Bukobawadau

Novemba 30 iwe ya mapumziko EAC-Mwinyi

Na Mtuwa Salira, EANA
 RAIS mstaafu wa Awamu ya Pili, Alhaj Ali Hassan Mwinyi, amependekeza nchi zote wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), zitangaze mapumziko ifikapo Novemba 30 kila mwaka ili kuongeza uelewa wa wananchi juu ya masuala ya mtangamano.
Novemba 30,1993 ndiyo siku ambayo Kamisheni ya Utatu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki ilizinduliwa na hatimaye kuzaliwa upya kwa jumuiya hiyo ambayo ilikufa mwaka 1977 ambapo hivi sasa tarehe hiyo huadhimishwa kama “Siku ya EAC” lakini siyo siku ya mapumziko katika nchi wananchama.
Alhaj Mwinyi aliyasema hayo hivi karibuni jijini Dar es Salaam, wakati akizindua ripoti ya
utafiti wa kwanza wa Afrika Mashariki juu ya ushiriki wa raia katika mchakato wa ushirikiano wa EAC.
Uzinduzi huo ulifanywa na Jukwaa la Dira ya Afrika Mashariki (VEAF), ambayo imebaini upo ushiriki hafifu wa raia katika mwenendo mzima wa mchakato huo.
“Nawahamasisha marais waliopo madarakani kwa sasa, kuienzi siku hii ya Novemba 30, 1993, ambayo Tume ya Utatu ya Afrika Mashariki ilizinduliwa Mjini Arusha, Hayati Mwalimu Julius Nyerere akiwemo,” alisema Alhaj Mwinyi.
Aliongeza kuwa, siku kama hiyo wananchi pamoja na mambo mengine wanaweza kufanya shughuli mbalimbali yakiwemo maonesho ya utamaduni, bidhaa za kilimo na viwanda katika majiji yote na mipakani na mwisho ya siku wananchi watakuwa na uelewa juu ya jumuiya hii.
Sehemu ya ripoti hiyo ilisema kuwa, ingawa kuanzishwa upya kwa jumuiya hiyo kulilenga iwe na misingi yake kwa wananchi, matokeo ya utafiti huo umebaini kinyume chake.
“Theluthi moja ya watu kama wa Tanzania na Kenya, hawajawahi kusikia juu ya mtangamano wa EAC, ilisema ripoti hiyo ambapo wanachama wengine wa jumuiya ni Uganda, Rwanda, Burundi.
Akizungumza katika tukio hilo, Katibu Mkuu wa zamani wa
EAC, Balozi Juma Mwapachu, alitaka mwananchi wa kawaida wahusishwe ipasavyo katika mchakato wa mtangamano.
Alisema wana Afrika Mashariki wanahitaji kueleweshwa zaidi kuhamasishwa zaidi na kuwafanya wawe wamoja,” alisema.
Naye Rolf Paasch ambaye ni Mkurugenzi Mkazi wa Shirika moja la Ujerumani la Frieddrich- Ebert-Stifstung (FES), nchini ambalo ndiyo limefadhili uzinduzi na utafiti huo, alitoa wito kwa wana Afrika Mashariki kufanya kila wanaloweza ili kuhusisha raia katika mchakato mzima wa mtangamano.
Next Post Previous Post
Bukobawadau