Bukobawadau

Viongozi wa Bunge watakosaje uadilifu na kuwataka wenzao wawe waadilifu?

Na Prudence Karugendo
MZEE mmoja ambaye ni mgonjwa wa akili katika kijiji cha Buleza, Muleba, mkoani Kagera, siku moja alifikishwa mahakamani, katika Mahamaka ya Mwanzo, mjini Muleba,  kwa kosa la kumjeruhi kwa kumpiga na jiwe mtoto wa jirani yake. Mzee huyo mgonjwa wa akili alifanya kosa hilo kutokana na watoto kumtania mara kwa mara kwa kumuita jina ambalo alikuwa halitaki.
Baada ya hakimu kumsomea mashitaka yake, mzee huyo, ambaye bado alikuwa anaonekana kajawa na hasira, hasira zake zote akazihamishia kwa hakimu. Akamwambai hakimu “huna adabu, yaani wewe mtoto ni wa kuniambia mimi nashitakiwa kwa kosa? Kwanza hujaniamkia, hujui mimi nimewalea kuanzia baba yako, mama yako na wewe mwenyewe? Baba yako na mama yako wakiniona wananiamkia, wewe huniamkii! Umetuna tu kwenye meza hapo na kuniambia eti nashitakiwa kwa kosa! Hujui huyu mtoto kanitukana? Au nimfuate hapo alipo nikamtandike viboko mbele yako? Na kwa maneno uliyoniambia tayari na wewe umenitukana, bahati yako sina jiwe hapa,  hata wewe ningekutandika nalo hapohapo ulipo”. Mara huyo akaondoka zake bila kusubiri kauli ya hakimu.
Hakimu akasema jamani mnamuona huyu mzee alivyo mgonjwa wa akili, inabidi muwe makini naye na kujihadhari kutomchokoza. Kesi ikawa imeisha.
Kwa namna yoyote kesi hiyo ya mgonjwa wa akili hatuwezi tukaifananisha hata kidogo na haya yanayowapata wabunge wetu. Yanayowapata wabunge wetu yanafanywa na watu wenye akili zao timamu. Wanayafanya wakiwa wanaelewa kwamba wanapindisha mambo makusudi kwa lengo fulani.
Nimeandika mara kadhaa nikilalamika kwamba wanayotendewa wawakilishi wa wananchi, wabunge, siyo. Wananchi hawawatumi Bungeni wawakilishi wao ili wakafundwe, wakafundishwe adabu na maadili, hapana. Hilo sio lengo la wananchi kupiga kura kuwachagua wabunge wao. Bunge halipo kufundisha adabu na maadili.
Kinyume chake ni kwamba Bunge lipo ili kuwapa wananchi fursa ya kuyapima maadili ya serikali yao iliyo madarakani. Pale ni mahali pa wananchi kuiwajibisha serikali yao kupitia kwa wawakilishi wao, wabunge.
Kwa mantiki hiyo basi, wasimamizi na waongozaji wa shughuli za Bunge, Spika, Naibu Spika na Wenyeviti wa Bunge, wanapaswa wawe wa kwanza kuonyesha uadilifu wao kwa kulitambua hilo, kwamba wabunge pale wametumwa na wananchi baada ya wananchi kuwa wamejiridhisha na uadilifu wao. Kwahiyo kitendo cha kusema kwamba wabunge fulani wamekosa uadilifu ni lazima kionekane kama matusi kwa wananchi wanaowakilishwa na wabunge husika, wapiga kura wao.
Fikiria mbunge anasimama kutaka kuelewa ni kwa nini barabara moja jimboni kwake haitengenezwi walau kwa kiwango cha changarawe ikaweza kupitika japo kwa kipindi cha kiangazi tu, lakini badala yake wananchi wanamuona DC wao analetewa mashangingi mawili mapya yasiyo na maana yoyote kwao, halafu mbunge huyo anaambiwa akae chini,  akigoma anatolewa nje kama mwizi eti kwa kosa la kukosa uadilifu Bungeni!
Jambo kama hilo likiangaliwa kwa umakini linatoa picha gani? Ni upande gani unaoonekana kukosa uadilifu? Mbunge anayetimiza wajibu wake au wasimamizi wa shughuli za Bunge wanaomzuia mbunge kutimiza wajibu wake?
Mara nyingi tumeshuhudia Spika wa Bunge, Naibu Spika na Wenyeviti wa Bunge, kwa nyakati tofauti, wakisimama upande wa serikali na kusaidia kuzizima kwa mabavu hoja za wabunge zinazokuwa zimeelekezwa upande wa serikali na kuonekana kuwa serilaki haina uwezo wa kuzitolea ufafanuzi. Je, huo ni uadilifu?
Bahati mbaya wasimamizi wote wa shughuli za Bunge ni makada wa chama tawala, chama kinachounda serikali iliyo madarakani inayotakiwa kuwajibishwa na wabunge kwa niaba ya wananchi. Sasa makada hao wa chama tawala wanapowazuia wabunge kutimiza wajibu wao wanatenda uadilifu?
Kwahiyo kinachoonekana kama ukosefu wa uadilifu wa baadhi ya wabunge wanapokuwa Bungeni hakinabudi kuonekana kwamba kinatokana na uendeshwaji wa Bunge lenyewe. Maana haiwezekani Spika, Naibu Spika au Mwenyekiti wa Bunge amkaripie mwakilishi wa wananchi kana kwamba anamkaripia mtumishi wake wa ndani halafu itegemewe kwamba uadilifu utaendelea kuwemo ndani ya Bunge.
Wanaopaswa kuulinda uadilifu ndani ya Bunge ndio wanaokuwa wa kwanza kuuvunja kutokana na madaraka waliyopewa kugeuka kilevi kinachowasahaulisha waliomo ndani ya Bunge ni watu wa aina gani na wana majukumu gani!
Katika kuhakikisha Bunge linaendesha shughuli zake kwa uadilifu zilitungwa Kanuni za Bunge. Lakini tumeshuhudia kanuni hizo zikipindishwa kwa makusudi ili ziwapendelee baadhi ya waliomo Bungeni huku zikiwabana wengine kinyume na utaratibu. Hayo yote tunayashuhudia kwa uchungu mkubwa tukiwa hatuna jinsi kama vile Bunge ni chombo kinachomilikiwa na watu walio nje ya jamii yetu! Na pengine, kwa kulijua hilo, ndiyo sababu uongozi wa  Bunge ulikuwa umefikiria kwamba Bunge liendeshe shughuli zake kwa kificho. Je, hapo kuna uadilifu gani?
Bunge ni sehemu inayopaswa kutofungamana na itikadi yoyote ya kisiasa, ni sehemu ya wananchi wote katika utofauti wao wa kiitikadi. Lakini sivyo ambavyo imekuwa ikiendeshwa. Bunge limegeuka sehemu ya kukomoana kiitikadi! Na hiyo imechangiwa kwa kiasi kikubwa na uongozi wa Bunge. Kuna uadilifu hapo?
Kwa vile wanaoendesha Bunge ni makada wa chama tawala ni nadra sana kusikia wabunge walioingia Bungeni kwa tiketi ya chama tawala wakiulalamikia utaratibu unaotumika Bungeni wakati wa vikao. Hii maana yake ni kwamba wabunge wa chama tawala wana upendeleo wa aina yake wanaoupata toka kwa viongozi wa Bunge ambao ni makada wa chama chao.
Tatizo letu, Waswahili, hupendelea kuangalia upande mmoja tu bila kuhangaika na upande wa pili ili kujua kukoje. Ni kwamba kila kitu mara zote huwa na uzuri na ubaya wake. Wakati baadhi yetu wakiufurahia utaratibu huu batili wa chama tawala kujipendelea kwa kila kitu, upo usahaulifu wa kwamba kila kizuri kina ubaya wake.
Ubaya wa tabia hiyo unaweza kuonekana pale tabia hiyo ya chama tawala kujipendelea inapokuwa ya mwendelezo kwa njia ya kulipiza kisasi pale mambo yanapokuwa yamebadilika, chama tawala kikageuka cha upinzani, na hivyo kuzidi kuuathiri uwakilishi wa wananchi. Ni kwamba chama kitakachokuwa kinatawala ni lazima nacho kitataka kufanya yaleyale ya chama kilichokitangulia.
Mwisho tujiulize, wawakilishi wa wananchi wanapochachamaa kutaka kieleweke, kama wajibu wao unavyowataka, wakaitwa wakajieleze kwenye Kamati ya Haki, Kinga na Maadili ya Bunge, ambayo tena kwa bahati mbaya haipo, muda wake umeisha, si yanakuwa yaleyale ya mgonjwa wa akili aliyemwambia hakimu kuwa hana adabu kumwambia kuwa anashitakiwa kwa kosa la kumjeruhi mtoto kwa jiwe? Maana wawakilishi wa wananchi wanahoji halafu nao wanaitwa wakahojiwe kwa nini wamehoji! Wanaonekana hawana adabu kwa kutimiza majukumu yao ipasavyo sawa na hakimu aliyekosa adabu kwa kumsomea mgonjwa wa akili shitaka lake.
0784 989 512
Next Post Previous Post
Bukobawadau