Bukobawadau

Ukaribisho Maalum wa Prof. Mama Anna Tibaijuka Ndani ya JamiiForums!



Ndugu WanaJF,

Kwa niaba ya uongozi wa JF, napenda kutumia fursa hii kumkaribisha rasmi Mh. Mama Prof. @Anna Tibaijuka hapa jamvini. Tuna imani wasomaji wa JF wanamfahamu Prof. @Anna Tibaijuka, ambaye ni Mjumbe wa Mkutano Mkuu (NEC) na Kamati Kuu ya CCM, Mbunge wa Muleba Kusini, Waziri wa Ardhi na Makazi, Mwanamama wa Kwanza Kuongoza Kurugenzi ya UNHABITAT, mwanzilishi wa Baraza la Wanawake Tanzania (BAWATA) na mengine mengi!

Mama Tibaijuka,
Jamiiforums.com ambapo watu huthubutu kusema kwa uwazi; Ndipo mahala pekee Jamii zote zinapokutana. Karibu ukutane na Jamii!

Wana JF,
Mgeni wetu anajiunga kujumuhika na Watanzania akipitia dirisha la Wanachama waliohakikiwa na kuthibitishwa (Verified Members) kutumia majina halisi. Katika kundi hili tayari tunao Watanzania wa kawaida, Watu maarufu na Wanasiasa mashuhuri ambao miongoni mwao ni @Dr F. Ndugulile, @Halima Mdee, @HKigwangalla, @Freeman A. Mbowe, @John Mnyika, @Mohammed Dewji, @Nape Nnauye, @Omari R Nundu, @Peter Msigwa, @Salome Sijaona, @Charles Kenyela, @Dr.W.Slaa, @Jerry Silaa, @Kitila Mkumbo, @Mwigulu Nchemba, @Rachel Mashishanga, n.k

Kujiunga rasmi kwa Mama Tibaijuka kwetu ni ishara njema kuwa na wengine walio katika utumishi wa umma na wenye hadhi ya juu katika Taifa letu sasa watazidi kushawishika kufuata nyayo. Uongozi wa JamiiForums unaotekeleza misingi ya usawa kwa wanachama wote, unawahakikishia ushirikiano. Pia tunazidi kuwakaribisha na kuwashauri viongozi wa Kisiasa, Serikali na Wakurugenzi wa Mashirika ya Umma wanaotembelea mtandao huu au wanaojadiliwa na wanachama wa mtandao huu, kujiunga kwa utaratibu wa majina halisi yaliyothibitishwa. Nyongeza ya hapo, tunawashauri kuchangia au kutoa majibu yaliyo ndani ya mamlaka yao katika mada/hoja zinazogusa nafasi zao.

Uzoefu hapa nchini na kwingineko duniani umebainisha kuwa Jamii ya wasomaji wa habari mara nyingi hubaki katika mtanziko (dilemma) juu ya taarifa au habari zitolewazo katika mitandao mpaka pale zinapothibitishwa na wahusika wenye mamlaka. Na katika mitandao mingine ukiachilia JamiiForums, mara nyingi tuhuma/taarifa hasi/kashfa zilizojengeka juu ya hisia zimekuwa zikisambaa kwa kasi zaidi na kujenga sura ya kuonekana kuwa ndiyo ukweli. Hivyo kujitenga na mitandao ya kijamii au kushiriki kwa majina yasiyo halisi ni mbinu aghali katika kukabiliana na tuhuma/taarifa hasi/kashfa. Mwisho wake husababisha gharama kubwa isiyo ya msingi katika kusafisha jina la mhusika au Taasisi. Ni falsafa isiyoyumba kwamba; giza huondolewa na nuru na vivyo hivyo uongo hudhihirishwa kwa kuletwa ukweli. Pamoja na jitihada yetu kubwa kuhakikisha kwa kila namna kuwa haki za wahusika/waathirika zinazingatiwa na wanachama katika kuhabarishana ndani ya Jamiiforums.com, bado suala la kuthibitisha au kukanusha linabaki kuwa ni la wahusika/waathirika (mtu au Taasisi) wanaojadiliwa ndani ya habari.

Ni furaha yetu kubwa kwamba wanachama wote wa JamiiForums na wote wanaotembelea mtandao huu wanafahamu sheria za JF na wanaijua vema dhana ya “User-Content-Generated-Website”. Hiyo ndiyo dhana itumikayo katika upashanaji habari hapa JF. Ni vema kusisitiza kwamba, yanayoandikwa katika JamiiForums ni maoni ya watumiaji wa mtandao huu na Uongozi wa JF una jukumu la kuzingatia kuwa maoni hayo yanazingatia Sheria tulizojiwekea.

Mama Tibaijuka amejiunga rasmi wakati ambapo Wana-JF na Watanzania kwa ujumla wana maswali mengi sana juu ya uporwaji wa ardhi na hatma ya migogoro ya viwanja na mashamba nchini. Ili kukidhi kiu hii tunafikiria kuandaa na kumualika Mama Tibaijuka katika Mjadala wa Ardhi. Tunaamini atatupa ushirikiano na pia Wana-JF mtaonyesha ushirikiano kama ilivyo ada yetu.

Mwisho, tunapenda kumtakia Mama @Anna Tibaijuka na Wanachama wetu wote ushiriki kamilifu unaozingatia Sheria na Taratibu tulizojiwekea katika kuanzisha, kuendeleza na kuchangia mijadala. Hatuna shaka kabisa na uvumilivu mkubwa wa Mama Tibaijuka katika kukabiliana na changamoto ya mijadala na hoja za aina na uzito wowote kutoka kwa Wana JF.

JamiiForums! 
Next Post Previous Post
Bukobawadau