Ni CCM dhidi ya matakwa ya walio wengi
Na Prudence Karugendo
MONGOSUTHU
(Gatsha) Buthelezi, ni mtawala wa kikabila (Chifu) wa kabila mojawapo pana
katika jamii wa Wazulu, KwaZulu – Natal, nchini Afrika Kusini. Kutokana na
kunogewa na utawala huo wa kijadi usio na aina yoyote ya demokrasia ndani yake,
ilifikia wakati Buthelezi akaungana na makaburu wa Afrika Kusini kuzipiga vita
harakati za wazalendo wa nchi hiyo za kuuondoa utawala wa kikaburu.
Makaburu ni
watu weupe waliokuwa wanajinufaisha na utajiri wa Afrika Kusini kwa mabavu
wakiwa wahamiaji toka Ughaibuni, huku wakiwa wamewatenga wazalendo wa nchi hiyo
na kuwafanya watu wa daraja la tatu.
Lakini
Buthelezi sio mweupe, ila alishawishika kuwa kibaraka wa weupe, wakati fulani, ili kuilinda hadhi yake iliyokuwa inapatikana
kwa njia zisizo za kidemokrasia sawa na za makaburu walizozitumia kujipa
ukubwa.
Kwa ufupi ni
kwamba Buthelezi aliiogopa demokrasia kwa hofu ya kwamba pengine ingesababisha
yeye kupokonywa kile alichokipata nje ya matakwa ya walio wengi. Maana kanuni
kuu ya demokrasia ni kuyaheshimu matakwa ya walio wengi.
Hapa nchini
kwetu kwa sasa wameanza kujitokeza akina Buthelezi wasio na idadi. Watu hao
wanaonekana kuzipinga kwa nguvu zote harakati zinazoendelea nchini za kuijenga
demokrasia ya vyama vingi. Wamejibanza kwa chama kimoja, chama tawala, na
kukipigia debe eti kitawale milele sawa na Buthelezi alivyokuwa akijipendekeza,
kiusaliti, kwa makaburu na kuwaombea
waitawale Afrika Kusini milele yote.
Wabaya hao
wa demokrasia wanaufanya usaliti wao huo wakiwa wamejikinga kwenye kivuli cha
CCM na kuonyesha kwamba wanakipenda sana chama hicho. Na chama hicho tawala,
kama walivyokuwa makaburu wa Afrika Kusini, kinaamini kwamba ndicho pekee
kilicho na haki ya kuitawala Tanzania pasipo kukiachia chama kingine chochote.
Lakini
hatahivyo, sio kweli kwamba CCM hakiujui ukweli unaowafanya wananchi waitamani
demokrasia, kinaujua sana. Ndiyo maana mpaka sasa, miaka 50 tangu nchi yetu
ianze kujiongoza chenyewe kikiwa ndicho pekee kilichoushikilia usukani, bado
kinadiriki kutamka kwamba nchi yetu bado ni changa! Sijui ni uchanga gani huo
wa zaidi ya miaka 50!
Kwahiyo kwa
kulielewa hilo CCM inaiangalia demokrasia kama adui yake namba moja, sababu
demokrasia itawawezesha Watanzania kumbadilisha mshika usukani na kumuondoa
huyu anayeifanya nchi iendelee kuwa changa hata baada ya zaidi ya miaka 50.
Ikumbukwe
kwamba maendeleo yoyote hutokana na mabadiliko. Kitu kisicho na mabadiliko
hudumaa, na katika udumavu hakuwezi kupatikana maendeleo.
Hata katika
mwili wa binadamu, udumavu wowote katika viuongo vya binadamu uweza kusababisha
ugonjwa wa saratani na baadaye kifo. Udumavu hauwezi kwa njia yoyote kumsaidia
mwanadamu.
Tanzania
kuendelea kutawaliwa na CCM ni kuukumbatia udumavu na kuyakataa maendeleo.
Tanzania kuendelea kutawaliwa na CCM ni kuwa tayari kuendelea na uchanga milele
yote.
Nchi zote
zilizoendelea duniani zimefanikiwa kutokana na kuyakubali mabadiliko.
Mabadiliko yanayoongozwa na demokrasia inayoyaheshimu matakwa ya watu. Hakuna
nchi hata moja iliyowahi kuendelea kwa kuung’ang’ania udumavu unaoletwa na hofu
ya mabadiliko.
Tuziangalie
nchi kama Marekani, Uingereza, Canada, Japan na zote tunazoziendea na kuzipigia
magoti ili zitusaidie. Hakuna hata moja iliyowahi kuendekeza udumavu kwa
kuyaogopa mabadiliko.
Tunaona
jinsi nchi hizo zinavyofanya mabadiliko karibu kila wakati wa mabadiliko
(uchaguzi) ukifika.
Historia
inatuonyesha kwamba zipo nchi ambazo watu wake walilazimika kufanya mapinduzi
ya nguvu ya umma baada ya watawala wao kunogewa kutawala na hivyo kuyaogopa
mabadiliko ambayo walihisi yangeweza kuwasababishia kupokonywa utawala wao.
Baada ya wananchi kuona watawala wao wanawadumaza huku mambo yakienda hovyo
wakaamua kuunganisha nguvu zao na kufanya mabadiliko ya lazima, mapinduzi.
Nchi
mojawapo iliyoshuhudia wananchi wanalazimisha mabadiliko kinyume na matakwa ya
watawala ni Ufaransa, katika mapinduzi
yaliyotokea kati ya mwaka 1787 – 99.
Bila ya
mabadiliko hayo ya kulazimisha si ajabu Ufaranza tungekuwa nayo kundi moja kwa
sasa, katika kundi la nchi zilizodumaa zikidai ni nchi changa.
Kwahiyo
tutaona kwamba mabadiliko ni ya lazima katika jamii. Na mabadiliko yoyote ni
haki ya wanajamii pasipo kutokea mtu wa kuihodhi haki hiyo.
Kwa
kuliangalia hilo, kwamba ukosefu wa mabadiliko ndio unaozifanya baadhi ya nchi
kukosa kujimudu, ndipo nchi tunazoziita za wahisani zikalazimika kuweka
shinikizo la kila nchi kuwa na demokrasia ya vyama vingi kama njia mojawapo ya
kuzisaidia nchi zilizodumaa kuondokana na udumavu. Nchi zilizodumaa
ziliyahitaji mabadiliko. Demokrasia ya vyama vingi ni njia mojawapo ya
kuyaelekea mabadiliko.
Hapa
Tanzania, pamoja na kuikubali kwa shingo
upande demokrasia ya vyama vingi, bado mabadiliko yanaonekana kuleta hofu kuu,
hasa kwa chama tawala. Watawala walio madarakani chini ya CCM wanaonekana
kutoyaelewa majaliwa yao ndani ya mabadiliko yanayoweza kuletwa na demokrasia
ya vyama vingi.
Udumavu
tulio nao kisiasa unajionyesha kwa njia hiyo. Watawala wetu hawajawa tayari
kuyapokea mabadiliko yatakayowafanya wao kuwa pembeni huku wengine wakitawala.
Bado wana kasumba kama ile ya makaburu ya kwamba mtu mweusi hawezi kuongoza
nchi hasa inayokaliwa na wazungu. Ndiyo maana tunasikia kauli za kwamba CCM
itatawala kwa karne nyingi zijazo pamoja na ukweli wa kwamba chama hicho
kimeidumaza nchi yetu, miaka zaidi ya 50 ya kujitawala bado inajiita nchi
changa!
Ni kwa
sababu hiyo tunakiona Chama Cha Mapinduzi kikifanya kila linalowezekana na
lisilowezekana kuhakikisha mabadiliko yanayoweza kukiondoa madarakani
hayafanikiwi. Kwa sasa tunaona hila za ajabuajabu zinazofanyika na nyingine
kuonekana ni za hatari ilmradi tu zinaweza kukisaidia chama hicho kubaki
madarakani.
Jambo la
kujiuliza ni kwa nini CCM itawale zaidi ya miaka 50 huku nchi ikiendelea
kuonekana changa na ombaomba lakini chama hicho kikose ujasiri wa kuyatamani
mabadiliko na kutamani kuendelea kutawala chenyewe? Kwa nini CCM kiendelee
kutamani kutawala katika hali kama hii ya kutia aibu? Kinatawala kikiwa
kinawathamini Watanzania au kinatawala kikiwa kimewafanya Watanzania watu wa
daraja la tatu kama makaburu walivyokuwa wanawachukulia wazalendo wa Afrika
Kusini?
Nitoe mfano
wa mtu aliyeithamini nchi yake na watu wake; Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, ulifika wakati Mwalimu akasema kwamba
aliyoyafanya kwa nchi yake na watu wake yalikuwa yanatosha. Akasema kwamba
ulikuwa wakati wa mtu mwingine kujitokeza na kujaribu, akasema kwamba angependa
kuona mtu mwingine anajaribu kuiongoza nchi yake, na pengine kuzidisha au kusahihisha pale
ambapo yeye alishindwa. Huyo aliithamini nchi yake na kuitakia mema. Je, kwa
nini CCM inashindwa kufanya hivyo kama kweli inaitakia mema nchi hii?
Wakati CCM
kikijiona kuwa ndicho chama teule kinachopaswa kuitawala nchi yetu bila
kukipisha kingine, kama ilivyokuwa imani ya makaburu kwa nchi ya Afrika Kusini,
vilevile wapo kina Buthelezi wanaokiunga mkono chama hicho ili kitawale milele
bila sababu yoyote wanayoweza kuionyesha kwa umma kwa nini wanafanya hivyo.
Katika zaidi
ya miaka 50 CCM kimeshindwa kuifanya nchi yetu kuwa komavu inayoweza
kujitegemea. Kwahiyo ipo haja gani ya chama hicho kuwafanya wananchi wayaogope
mabadiliko? Na wanaokiunga mkono wanalo lipi la kutushawishi tuendelee kukiona
kuwa ndicho pekee kinachoweza wakati ukweli tunauona kuwa chama hicho
kimeshindwa tena vibaya?
Kama CCM
ingekuwa na nia njema na nchi hii, kama alivyokuwa Mwalimu Nyerere, ingekubali
bila woga wowote kuwaacha wananchi
wafanye mabadiliko kwa matakwa yao. Baada ya kipindi fulani wananchi wanaweza
kuona kuwa pengine wamepotoka, kama mabadiliko yao yatakuwa yameenda mrama na
kushindwa kuzaa matunda yaliyokusudiwa, na hivyo kuamua kukirudisha CCM kwenye
usukani. Hiyo ndiyo demokrasia, kufanya mabadiliko yenye mwelekeo wa maendeleo bila
mizengwe wala shinikizo.
Ni kwamba
watu wanataka mabadiliko, hiyo ni haki yao. Lakini kinyume na matakwa ya wengi
CCM inataka ifanye kila mbinu kuyazuia mabadiliko hayo. Na kwa vile chama cha
siasa sio mashine, ila ni taasisi
inayoongozwa na wanadamu, naweza kuamini kwamba yanayojitokeza ni mbinu
zinazofanywa na watu wachache wakiungwa mkono na kina Buthelezi ili kuyazuia
mabadiliko yanayotakiwa na walio wengi kwa manufaa ya hao wachache.
Wakati
namalizia kuandika makala haya, msomaji mmoja wa Tanzania Daima, John Mnzajila,
wa Gairo, kanitumia ujumbe mfupi wa maandishi akisema kwamba “Bado historia ya
dunia inaonyesha kwamba chuki, fitina au uovu wowote ule kwa wengine havijawahi
kushinda popote pale toka kuumbwa kwa ulimwengu”. Tuitafakari kauli hiyo.
0784 989 512