Bukobawadau

KISA CHA KAKA ALIYEMUUA DADA YAKE

Tukio hilo la kusikitisha lilitokea Alhamisi iliyopita maeneo ya Mlalakuwa-Mwenge, Dar baada ya kijana huyo, Manyaki Warioba kudaiwa kumpiga hadi kumuua dada yake, Joyce Warioba a.k.a Mama Vai.
Chanzo chetu ndani ya jeshi la polisi kilisema kuwa mkasa wenyewe ulikuwa hivi:

ASUBUHI
Mama yao aliwaaga Manyaki na Joyce kwamba anasafiri kwenda kwao Musoma ambako kulikuwa na msiba, hivyo aliwaomba wamsindikize Ubungo akapande basi.
Joyce alichukua sanduku na pembeni yake alikuwa amesimama Manyaki, nyuma yao mama mzazi akawa anawafuata taratibu kutokana na uzee.
Joyce hakwenda Stendi ya Mabasi Ubungo badala yake aliyekwenda huko ni Manyaki. 
Habari zilisema kuwa wakiwa Ubungo mama yao alikumbuka kwamba kuna fedha alikuwa amezisahau kuwakabidhi ili walipie umeme, maji na kuzoa takataka.
Ilisemekana kuwa mama huyo alimruhusu Manyaki kurudi haraka nyumbani ili aziwahi fedha hizo ambazo zilikuwa shilingi 86,000 kabla hazijakwapuliwa na Joyce.
Ilidaiwa kuwa Manyaki alipofika nyumbani alikwenda moja kwa moja hadi sehemu aliyoelekezwa na mama yake kwamba atazikuta fedha hizo lakini hakuzikuta.
Ilielezwa kuwa baada ya kuona hivyo kaka huyo alimuita Joyce na kumuuliza kama alichukua fedha lakini akaruka kimanga kwamba hakuelewa chochote kuhusu hela hizo.
“Manyaki alipoambiwa hivyo alihamaki akaanza kumpiga dada yake na baadaye akamchukua na kwenda kwa sangoma ili kuangalia kama kweli alichukua fedha au la,” kilidai chanzo.
Ilielezwa kuwa wakiwa njiani kurudi nyumbani, Manyaki alipandwa na hasira na kwa kushirikiana na wenzake wakaanza kumpa kipondo dada yake  hadi kumchania ‘skin tight’ yake.
 “Watu waliona jinsi walivyokuwa wakimpiga na walisikitika sana lakini hawakuwa na cha kufanya kwa kuwa waliona ni suala la wanandugu,” kilidai chanzo chetu.

KIFO CHA MAUMIVU
Ilisemekana kuwa Joyce alipofikishwa nyumbani, aliwaambia waliokuwa wakimpiga kuwa hajaiba fedha hizo na ili kujiokoa aliamua kutoa shilingi 10,000 alizozipata katika biashara yake ya njugu, lakini haikusaidia.
“Kipigo kiliendelea hadi akaishiwa nguvu na akawa anaomba maji wakamnyima, kuona hivyo mtoto wake alimpa lakini baadaye aliinua mkono mmoja akaonyesha ishara ya kuwaaga ‘wauaji’ wake huku akisema jamani mimi sijaiba fedha, akakata roho,” kilidai chanzo chetu.
Uwazi lilielezwa kuwa polisi kutoka Kituo cha Chuo Kikuu cha Dar es Salaam waliitwa ambapo Manyaki alikutwa akiwa nyumbani hapo akatiwa mbaroni na maiti ikachukuliwa na kupelekwa katika Hospitali ya Mwanyamala kwa uchunguzi zaidi.

MAMA AJILAUMU
Habari zilidai kuwa mama wa marehemu aliarifiwa kuhusu kifo hicho akiwa njiani na alipofika Singida alikatisha safari na kurejea nyumbani Dar.
Mama Warioba mara baada ya kuwasili nyumbani, aliangua kilio akijilaumu kwamba angetoa fedha zile siku moja kabla ya siku ya safari, hayo yasingetokea.
“Kwa nini mmempiga hadi mmemuua jamani, nani atanipikia uji nikiumwa?” alisikika akisema mama huyo huku akibubujikwa machozi.

KAMANDA WA POLISI
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kinondoni, ACP Camillius Wambura, hakupatikana kuzungumzia tukio hilo lakini afisa mmoja wa polisi ambaye hakutaka jina lake kutajwa gazetini alithibitisha kutokea kwa mauaji hayo.
Habari zilizolifikia Uwazi muda mfupi kabla ya kwenda mtamboni, familia ilitarajiwa kukabidhiwa mwili wa marehemu jana (Jumatatu) kwa ajili ya maziko. 
CREDIT;GLOBAL
Next Post Previous Post
Bukobawadau