Bukobawadau

MEMBE: MSIJE DAR WAKATI WA ZIARA YA OBAMA


 Waziri wa Mambo ya Nje, Bernard Membe amewashauri watu walioko mikoani kusitisha safari za kuja Dar es Salaam wakati wa ziara ya Rais wa Marekani, Barrack Obama kutokana na wingi wa wageni katika jiji hilo.
Ugeni huo pamoja na ule wa viongozi kumi na moja kutoka nchi mbalimbali duniani watakaohudhuria mkutano wa kimataifa wa Smart Partnership utakaofunguliwa kesho na Rais Jakaya Kikwete kwenye Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Julius Nyerere, umesababisha kuimarishwa kwa ulinzi katika maeneo mbalimbali hasa katika hoteli za kitalii ambazo zimeanza utaratibu wa upekuzi kwa wageni wake.
Akizungumza na katika mahojiano na Redio ya Clouds jana, Membe alisema jiji limefurika kwa wingi wa wageni.
“Hoteli na nyumba za wageni zimefurika wageni na magari mengi yamekodiwa. Kwa ujumla, huduma za kijamii zitakuwa shida,” alisema.
Rais Obama na mkewe Michelle watawasili nchini Jumatatu na tayari wapambe na maofisa usalama kutokana Marekani wameanza kuwasili. Mbali ya ujio huo, wake wa marais kutoka nchi 14 za Afrika watakaokutana na Laura Bush, mke wa Rais wa zamani wa Marekani, George Bush. Pia Michelle atahudhuria mkutano huo utakaofanyika Jumanne na Jumatano ijayo.
“Jiji la Dar es Salaam litakuwa na mambo mengi kwa hiyo wale wenye kuja kutaka kustarehe wafute safari zao,” alisema na kuongeza: “Kama kuna watu ambao hawapo Dar es Salaam na hawana sababu za kuja mjini waache tu mpaka wageni watakapoondoka kwa sababu jiji la litakuwa limejaa na baadhi ya barabara zitachukuliwa zitumike na wageni hao.”
Alisema katika kipindi cha siku tano zijazo, baadhi ya barabara za Jiji la Dar es Salaam zitakuwa na shughuli nyingi na nyingine zitalazimika kufungwa. Barabara itakayofungwa ni pamoja na ile ya Mwai Kibaki na ile ya Bagamoyo itakuwa na shughuli nyingi pia wakati Michelle atakapokwenda Jumba la Makumbusho, Jumanne ijayo.
Wasafiri wa mikoani
Wasafiri wa mikoani wataathirika zaidi Jumanne ijayo wakati Rais Obama atakapokwenda kutembelea mitambo ya kufua umeme ya Kampuni ya Symbion Ubungo.
Kituo hicho kipo Barabara ya Morogoro, ambayo ndiyo inayotumiwa na magari yanayoingia na kutoka mikoani.
Rais Obama atakwenda katika kituo hicho yapata saa 4.00 asubuhi na kwa kiasi kikubwa itaathiri magari ya usafirishaji wa mizigo na abiria yatakayokuwa yanatoka na kuingia Dar es Salaam kabla na wakati huo.
Next Post Previous Post
Bukobawadau