Bukobawadau

JK KUZINDUA BARABARA, KIVUKO KAGERA


Na Bernard Bugoma

RAI S Jakaya kikwete anatarajiwa kuzindua ujenzi wa barabara na kufungua kivuko katika Mkoa wa Kagera kuanzia Julai 26 hadi 28.Kwa mujibu wa Taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa jana na Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Balozi Herbert E. Mrango ilisema Rais Kikwete atakuwa mgeni rasmi katika sherehe za uzinduzi wa miradi ya barabara na kufungua kivuko mkoani humo.

Balozi Mrango alisema uzinduzi na ufunguzi wa miradi hiyo utaanzia tarehe 26 Julai 2013, ambako Rais ataweka jiwe la msingi kwa ajili ya ujenzi wa barabara ya Kagoma - Biharamulo - Lusahunga yenye urefu wa kilomita 154. Ujenzi wa sehemu ya Kagoma - Biharamulo - Lusahunga unagharamiwa na Serikali ya Tanzania.Hata hivyo Julai 27 Rais Kikwete atafungua rasmi kivuko cha Ruvuvu kinachotoa huduma ya kuvusha magari na abiria katika mto Ruvuvu eneo la Rusumo, kivuko ambacho kinauwezo wa kubeba tani 35 (magari madogo 4 na abiria 80 kwa pamoja) kimenunuliwa kwa kutumia fedha za ndani.
Aidha Julai 28 Rais ataweka jiwe la msingi katika barabara ya Kyaka - Bugene - Kasumulo yenye urefu wa km 59.1. Mradi huu unagharamiwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Sherehe za uzinduzi wa ujenzi wa barabara hii zitafanyikia kijiji cha Omugakorongo.

Kutekelezwa kwa miradi hii ni mafanikio makubwa sio tu kwa sekta ya usafirishaji bali pia kwa uchumi wa Mkoa wa Kagera na Taifa kwa ujumla ambapo barabara hizo na kivuko vitaimarisha huduma ya usafiri katika Mkoa wa Kagera na hivyo kuboresha biashara na usafiri kati ya mkoa huo na mikoa mingine ya Tanzania pamoja na nchi jirani za Burundi, Rwanda na Uganda..
Next Post Previous Post
Bukobawadau