Bukobawadau

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

TAARIFA YA TEF KUHUSU MULINDWA KUSIMAMISHWA UANACHAMA
Tanzania Editors Forum
AZIKIWE STREET PLOT No. 2309/50
P.O.BOX 75206 Dar es Salaam, Tanzania

Tel: +255 22 123236
Mob: +255 715 339090, +255 767 757669

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

1. Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) katika kikao chake leo, Jumatano, Mei 15, 2013 limemsimamisha uanachama kwa muda usiojulikana, Mhariri wa Mtanzania Jumatano, Charles Mulinda. Kwa maana hiyo Mulinda ataendelea kuwa nje ya TEF hadi hapo itakapoamuliwa vinginevyo.

2. TEF imechukua uamuzi huo baada ya kupokea na kujadili kwa kina taarifa ya Kamati ndogo ya wahariri watatu ambayo iliongozwa na Mhariri wa Nipashe, Jesse Kwayu kwa ajili ya kuchunguza habari iliyochapishwa na Gazeti la Mtanzania, Jumatano Aprili 17 mwaka huu ikiwa na kichwa kisemacho “Mtandao Hatari”.

3. Habari hiyo iliwataja wahariri wawili, Ansbert Ngurumo wa Tanzania Daima na Deodatus Balile wa Jamhuri kuwa ni washirika wa Joseph Ludovick, mshitakiwa katika kesi ambayo ilikuwa ikihusishwa na ugaidi (kabla ya kubadilishwa na mahakama) lakini ikiwahusisha kwa namna moja au nyingine na tukio la kuumizwa kwa Mwenyekiti wa TEF, Absalom Kibanda.

4. Yalikuwa ni maoni ya wahariri wengi katika Mkutano wa April 18, 2013, kwamba habari hiyo ilikuwa na upungufu mkubwa kitaaluma, hivyo kuamua kuchunguza habari hiyo na kubaini iwapo kulikuwa na ukiukwaji wa maadili na misingi ya kitaaluma ya habari.

5.0 Kamati hiyo pamoja na mambo mengine ilipaswa kuchunguza yafatayo:

5.1 Kuchunguza mazingira ya kuchapishwa kwa habari hiyo na kama kulikuwa na msukumo wowote nyuma ya kuandikwa kisha kuchapishwa kwakwe.

5.2 Kuchunguza chanzo/vyanzo vya habari hiyo na kubaini kama kulikuwa na ajenda maalum.

5.3 Kuchunguza ushahidi wa tuhuma zilizotolewa dhidi ya Deo Balile na Ansbert Ngurumo (kama Mullinda) alivyokiambia kikao cha Aprili 18 kwamba alikuwa na ushahidi way ale aliyoyaandika.

5.4 Kuchunguza na kubaini iwapo habari husika ilikidhi vigezo vya kitaaluma.

6.0 Katika uchunguzi wake Kamati ilibaini yafuatayo:
6.1 Kwamba kulikuwa na ukiukwaji wa maadili ya kitaaluma katika mchakato mzima uliowezesha kuandikwa na kuchapwa kwa habari husika na kwamba habari hiyo haikuwa na sifa wala vigezo vya kihabari.

6.2 Mulinda akiwa Mhariri wa Gazeti la Tanzania Jumatano, alishindwa kuthibitisha usahihi wa taarifa hiyo na hata alipotakiwa kutoa ushahidi wa tuhuma dhidi ya wahariri aliowataja hakuweza kufanya hivyo.

6.3 Tangu kuandikwa kwake, kuhaririwa na hadi kuchapishwa kwa taarifa hiyo, hakukuwa na vikao rasmi vya wahariri ambavyo kimsingi ndivyo vinavyopaswa kufanya uamuzi kwamba ni habari gani ichapishwe na kwa vigezo gani.

6.4 Kwamba kulikuwa na nguvu (msukumo) ya ziada katika kuchapishwa kwa habari hiyo kwani taarifa kwamba habari hiyo ingechapishwa zilifahamika siku moja kabla ya kuchapishwa kwa habari yenyewe.

6.5 Kwamba Mhariri husika alithibitika kukaidi uamuzi wa TEF kwa kuendeleza mjadala huo katika Makala yake ya Mchokonozi ya Mei 8, 2013 iliyobeba kichwa cha Habari "Simba hapigani na Binadamu" huku akijua kuwa kufanya hivyo ni kuingilia Uhuru wa Kamati iliyokuwa ikiendelea na uchunguzi wa suala hilo.

7. 0 Hitimisho
7.1 Kwa kuzingatia matokeo hayo TEF inaushauri Uongozi wa New Habari (2006) Ltd na vyumba vingine vya habari kuboresha mfumo wake wa usimamizi wa uhariri ili kuziba mianya kwa habari tata kama hiyo ya "Mtandao Hatari" kupenya na kuwaumiza baadhi ya watu bila kuwapo kwa uthibitisho wa tuhuma husika.

7.2 TEF inaendelea kuchukua hatua nyingine za ndani kuimarisha usimamizi wa nidhamu na maadili kwa wahariri ikiwa na itaendelea kuchukua hatua dhidi ya ukiukwaji wowote ule wa kitaaluma utakaofanywa katika vyombo vya habari.

Imetolewa na Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF)
Dar es Salaam, Mei 15, 2013
Next Post Previous Post
Bukobawadau