Bukobawadau

Figo za Mandela zaacha kufanya kazi *Serikali sasa yampigania afikishe miaka 95, Julai 18

IKIWA takribani mwezi mmoja sasa tangu Rais wa Kwanza Mweusi wa Afrika Kusini, Nelson Mandela, akimbizwe hospitalini akiwa mahututi kutokana na ugonjwa wa mapafu, taarifa zilizopatikana hivi karibuni zinaeleza kuwa madaktari bingwa wanaomtibu, wamegundua ugonjwa mwingine mwilini mwake.

Nje ya Hospitali ya Medi Clinic iliyoko Pretoria, ambako waandishi wa habari kutoka mashirika mbalimbali ya habari duniani wamefurika wakifuatilia mwenendo wa afya ya Mandela, juzi na jana, zilivuja taarifa kuwa Mandela ambaye anaishi kwa msaada wa mashine maalumu inayomwezesha kupumua, madaktari wake wamebaini kuwa figo zake zimeshindwa kufanya kazi.

Kwa mujibu wa taarifa hizo, madaktari bingwa wanaomtibu wameanza kupambana na ugonjwa huo kwa kumuwekea mashine ya kusaidia figo zake kufanya kazi na kwamba wanaangalia uwezekano wa kuzibadilisha bila kusababisha madhara mengine katika mwili wake ambao sasa unalindwa dhidi ya magonjwa nyemelezi.

Tayari Shirika la Utangazaji CNN, ambalo lina timu ya waandishi wake nje ya Hospitali ya Medi Clinic, limekwishatangaza taarifa za kubainika kwa ugonjwa huo na kwamba madaktari wamemuwekea kipimo kinachowezesha figo zake kufanya kazi.

Kabla ya kupatikana kwa taarifa hizo, ilielezwa kuwa madaktari wake walibaini hawawezi kuyatibu mapafu ya Mandela kutokana na madhara makubwa yaliyonayo na badala yake wamemuweka chini ya uangalizi wao maalumu wakihakikisha kuwa hapatwi na magonjwa nyemelezi yanayoweza kuhatarisha uhai wake.

Kupatikana kwa taarifa hizi kumezidisha wasiwasi wa mwenendo wa afya ya Mandela kwa waandishi wa habari walioko Hospitali ya Medi Clinic, ambapo wengi wamekuwa wakijitahidi kuzifikia mamlaka zinazohusika ili kutoa taarifa rasmi pasipo mafanikio kutokana na usiri uliopo.

Wakati zikipatikana taarifa za kugunduliwa kwa tatizo jipya kwa Mandela, baadhi ya vyombo vya habari nchini hapa, jana vilimkariri mmoja wa marafiki zake wa karibu kwa muda mrefu, Denis Goldberg, akieleza kuwa mashine zinazomsaidia Mandela kupumua haziwezi kuondolewa.

Goldberg alikaririwa akieleza kuwa alipewa taarifa za uwezekano wa kuondolewa kwa mashine hizo ili kumwezesha Mandela kupumzika, lakini madaktari wake walikataa kuziondoa kwa kueleza wanaweza kuziondoa iwapo watabaini sehemu muhimu za mwili wake hazifanyi kazi tena.

Kwa mujibu wa gazeti la The Star la Afrika Kusini, Goldberg, aliyekuwa mpinzani wa siasa za ubaguzi wa rangi, ambaye alimtembelea Mandela hospitalini Jumatatu iliyopita, alisema suala hilo lilijadiliwa na kufikia tamati kuwa mashine hizo hazitaondolewa.

Kauli hii ya Goldberg inapingana na ile iliyotolewa mapema wiki hii, ikikariri nyaraka zilizotolewa mahakamani na Makaziwe Mandela, mtoto mkubwa wa kike wa Mandela, ambazo pamoja na mambo mengine, zilieleza kuwa familia ilishauriwa na madaktari ikubali mashine hizo ziondolewe ili aweze kupumzika badala ya kuzidi kumuongezea maumivu.

Familia na ugomvi wa utajiri wake

Wakati Mandela akiwa mahututi hospitalini, familia yake imekuwa katika vita ya kugombea mahali panapostahili kuwa eneo maalumu la kuzika miili ya wanafamilia hiyo, vita ambayo inatafasiriwa na wengi nchini hapa kuwa kiini chake ni kutaka kurithi utajiri mkubwa alionao.

Hilo limethibitishwa pia na mjukuu wake mkubwa wa kiume, Mandla Mandela, ambaye katika mkutano wake wa hivi karibuni na waandishi wa habari baada ya kushindwa kesi ya ugomvi wa makaburi, alitaja utajiri wa Mandela kuwa moja ya sababu za ugomvi huo.

Hata hivyo, Mandla, kijana tajiri na chifu wa Mzove, ambaye alifunguliwa kesi na shangazi yake, Makaziwe na kuungwa mkono na wanafamilia 15, wakimtuhumu kuvamia eneo la makaburi la familia nyakati za usiku na kuiba mabaki ya miili ya watoto watatu wa Mandela, hatua ambayo inadaiwa ililenga kujihalalishia udhibiti wa mazishi ya rais mstaafu huyo.

Wakati kesi hiyo ikiendelea katika Mahakama Kuu ya Mthatha ya Jimbo la Eastern Cape, Mandla alikuwa akishutumiwa kusababisha mgogoro wa kifamilia kwa lengo la kutaka kumzika Mandela kwenye makazi yake ya Mzove, baada ya kufa ili alitumie kaburi lake kuchuma fedha kutokana na biashara ya utalii ya kuzuru kaburi hilo.

Madai mengine yaliyoibuka dhidi ya Mandla yalimhusisha na kuuza haki ya kutangaza mazishi ya Mandela kwa kituo kimoja cha utangazaji cha kimataifa na kuvuna mamilioni ya Rand.

Kwa upande mwingine, Makaziwe naye amedaiwa kuingia katika vita na mpwa wake, Mandla kwa sababu ya kutaka kurithi utajiri wa baba yake atakapofariki.

Makaziwe, mwenye umri wa miaka 60 sasa, kama ilivyo kwa Mandla, naye anadaiwa kuwa na utajiri mkubwa, huku akiwa anaishi nje ya Afrika Kusini, lakini hayuko tayari kuona mali za baba yake zikiangukia mikononi mwa mjukuu.

Mandela anatajwa kuwa na fedha nyingi katika mfuko wake wa Mandela Foundation pamoja na sehemu nyingine ambazo atakayezirithi atakuwa bilionea.
Next Post Previous Post
Bukobawadau