Bukobawadau

HITIMISHO LA ZIARA YA RAIS KIKWETE MKOANI KAGERA,AONGELEA SWALA LA MBUNGE NA MEYA

 Rais Kikwete akiwasili ndani ya uwanja wa kaitaba.
Mh. Balozi Kagasheki, Mh. Mama pangani wakisalimiana na Rais Kikwete mata tu baada ya kuwasili uwanjani kaitaba.
Viongozi mbalimbali wa kichama.
 Kundi zima la Kakau Band limeweza kutoa burudani safi

KUHUSU SWALA LA MH.JK MEYA AMANI NA BALOZI KAGASHEKI
RAIS Jakaya Kikwete amesema kuwa mgogoro wa utekelezaji wa miradi mitatu ya uuzaji viwanja, ujenzi wa soko la kisasa na kituo cha mabasi uliowagawa meya wa manispaa ya Bukoba, Anatory Amani, na mbunge, Khamis Kagasheki, ni jambo dogo wanalopaswa kulimaliza wenyewe.

Akihutubia mkutano wa hadhara jana jioni katika uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba baada ya kuhitimisha ziara yake mkoani Kagera, Rais Kikwete alisema kuwa mgogoro huo uishe na taratibu za kujengwa soko ufuatwe huku akisisitiza kuwa lazima litajengwa tu.

Alisema lazima kuwa na mabadiliko kwani soko lililopo ni la muda mrefu na hivyo linahitajika kujengwa jipya ila kwa kufuata utaratibu.

Rais Kikwete alisema kuwa haina maana viongozi hao kugombana ila haki lazima itendeke kwa wanaotoka na wanoingia ili kipaumbele kiwe kwa wale wanaoingia.

Aliongeza kuwa wananchi wawe watulivu na haki itatendeka ila wale wanaotoka watafutiwe eneo la kwenda kufanyia biashara zao kabla ya kuondolewa kupisha ujenzi huo.

Rais alikuwa akizungumza baada ya Balozi Kagasheki kuhutubia akielezea utata wa miradi hiyo iliyozua mtafaruku na kusababisha mgawanyiko mkubwa kwa Chama cha Mapinduzi (CCM) Bukoba Mjini.

Meya Amani anatuhumiwa na baadhi ya madiwani wa manispaa hiyo kuwa ametumia vibaya madaraka yake na hivyo kujihusisha na vitendo vya ubadhirifu katika miradi hiyo.

Tayari madiwani nane wa chama hicho pamoja na Kagasheki na madiwani wa upinzani wametia saini hati ya kumtaka mkurugenzi wa halmashauri hiyo, aitishe kikao cha dharura ili kumng’oa meya huyo.

Hoja ya kumng’oa meya iliibuliwa mwaka jana na Kagasheki, ambaye pia ni Waziri wa Malialisili na Utalii, akiunga mkono msimamo wa CHADEMA, kupinga miradi ya uuzwaji wa viwanja zaidi ya 5000 na ujenzi wa soko la kisasa.

Kagasheki aliapa mbele ya wapigakura wake kuwa hayuko tayari kusutwa na Katibu Mkuu wa CHADEMA, Dk. Willibrod Slaa, kutokana na mikataba ya siri yenye harufu ya kifisadi aliyoisaini Amani kwa kificho bila kuwashirikisha madiwani wenzake.

Baadhi ya vigogo wa serikali na chama mkoa wa Kagera, wamekuwa wakifanya jitihada za kumnusuru Amani kwenye sakata hilo.

Vigogo hao ni Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Fabian Massawe, Mkuu wa Wilaya ya Bukoba Mjini, Mwenyekiti na Katibu wa CCM Mkoa.

Sakata hilo lilifikishwa hadi kwa Waziri Mkuu Mizengo Pinda, ambapo Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Tamisemi), Hawa Ghasia, aliunda tume ya kuchunguza tuhuma hizo baada ya vigogo wakuu wa CCM kushindwa kuutatua mgogoro huo.

Halmashauri ya Manisapaa ya Bukoba ina madiwani 24 ambapo kati yao watatu wanatoka CUF, wanne ni wa CHADEMA na 17 wanatoka CCM.

Na ili kupitisha uamuzi huo wa kumuondoa meya, ni lazima robo tatu ya madiwani yaani 16, wapige kura ya kuunga mkono hoja hiyo.

Miongoni mwa vigogo waliosaini hati ya kutaka kuitishwa kikao cha kumng’oa meya huyo ni Naibu wake, Alexander Ngalinda (Diwani wa Kata ya Buhende), na Yusuf Ngaiza (Kashai) ambaye pia ni mwenyekiti wa CCM, manispaa ya Bukoba.


Next Post Previous Post
Bukobawadau