Bukobawadau

Kona ya Karugendo Tatizo la maji Tanzania ni janga la kitaifa

KWA muda mrefu Serikali ya Tanzania imekuwa ikitangaza kwamba huduma ya maji safi na salama vijijini imefikia asilimia 57.  Lakini hivi karibuni kwenye kongamano la wadau wa maji, serikali imekiri asilimia 40 ndiyo inafikiwa huduma ya maji safi na salama vijijini na kwamba magonjwa ya kuharisha na mengine yanayotokana na tatizo hili yanachukua uhai wa watoto 20,000 kila mwaka. Kama takwimu hizi ni za kweli basi,  hatuwezi kuwa na kigugumizi kutangaza tatizo la maji ni janga la kitaifa.
Tunataka tusitake, tatizo la maji katika taifa letu ni janga la kitaifa ambalo labda litakuwa baya kuliko majanga yote tunayoyajua.
Inawezekana kabisa janga hili liko juu ya uwezo wetu, maana tatizo la maji ni tatizo la dunia nzima na wachambuzi wa suala hili la maji wanaonya tusipokuwa waangalifu kutunza mazingira yetu, kuna hatari  tatizo la maji likatuingiza kwenye vita ya tatu ya dunia; itakuwa ni vita ya kugombea maji lakini pia kuna uwezekano mkubwa hili ni janga la kujitakia kutokana na kuzingatia ukweli kwamba, Tanzania imepata misaada mingi kuboresha sekta ya maji lakini tija ni finyu mno.
Miradi mingi imeanzishwa, lakini cha kushangaza asilimia 46 ya miradi hiyo haifanyi kazi. Malengo ya milenia ni kwamba kufikia 2015, asilimia 65 ya watu vijijini wapate maji safi na salama na asilimia 90 mijini wapate maji safi na salama. Lakini hadi sasa malengo haya bado hajafikiwa. Tatizo nini?
Utafiti juu ya usambazaji wa maji safi na salama vijijini uliofanyika hivi karibuni kwenye nchi 13 zinazoendelea, umeonyesha kwamba  tatizo la kutoa huduma ya maji safi na salama ni kubwa na kwamba matatizo yanayokwamisha maendeleo ya miradi ya maji kati ya nchi hizi yanafanana.
Matatizo hayo ni serikali za nchi hizi kushindwa kupeleka madaraka kwa wananchi, miradi ya maji kupangwa na kupelekwa vijijini kutoka juu na kwenda chini, badala ya miradi hii kuanzia chini kwa wananchi na kwenda juu, majukumu ya wadau wote kwenye miradi hii ya maji kuwekwa wazi, serikali za mitaa kutokuwa na uwezo wa kuendesha miradi hii, sera nzuri za maji, bila utekelezaji, miradi hii kutegemea kwa kiasi kikubwa misaada kutoka nje, wananchi kutokuwa na uwezo wa kuendesha miradi hii ya maji kwa ufanisi.
Hivyo, kwa upande Tanzania tunaweza kupambana na janga hili la kitaifa, kama tunaweza kutafuta majibu ya changamoto ya miradi endelevu ya maji. Kwa kifupi changamoto kubwa inayoikumba miradi ya maji hapa Tanzania ni utatu mtakatifu wa uwajibikaji, ushirikishwaji na uwezeshwaji.
Kama serikali ingewajibika ipasavyo na kutambua kwamba wajibu wake si sera na kuisimamia  tu miradi ya maji, bali ni kuhakikisha inawashirikisha, kuwawezesha na kuwajengea uwezo watu wa vijijini kuiendesha na kuisimamia miradi ya maji, matokeo yangekuwa mazuri.
Hoja inayojengwa kwamba mipango ya kupeleka maji vijijini inatoka juu na kwenda chini, badala ya kutoka chini na kwenda juu, inalenga kuonyesha kabla ya kupeleka maji vijijini ni muhimu wananchi wenyewe kupanga na kujiandaa kuipokea miradi hiyo; inawezekana serikali inawapelekea wananchi maji wakati wao tatizo lao ni kupata trekta au kujengewa shule.
Hoja hizi na nyingine nyingi juu ya miradi endelevu ya kusambaza maji safi na salama vijijini zilijadiliwa Mei 14, 2013 katika kongamano la wadau katika sekta ya maji lililoandaliwa na ubalozi wa Uholanzi kwa kushirikiana na Shirika la Maendeleo la Uholanzi SNV.
Kwa miaka mingi sasa, ubalozi wa Uholanzi na shirika hilo la maendeleo la Uholanzi, wamekuwa wakisaidia sekta ya maji katika wilaya 26 za Tanzania; kwa kuwajengea wananchi uwezo na kuisaidia miradi ya maji vijijini. Na wala haya si malalamiko au kumnyoshea mtu kidole, na si ukweli kwamba hakuna mafanikio, kuna miradi ya maji inaendelea vizuri na mingine imekufa kabisa, hoja ni je, tunaweza kufanya ili miradi hii iwe endelevu? Mashirika ya misaada yakijitoa, miradi hii ya maji itakuwaje?
Lengo kuu la mkutano huu ni kujadili kwa kina umuhimu na upana wa dhana ya uendelevu wa huduma ya maji vijijini.  Miradi mingi inapojengwa na kukamilika inafanya kazi kwa muda mfupi na hivyo haitoi huduma endelevu. Mkutano huu pia ulitoa fursa ya kubadilishana uzoefu juu ya umuhimu wa suala la uwajibikaji wa kila mdau katika kuboresha upatikanaji endelevu wa huduma ya maji.
Kongamano hili lilifunguliwa na Waziri wa Maji, Profesa Jumanne Maghembe, ambaye alisisitiza  umuhimu wa kuwa na miradi endelevu ya maji.
Katika hotuba yake ya ufunguzi, Maghembe alisema; “Tunahitaji kuwajengea uwezo wananchi ambao tunawapatia huduma ya maji ili watimize wajibu wao katika kuifanya miradi hiyo iwe endelevu. Tunapoandaa miradi lazima tufikirie wale ambao watalipia huduma na uwezo wao wa kulipia,”
Na kwamba;  “Vyombo vya watumiaji maji vinakosa uelewa, kwa mfano kutokana na kukosekana uelewa, utashi wa kumiliki miradi ya maji unakosekana. Vyombo vya watumiaji maji vinatakiwa si kuanzishwa na kusajiliwa tu bali pia kujengewa uwezo. Na vyombo hivi vya watumiaji maji vikisimamiwa vinaweza kufanya kazi kwa ufanisi.’’
Hata hivyo, ushuhuda mwingi uliotolewa kwenye kongamano hili ni kwamba miradi mingi ya maji vijijini imekufa au imekwama kabisa. Miundombinu imechakaa na hakuna mpango wa kuikarabati, vyanzo vya maji vimekauka kwa vile watu hawatunzi mazingira, sehemu ambapo maji yanasukumwa na mashine zinazotumia mafuta, kuna tatizo la kupata mafuta hayo na kama ni umeme kuna tatizo la kulipa bili ya umeme! Na wakati mwingine wataalamu wa maji kutoka wilayani hawana magari au mafuta ya kufikisha kwenye vyanzo vya maji ili kutoa huduma.
Kinachojitokeza ni kwamba bila ushirikiano wa serikali, mashirika ya misaada, wadau wote wa maji na wananchi itakuwa vigumu kutengeneza miradi endelevu ya maji. Na ikumbukwe kwamba bila maji safi na salama, afya za Watanzania wengi na hasa watoto itakuwa hatarini. Utatu mtakatifu wa uwajibikaji, ushirikishwaji na uwezeshwaji, ukifanya kazi kwa pamoja na kuweka wazi umilikaji wa miradi hii ya maji ni lazima miradi hii iwe endelevu, kinyume cha hapo ni kutwangia maji kwenye kinu!
Serikali yetu ni lazima iwe bunifu kama ilivyofanya Serikali ya Rwanda kwa kutunga sheria juu ya maji ya mvua. Nchini Rwanda ni kosa la jinai kushindwa kuyakinga maji ya mvua na kuyaruhusu kutiririka kwenda kwa jirani au kwenda barabarani. Sheria hii imemuwezesha kila Mnyarwanda kukinga maji ya mvua na matokeo yake sasa kila Mnyarwanda anaweza kupata maji safi na salama mwaka nzima.
Hapana shaka kwamba sheria hii ya maji ya mvua inaufanya mradi huu kuwa endelevu. Sheria hii ya Rwanda, inasukuma uwajibikaji, kwa njia moja ama nyingine inashirikisha wananchi juu ya suala zima la kuvuna maji ya mvua. Serikali kwa kiasi kikubwa imewezesha wananchi wake kujenga nyumba za bati na kuachana nyumba za nyasi hivyo kuweza kuvuna maji ya mvua bila matatizo makubwa.
Sehemu za Tanzania ambazo zina mvua nyingi na zina matatizo ya maji  safi na salama, kwa nini serikali kwa kushirikiana na wadau wa maji na mashirika ya kimataifa isiwawezeshe watu kuvuna maji ya mvua na kuwa na uhakika wa kupata maji safi na salama? Haiwezekani mradi wa kuvuna maji ya mvua usiwe endelevu!
Next Post Previous Post
Bukobawadau