Bukobawadau

Rai ya Jenerali ;Nyoka akugongaye mbugani si yule umkutaye kitandani

NI vigumu kuamini mambo tunayoyashuhudia kwa kuyaona na kuyasikia. Binafsi najiuliza ni nini kimetusibu hadi tunafanya mambo yakitoto kiasi hiki? Na ni kwa nini tunaonyesha kila dalili za jamii ya watu waliokata tama kabisa na sasa wanajifanyia kila linalokuja akilini mwao… alimradi.
Siendi mbali, na wala tusiende mbali kwa sababu siku hizi huhitaji kwenda mbali kukutana na uthibitisho wa kile ambacho nimekuwa nikikisema muda wote huu, nacho ni kwamba hatuna muda wa kufanya jambo lolote kwa kulitafakari kwa makini kwa sababu tuko “transit” tukienda nisikokujua.
Tusiende mbali kwa sababu hatuhitaji kielelezo zaidi kuliko jinsi ambavyo serikali yetu iko “bize” inafanya madudu, ikihaha huku na kule ili kueleza jambo ambalo yenyewe haijalielewa. Ni dhahiri kwamba maelezo ya asiyeelewa hayawezi kumwelewesha mweleweshwaji na akaelewa.
Ni kweli kwamba tarakimu na asilimia za viwango vya watoto wetu kufeli katika mtihani wa kidato cha nne ni za kutisha kwa baadhi ya watu. Lakini hazishangazi, kwa sababu hali ya elimu tunayowapa watoto wetu ni ya kutisha. Kwa hiyo, ingawaje ni halali kwa yeyote kutishika kutokana na takwimu za mwaka jana, lakini si halali kushangaa.
Labda nijieleze kidogo. Ukiwa unatembea katika mbuga ambayo inajulikana kuwa na nyoka wengi, na ukagongwa na nyoka, utatishika bila shaka, lakini hutakiwi kushangaa kwa sababu unajua fika kwamba mbuga hiyo ni maskani ya nyoka na wewe umewaingilia katika maskani yao.
Lakini ukikodi chumba katika hoteli ya nyota tano, kama Serena kwa mfano, kisha wakati umelala kitandani ukajikuta umemlalia nyoka, hata asipokugonga, utatishika na kushangaa kwa mara moja.
Utatishika kwa sababu ile ile ya yule aliyetembea mbugani na akagongwa na nyoka, kwa sababu kuna hatari ya kweli ya kifo, lakini katika hoteli kama Serena utashangaa ni jinsi gani hoteli kama ile imeruhusu nyoka kitandani. Kwa kweli utakuwa na haki hata ya kushuku kwamba “wabaya” wako, kama unao, wamepanga wafanyakazi wa Serena wakutegeshee mdudu huyo hatari kama mwenza wako wa usiku. 
Sasa, kuhusu matokeo mabaya ya kidato cha nne, tunashangaa nini? Au tunataka kusema kwamba hatukujua kwamba hali ni mbaya katika shule zetu na kwamba elimu tunayowapa watoto wetu haifai hata kuwafanya wapagazi wa watu wa mataifa mengine?
Au ni kwamba tunajua fika kwamba mambo ni mabaya sana katika shule zetu, kwamba mfumo wa elimu ulikwishakusambaratika kitambo na kwamba watoto wengi wanahitimu na kutoka shuleni wakiwa mbumbumbu kama walivyoingia, lakini tunaamini papo hapo kwamba kwa kudra za nguvu fulani watafanya vizuri.
Najua kuna misemo mingi inayoeleza mtazamo kama huu, kama vile “kuvuna usichopanda” na kadhalika. Lakini kwangu ni kukosa uaminifu kwa nafsi zetu, na tunajidanganya sisi wenyewe iwapo tutaamini kwamba tutazembea kufanya wajibu wetu na bado tufanikiwe.
Hii pia ni aina ya ufisadi, kwa maana ya neno la Kiingereza “corruption.” Ni ufisadi kuwaona wenzako wanafanya kazi kwa nguvu,  bidii na maarifa wakati wewe umelala ama unalewa na kisha utaraji kuvuna sawa na wao wanavyovuna.
Aidha ni aina ya ushirikina, kama ambavyo nilikwishakueleza katika safu hii huko nyuma. Siwezi kushangaa nikiambiwa kwamba wazazi na watoto wa nchi hii wanaamndamana kwenda Mlingotini kutafuta “fundi’ wakufanya mambo ili watoto wapate kufaulu katika mitihani.
Kwa jinsi hii haiwezi kunishangaza kwamba tumetambuliwa barani Afrika kama vinara wa waumini wa uchawi. Ungedhani kwamba taarifa kama hizi zingewasumbua watawala wetu, na tungesikia ni nini wanapendekeza tufanya kuondoa picha hii. Kusema kweli ni picha inayolidhalilisha Taifa letu.
Kama unataka kutishika zaidi, fikiria kwamba watoto wenye ulemavu wa ngozi, albino, wamo hatarini hapa nchini kila wanakokua kwa sababu ule ujuha tulioulea kwa miongo kadhaa sasa umekomaa na umerudi kututesa kwa maumivu makubwa na aibu kubwa kwetu sote. Haipendezi kutembea duniani ukijulikana kwamba unatoka nchi ya wachinjaji wa albino kwa imani kwamba viungo vya masikini hawa vinaweza kuleta bahati na mafanikio yasiyotokana na kazi ya mhusika.
Sasa najiuliza, ni watoto wangapi mazuzu ambao nao wana wazazi wao mazuzu vivyo hivyo, ambao wanaweza kuwaambia wazazi wao wawafanyie mpango wapate viungo vya albino ili waweze kufaulu katika mtihani ujao? Labda viungo vya albino wanaosoma nao katika darasa moja au shule moja, au shule ya jirani? Nasema tutafakari.
Nchi ikiishakujiachia ikatawaliwa na ushirikina wa aina mbalimbali, (na washirikina wengi hawajijui kuwa ni washiriki na kwa sababu ushiriki na wako ndiyo imani ya mwenzio) inakuwa imepotea na hakuna njia yoyote kwa nchi kama hiyo kuendelea.
Anayebisha na anionyeshe nchi moja tu ambayo watu wake walio wengi ni washirikina wasiotaka kujua (ila kuamini tu) na ambayo imepiga hatua za maendeleo endelevu, hata kama inazo rasilimali kubwa.
Ushirikina hauhitaji kuwa na sanamu za mizimu chumba kwako au kucheza uchi na madogoli (alama za dini za mababu zetu), bali unaweza pia kupatikana katika kuamini katika mizungu, mambo yasiyokuwa na mashiko. Kwa maneno mengine ni kushindwa kutafakari kwa kina matatizo yetu na badala yake tukakimbilia majibu rahisi kwa maswali magumu.
Watoto wamefeli vibaya, na sisi tunasema jibu lake ni nini? Moja, wachape viboko. Pili, kwa kweli ukiangalia vyema hawajafeli bali mitihani yao ilisahihishwa vibaya na alama zao hazikupangwa sawa sawa. Kwa hiyo? Badilisha alama zao ili wengi wapasi. Ushirikina
Next Post Previous Post
Bukobawadau