Ubadhirifu umekithiri vyama vya ushirika, asema Waziri Chiza
Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Christopher Chiza,
amesema uchunguzi kwenye vyama vya ushirika nchini umeonyesha kuwa
ubadhirifu wa fedha na mali za wanachama ni mkubwa.
Akiwasilisha makadirio ya bajeti ya wizara yake
bungeni jana, Waziri Chiza alisema taarifa za ukaguzi zimewasilishwa
kwenye bodi za uongozi wa vyama na baadhi zimewasilishwa katika mikutano
mikuu ya vyama husika.
“Mfano, taarifa ya Chama Kikuu cha Ushirika cha
Wetcu Ltd, imewasilishwa kwenye mkutano mkuu maalumu na wanachama
wamefikia uamuzi wa kuiwajibisha bodi kwa kuiondoa madarakani na kuteua
ya muda,” alisema.
Chiza alitaja vyama vilivyofanyiwa ukaguzi maalumu
kuwa, ni Shirikisho la Vyama vya Ushirika (TFC), Chama Kilele cha
Ushirika wa Tumbaku (TTCA), Muungano wa Vyama vya Ushirika wa Akiba na
Mikopo (Sccult), Vyama Vikuu vya Ushirika vya KNCU (1984) Ltd, Wetcu
Ltd, Cetcu Ltd na Tanecu Ltd.
Vyama vingine n vya ushirika vya msingi 192
vinavyohusika na zao la tumbaku Mkoa wa Tabora na 14 vya Mkoa wa
Singida,vyama vya ushirika vya msingi vya mazao (Amcos) 97 mkoani Pwani,
18 vya Wilaya ya Tunduru, vyama vya ushirika wa Akiba na Mikop vya
Mzalendo, Kurugenzi Njombe, Mpwapwa Teachers, Fune, Gogogo, Luiche,
Kisesa na Chawampu Amcos.
Kuhusu Uwakilishi wa Bodi ya Kahawa, Waziri Chiza
alisema kumekuwa na hoja ya uwakilishi kwenye bodi hiyo na kanuni
kuruhusu uuzaji wa kahawa mbichi na kwamba, tayari amefanya mabadiliko
katika bodi.
“Serikali imefanya marekebisho katika Bodi ya
Wakurugenzi wa Kahawa kwa kuteua bodi mpya ya wakurugenzi. Pia, rasimu
ya marekebisho ya kanuni za sheria ya kahawa ya mwaka 2012 inayozingatia
kudhibiti uuzaji kahawa mbichi na kuhakikisha kahawa yote inayouzwa
inachakatwa imetayarishwa,” alisema.
Waziri Chiza alisema tathmini ya utekelezaji wa
ASDP imeonyesha kuwapo kwa fedha ambazo hazikutumika katika miaka ya
nyuma ngazi ya halmashauri.
Alisema hadi Desemba 2012 takriban Sh25.8 bilioni zilizotengwa kwa ajili ya miradi ya umwagiliaji zilikuwa hazijatumika.
“Sababu kubwa zilizochangia fedha hizo kutotumika
ni upungufu wa wahandisi na mafundi sanifu wa umwagiliaji na mtiririko
mbaya wa fedha,” alisema.