Bukobawadau

Mwalimu Songea ajifungua watoto watano chanzo Gazeti la Mwananchi.

Songea. Mwalimu wa Shule ya Sekondari Luwawasi iliyopo Manispaa ya Songea, Sophia Mgaya (28) amejifungua kwa njia ya upasuaji watoto watano jana asubuhi katika Hospitali ya Rufaa ya Songea ambapo watatu kati yao ni wa kiume na wawili wa kike.

Upasuaji huo ambao umefanywa na Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Wanawake, Dk Mgonde umefanyika kwa mafanikio ambapo ulifanywa saa 5:15 asubuhi na kumalizika 5:45 asubuhi baada ya Mwanamke huyo kugundulika akiwa na tatizo la kutanguliza kitovu wakati ujauzito wake ukiwa na miezi saba.

Akizungumza na waandishi wa habari jana katika wodi ya wajawazito hospitalini hapo, Ofisa muuguzi msaidizi Vilgilia Mselewa amesema, walimpokea mama huyo jana saa 6 mchana baada ya kufanyiwa upasuaji na hali yake pamoja na wanawe inaendelea vizuri.

Amesema, mtoto wa kwanza ni wa kike amezaliwa akiwa na gramu 730, mtoto wa pili ni wa kiume ana uzito wa gramu 810, watatu wa kiume alikuwa na gramu 670 wanne wa kiume gramu 820 na watano ni wa kike aliyekuwa na gramu 430, hali za wototo zinaendelea vizuri na wapo kwenye chumba cha watoto ambao hawajatimiza miezi.

Akizungumza hospitalini hapo na Mwananchi, Mama mzazi wa watoto hao, amesema amefurahi kupata watoto hao na anamshukuru Mwenyezi Mungu kwa upendo mkubwa aliompatia kwani alilia sana alipopoteza mwanaye wa kwanza wa kike aliyezaliwa mwaka 2010 na kufariki akiwa na miezi saba.

Aidha amewashukuru madaktari na wauguzi kwa msaada walimpatia kwani bila wao hali ingekuwa mbaya na amewataka Watanzania kuendelea kumwombea yeye na wanaye ili aweze kupata afya njema na kuweza kuwalea watoto wake kwani ana hamu ya kuwaona wakikua na kuendelea kumfariji katika maisha yake.

Naye baba mzazi wa watoto hao Zacharia James (30) mkazi wa Mkoa wa Njombe amemshukuru Mungu kwa kumpatia watoto hao.
Next Post Previous Post
Bukobawadau