana Ludovick. “
Ndugu yangu Zitto,
Nimeamua kwa makusudi kukaa kimya na kutoshiriki kuchangia au kujibu michango ya wengine na haswa linapotajwa jina langu kwa namna moja au nyingine. Nafanya hivyo sasa nikiamini, kuwa Zitto hukuwa mitandaoni, kwamba ulikuwa kambini ( JKT) na pengine hukuweza kuyasoma maelezo yangu ya ufafanuzi wa jinsi nilivyofahamiana na Ludovick na hata hatua nilizochukua  mara sakata la Ludovick na Lwakatare pale Machi 17 lilipowekwa wazi kwenye moja ya magazeti  kuwa ni ‘ tuhuma dhidi ya kushiriki kupanga njama za ugaidi’.
Ndugu yangu Zitto,
Nakufahamu zaidi wewe kama Zitto kuliko ninavyomfahamu Ludovick ambaye nilimfahamu kaka kijana mwanaharakati aliyekuwa akifuatilia makala zangu tangu jarida la Rai. Alipata kunipigia simu na kuniomba kukutana nae kama ilivyo kwa wengi ambao hupenda wakutane na kuzungumza nami mbali ya kusoma makala zangu au kunifuatilia kwenye blogu. Bila shaka hali hiyo inakukuta wewe Zitto pia.
Ni katika namna hiyo, ikatokea kwa Ludovick kunisaidia na kazi za kuingiza magazeti kwenye Mjengwablog na kunisaidia kunipelekea, kwa niaba yangu,  ankara zangu kwa Watangazaji wa kwenye Mjengwablog kama vile Vodacom na Benki ya Azania. Ni kwa sababu mimi kwa miaka kumi sasa naishi na kufanya kazi nikiwa Iringa na kwamba ofisi nyingi ziko Dar.
Ndugu yangu Zitto,
Kwa zaidi ya miaka 25 sasa, kupitia kalamu yangu ninekuwa nikifanya kazi ya jamii. Na jamii ina maana ya watu. Kuna wakati nilimwambia jamaa yangu mmoja, kuwa leo hii nikitembelea Gereza lolote lile hapa Tanzania, yumkini nitakutana na maafande wawili au watatu wa Jeshi la Magereza wanaonifahamu kupitia makala zangu pengine tangu enzi za Rai. Na kwamba, kama nitaingia kutembelea ndani gerezani, yumkini nitakutana na wafungwa hata kumi ambao wananifahamu kupitia makala zangu za tangu enzi za Rai.
Sasa nikisimama na kuongea na wafungwa hao ambao wengine wamefungwa kwa makosa ya ujambazi kuna atakayedhani kuwa Maggid huyu lazima atakuwa mhalifu na pengine jambazi, maana inakuwaje amefahamiana na wahalifu walio gerezani!
Naam, kwa kazi zetu hizi za kijamii, huwezi ukamtilia mashaka kila mwanajamii unayekutana nae barabarani, anayeongea nawe kwenye simu au anayetaka kukutana nawe mzungumze.
  1. mimi kama mtu mzima, ninapokutana na kijana wa Kitanzania anayeonyesha kufuatilia maandiko yangu na kazi zangu za kwenye blogu, kisha akaonyesha kuwa na utayari wa kunisaidia kutuma picha au ku-upload kazi za mtandaoni ikiwamo magazeti ambayo Dar yanapatikana mapema zaidi, na mimi nina shida ya usaidizi huo, ni kwa nini basi nishindwe kushukuru kujitolea kwake?
Mjengwablog inatembelewa na watu wengi. Kazi zimekuwa nyingi sana. Ni chombo cha habari kama vingine, lakini, hakifanyi mauzo kama ya magazeti na wala  hakipewi ruzuku ya Serikali,  na mara nyingi hata matangazo hatupati tukaweza kujiendesha ikiwemo kuajiri.
Hivyo, tunategemea pia watu wa kujitolea katika kuifanya kazi yetu ya kijamii. Na pale  inapopatikana posho kidogo tunawapa wanajiotolea lakini hatuwezi kuita ni  mishahara.  Ninao vijana wanaoendelea kujitolea kwenye Mjengwablog na gazeti la mtandaoni la Kwanza Jamii,  wawili wako Iringa, na kwa sasa Dar sijapata mtu wa namna hiyo. Namtafuta.
 Ndugu yangu Zitto,
 Katika Tanzania hii, kama wanahabari na wanaharakati wa mitandaoni wangepewa jukumu la kutuhumu, kukusanya ushahidi, kuendesha mashtaka na kuhukumu, basi, Watanzania wengi nikiwamo mimi nduguyo tungeshakuwa gerezani siku nyingi sana.
 Ni bahati njema vyombo vyetu vya usalama, licha ya kufuatilia ya magazetini na kwenye mitandao, vinafanya kazi zao kwa weledi. Naamini kabisa, siku ambayo vyombo vyetu vya usalama vitaona haja ya kuniita na kunihoji kuhusiana na nilivyomfahamu Ludovick, vitafanya hivyo kwa kuzingatia taaluma yao inavyowaelekeza na si kwa mashinikizo ya magazetini na mitandaoni. Mpaka sasa sijapata hata ‘ miss call’ moja  ya kutoka vyombo vya usalama, na hiyo haimaanishi kuwa hawaijui kazi yao. Kama kutakuwa na haja ya wanazo namba zangu na wanajua hata ninapoishi.
 Ndugu yangu Zitto,
Nilichojifunza kutoka kwenye kauli ya January Makamba ni ukweli, kuwa si wanasiasa tu ambao hampendani, bali hata baadhi yetu wanahabari na tunaojiiita wanaharakati hatupendani pia.
Katika hili la Ludovick na Lwakatare kuna miongoni mwetu waliohangaika na wanaozidi kuhangaika kutafuta hata ‘ link nyepesi’ tu ya kumwuingiza, kwao wao, ni  ‘ Mwanahabari na bloga maarufu Maggid Mjengwa’ kwenye hili sakata la Ludovick na Lwakatare.
Na ikiwezekana, mimi Maggid,  niorodhoshwe kama mtuhumiwa wa kupanga njama za kumdhuru Kibanda na wanahabari wengine.  Tukifika hapo ndipo kitakuwa kilele cha furaha yao. Watakunywa mvinyo na bia. Watafurahi. Halafu iweje? Unajiuliza.
Ndugu yangu Zitto,
Ndivyo Watanzania tulivyo. Tunafurahia maanguko ya wenzetu, na hasa wale tuliotoka nao chini kwenye taaluma na wakaonekana kupanda chati kwa haraka. Mimi Maggid ni raia wa kawaida tu ninayejitahidi siku zote kuishi maisha adilifu na ya kujikimu.
Lakini, kwa wengine, mimi kuwa na Mjengwablog yenye umaarufu na hata kuanzisha kijarida cha kijamii cha ‘ Kwanza Jamii’ ni nongwa kwao. Ni yale yale ya mafarisayo walipomshangaa Yesu kwa kusema; “ Hivi ni Yesu huyu huyu mwana wa Joseph Fundi Seremala?!”
Ndio, moja ya matatizo yetu ni kutokuwa na wivu wa maendeleo, bali wivu dhidi ya wenye kujaribu kupiga hatua za maendeleo.
Ndugu yangu Zitto,
Kufikiri tu wazo la kutuhumu nayo ni tuhuma. Wanaonifahamu, bila shaka nawe ukiwemo,  hawawezi  kufikiri wazo la mimi kushiriki kupanga njama ya kumdhuru mwanahabari wa Tanzania au popote pale duniani, kumdhuru  raia wa Tanzania au popote pale duniani. Ukweli huo hapo juu nilipata kumweleza ndugu yangu  Ansbert Ngurumo kupitia jukwaa hili alipohoji mimi kusitisha rasmi usaidizi wa Ludovick kwenye Mjengwa blog kuanzia Machi 17.
 Ansbert pia aliniuliza; je, kama wewe ( Maggid) utahisiwa au kutuhumiwa kuhusika na suala la Kibanda ina maana utaacha kublogu?
Ndipo nikamjibu;
Kuwa kusitisha usaidizi wa Ludovick kwenye Mjengwablog ni kumsaidia Ludovic kutokuhusishwa na yanayofanyika Mjengwablog kwa sasa ikiwamo machapisho wakati yuko kwenye kesi.
Nikasema, kuwa sisi  wenyewe ( wanahabari) kilio chetu siku zote kimekuwa kuwataka watendaji Serikalini an kwingineko wanapokumbwa na tuhuma wakae pembeni kwa maana ya kujiuzuru kupisha uchunguzi, lakini, katika hili la Ludovick hatuoni kama hilo ni muhimu!
Kwenye hoja yake ya pili nikamjibu;
Kuwa kama atatokea Mtanzania mwenye akili timamu, akatoa tuhuma dhidi yangu, mimi Maggid Mjengwa, kuwa nahusika na kuratibu au kupanga njama za kumdhuru mwanahabari wa Tanzania au popote pale duniani. Kumdhuru raia wa Tanzania au popote pale duniani, basi, hata kama atakuwa na ushahidi mmoja tu wenye mashiko, itatosha kwangu kuacha mara moja kufanya yote yale ya kijamii kwa kutumia kalamu yangu. Bahati mbaya au nzuri, ndugu yangu Ansbert hakurudi tena kuendelea na mjadala ule.
 Ndugu yangu Zitto,
 Ndio, mwenye kunifahamu hawezi kufikiri wazo la mimi kupanga njama za kumtendea uovu mwanahabari au raia wa Tanzania. Ndio maana kuna wengi pia wamenipigia simu za kunipa pole ya juu ya kilichotokea na jina langu linavyotajwa kwa dhamira ovu.
 Alfred Mwambeleko ni kijana kada wa Chama Cha Mapinduzi.  Huyu ananifahamu tangu tukiwa wote Sangu Secondary ‘ A’ Level. Yeye na mimi, tukiwa wanachama wa CCM-Youth mwishoni mwa miaka ya 80, tulishirikiana kuandaa mijadala ya wazi pale shuleni ili vijana wajizoeshe kutoa fikra zao huru mbele ya watu.
 Majuzi hapa Mwambeleko alinipigia simu nikiwa Iringa. Alisoma jarida la moja la kila wiki akiwa na wenzake kwenye ofisi ndogo ya CCM, Lumumba. Ni kuhusiana na sakata la Ludovick na Lwakatare. Alfred Alinipigia simu kunipa pole na akatamka;
 “ Nimewaambia jamaa zangu hapa, kuwa Maggid is innocent”
 Ni kwa nini basi ndugu yangu Alfred awaambie wenzake kuwa mimi ni ‘ innocent’?
 Jibu; ni kwa sababu , coverage ya jarida lile  ilionyesha kunituhumu mbele ya jamii. Na kuna jarida lingine la kila Jumapili lilifanya hivyo pia.  Niliongea na wahariri wake kuwaeleza masikitiko yangu. Walikuwa waungwana, walinielewa. Maana, huwezi kuandika fulani ni mtu wa karibu wa fulani wakati unajua kabisa maana ya ‘ Mtu wa karibu’.  Huwezi pia kuandika fulani ni mwajiriwa wa kampuni fulani wakati huna ushahidi huo na Mkurugenzi wa kampuni anapatikana kuweza kuthibitisha au kukanusha.
Ndugu yangu Zitto,
Wewe pia ni mhanga wa ninaouita  ‘Uandishi wa habari usio wa kuwajibika’. Juzi tu umekanusha habari kuu kwenye moja  ya majarida yetu ikidai kuwa kulikuwa na njama za wewe kuwekewa sumu. Ukatamka kuwa ni  Uongo Mtupu!  Nilidhani gazeti lile lingethibitisha ilichoandika ili tujue nani mkweli na nani mwongo. Halikufanyika- Irresiponsible journalism!
Imefika wakati magazeti tuliyoyategemea yatuletee habari za kina na zilizofanyiwa uchunguzi kimsingi wanatuletea ‘ udaku’. Na wenye kuandika udaku mara nyingi huwa hawataki – ku-balance story.  Kwenye udaku kubalance story ina maana ya kuua udaku wenyewe, maana hakutakuwa na story ya kidaku. Inasikitisha kwamba tumefika hapa.
Ndugu yangu Zitto,
Hata mimi nastushwa na habari ninazoendelea kuzipata kuhusu Ludovic.  Sijutii kuyafanya maamuzi niliyoyafanya ya kumsitisha  mara moja Ludovic kufanya usaidizi kwenye Mjengwablog.
Inatosha tu mtu kutuhumiwa ili kuchukua hatua. Ni kumpa nafasi pia mtuhumiwa, ni kumsaidia. Ni wajibu wa kiraia. Kizalendo.
Pale Oyesterbay Police kuna rekodi yangu ya kumripoti mdogo wangu wa tumbo moja; baba mmoja  na mama mmoja, kwa kutuhumiwa kutenda kosa la jinai.
Ni miaka kadhaa iliyopita, nilimkamata na kumpeleka mwenyewe kituoni akaandikishwe maelezo na afunguliwe mashtaka na Jamhuri.
Ndugu zangu hawakuinelewa. Lakini leo wamenielewa. Kuwa kijana yule ndugu wa damu sasa amejitahidi kuwa  raia mwema. Hajapatikana na makosa mengine ya jinai. Na kijana mwenyewe, kwa maana ya mdogo wangu, anatambua sasa kuwa nilimsaidia.
Nayasema nikiwa na maana, hakuna Mtanzania au mtu mwingine yeyote ninayeweza kushirikiana nae kufanya uhalifu au kumlinda nikigundua kuwa amefanya uhalifu. Nitamripoti.
Siku ile ya Desemba 9, pale Nkrumah nami nilipata fursa ya kuongea. Nilizungumzia mambo mamkubwa mawili; haki na wajibu.
Nikatoa mfano wa kisa cha aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani wa Uingereza wakati wa Tony Blair, aliitwa Jack Straw.
Ilitokea asubuhi moja, Jack Straw alisoma gazetini kuwa mtoto wa Waziri wa Mambo ya Ndani amewatoroka maaskari wa barabarani baada ya kutenda kosa la barabarani.
Jack Straw baada ya kusoma hayo, akamchukua mwenyewe mtoto wake na kumpeleka kituo cha polisi. Waandishi wa habari walikusanyika kutaka kumsikia Waziri mwenye dhamana ya Usalama.
Jack Straw akatamka; “ Nimemkabidhi mwanangu kwenye mikono ya polisi, nikiamini kuwa atashughulikiwa kwa mujibu wa sheria za nchi bila kujali kuwa ni mtoto wa Waziri wa Mambo ya Ndani. Lakini, nimewaambia pia Polisi, kuwa wasimkandamize mwanangu , kwa vile tu ni mtoto wa Waziri wa Mambo ya Ndani.”- Jack Straw.
Hapo tuna ya kujifunza juu ya haki na wajibu.
Ndugu yangu Zitto,
Nimeandika sana. Lakini nimalizie na kauli yako  kuwa; Ukweli hautengenezwi, bali hutafutwa”. Ni sahihi kabisa.
Lakini labda nichokoze swali la kufikirisha; Tunafanyaje basi pale tunapotambua ukweli mwingine, kuwa, kwa wengine, ukweli wanauumba. That, they are simply crafting lies!
Sijaufunga mjadala, ingawa sitajadili yaliyo mahakamani.
Maggid Mjengwa,
Iringa
Next Post Previous Post
Bukobawadau