Bukobawadau

KULA BILA KUNAWA Katika Ushirika wengine wanakula hata kwa miguu

Na Prudence Karugendo
WAKATI Mkutano Mkuu wa CCM ulipomuidhinisha Mzee Ali Hassan Mwinyi kugombea urais mwaka 1985, wakati huo akiwa mgombea pekee, mtangulizi wake aliyekuwa ameamua kustaafu kwa hiari yake, Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere, alimwambia Mwinyi kwamba mimi nakuonea huruma sana tofauti na wanaoshangilia na kukupongeza. Nyerere alisema kwamba urais ni mzigo mzito sana ambao mtu mwadilifu anapaswa afikirie mara kadhaa kabla ya kuamua kumpongeza aliyependekezwa au kuchaguliwa kuubeba.
Uzito wa mzigo wa urais, pamoja na mambo mengine, unachangiwa na nguvu ya maamuzi ambayo mara nyingi huwa ni ya mwisho yanayoweza kutolewa na rais bila kuhojiwa. Hiyo ni kwamba endapo rais ana wasaidizi wanaotetereka kimaadili anaweza kujikuta amefikia uamuzi ambao baadaye unaweza kuitesa roho yake wakati yeye ndiye mtoa uamuzi. Urais ni mzigo mzito sana.
Wakati Rais Kikwete anajiandaa na ziara ya kuutembelea mkoa wa Kagera juma lililopita, mkoa wa Kagera ulitoa ratiba ya shughuli alizopangiwa kuzifanya wakati wa ziara hiyo. Shughuli mojawapo ilikuwa ni ya kuzindua jengo linalodaiwa ni la kitega uchumi la chama kikuu cha ushirika cha KCU (1990) Ltd.
Zilifanyika jitihada za wazi kutoka kwa wakulima wa kahawa wa maeneo yanayounda chama hicho cha KCU (1990) Ltd. za kutaka iondolewe kwenye ratiba ya shughuli za rais mkoani humo, shughuli ya rais kulizindua jengo hilo, lakini jitihada zao zote zikagonga mwamba kutokana na waratibu wa ziara hiyo ya rais, wakiongozwa na mkuu wa mkoa, Fabian Massawe, kufumba macho na kuziba masikio na kujifanya hawayaoni wala kuyasikia malalamiko yaliyokuwa yanatolewa na wanaushirika wa KCU (1990) Ltd..
Kwahiyo ikambidi rais aifuate ratiba aliyopangiwa na kulifungua jengo hilo huku akikisifia chama hicho cha ushirika kwa ufanisi wake akisema walau kinacho kitu cha kuonyesha. Lakini wakati akitoa sifa hizo watu wengi kati ya wachache waliohudhuria hafla hiyo walikuwa wakiguna, ukiondoa wachache waliolichukulia tendo la rais kukubali kulifungua jengo hilo kama mkombozi wao. Na hao ni viongozi na watumishi wa KCU (1990) ltd..
Bilashaka hata rais atakuwa amejiridhisha mwenyewe kwamba kuna kinachoendelea kutokana na uchache wa watu waliohudhuria ufunguzi huo, na hasa pale aliposema “Ushirika hoyee” watu wakakaa kimya huku viongozi na watumishi wa KCU (1990) Ltd. pekee yao wakiitikia kwa kupaza sauti kwa nguvu zao zote ili kufidia sauti za watu wengine walioamua kukaa kimya.
Kweli urais ni mzigo mkubwa.
Ila katika nasaha zake baada ya uzinduzi wa jengo hilo ndipo rais akatoa kilichowakuna wanaushirika, kwamba kipaumbele cha ushirika kinapaswa kielekezwe kwa wanaushirika wenyewe. Na kuongeza kwamba viongozi wa vyama vya ushirika wanakula bila kunawa, msemo ambao unaweza kutafsiriwa kirahisi kama viongozi wa ushirika kushiriki wizi wa mali za ushirika.
Hatahivyo nataka nimuongezee rais kwenye usemi wake huo, kama nilivyotumwa na baadhi ya wanaushirika wa KCU (1990) Ltd. niliowasiliana nao, kwamba viongozi na watumishi wa KCU (1990) Ltd. mbali na kula bila kunawa wanadiriki hata kula kwa miguu baada ya kuona mikono yao michafu haiwatoshi.
Wanaushirika hao, ambao hawana uhakika kama kweli jengo alilolizindua rais ni mali ya chama chao, wanayo maswali mengi yanayowasumbua. Kwanza kabisa wanauliza, uimara wa ushirika unapaswa kuangaliwa kupitia kwenye majengo na vitega uchumi vinavyodaiwa ni mali ya ushirika au kwa kuwaangalia wanaushirika wenyewe walivyo kiuchumi?
Wanauliza inawezekanaje wanaushirika wapate mlo mmoja kwa siku kutokana na kukosa uwezo wa kujikimu, washindwe kupeleka watoto shule na mambo mengine mengi, kisa wamekopesha zao lao la biashara kwa chama chao cha ushirika bila chama hicho kuwapa matumaini yoyote ya kuwalipa, halafu ushirika udai uko imara kwa kuonyesha majengo na kudai ni vitega uchumi? Hivyo vitega uchumi vipo kwa manufaa ya nani kama vinawaacha wanaushirika wabaki wakiadhirika na kutaabika kwa ukata?
Kuhusu jengo alilolizindua rais huku risala ya ushirika ikisema kwamba jengo hilo limejengwa kwa pesa za KCU (1990) Ldt., wanaushirika wanauliza pesa hiyo imetoka wapi wakati wakati chama hicho muda wote kinanunua kahawa yao kwa mkopo kwa madai ya kwamba hakina pesa, na ikizingatiwa kwamba mahesabu ya chama hicho yanaonyesha jinsi chama hicho kilivyopata hasara ya karibu jumla ya shilingi 3,000,000,000 kwa miaka 5 mfululizo?
Wengine wanasema kwamba kabla ya rais kuzindua kitega uchumi hicho, ambacho rais hakuelezwa ni lini faida yake inagawanywa kwa wanaushirika na kwa namna gani, angeonyeshwa vitega uchumi vingine vya ushirika huo vilivyogeuka magofu kama ilivyo Hoteli ya Lake. Baada ya rais kuiona hoteli hiyo inayotumia pesa ya wakulima kiasi cha shilingi 150,000,000 na kuingiza milioni 1 tu kwa mwaka, pengine viongozi wa ushirika wangekuwa katika nafasi nzuri ya kumweleza rais ni kwa miujiza gani wangekitunza kitegauchumi hicho kipya kwa manufaa ya wakulima, kama kweli ni chao, kabla hawajakigeuza gofu kama walivyofanya kwa vitegauchumi vingine vingi.
Jambo la kushangaza katika ushirika wa KCU (1990) Ltd. ni kwamba wale wanaojaribu kuhoji juu ya kinachojionyesha ni ufisadi wa wazi, kula bila kunawa au kula kwa kutumia mikono michafu na miguu, wanapigwa vita ya kutisha na kuzushiwa kashfa za ajabuajabu. Archard Felician Muhandiki ni mwakilishi wa chama cha msingi Kamachumu, Muleba. Mwakilishi huyo bila kificho chochote amekuwa mwiba mkali kwa ufisadi ndani ya KCU (1990) Ltd.
Lakini Muhandiki anadai kushambuliwa kila upande kwa sasa, mashambulizi anayosema yanajionyesha yanavyochochewa dhidi yake kutokana na msimamo wake wa kupinga ufisadi ndani ya ushirika.
Mwandiki anasema kwamba kwa muda mrefu alikuwa akipanga ofisi zake kwenye jengo la ushirika mtaa wa Lumumba Jijini Dar es salaa, kabla ya kuhamia kwenye jengo lingine. Anasema hata alipohama aliacha kodi yake ikiwa haijaisha. Lakini anasema Katibu Mtendaji wa Shirikisho la Vyama vya Ushirika, Willigs Mbogoro, ambaye ndiye mhusika mkuu wa jengo hilo la ushirika, anapita mitaani akimchafua Muhandiki kwamba alifukuzwa katika jengo hilo kutokana na kudaiwa kodi.
Anasema anachokifanya Mbogoro ni mwendelezo wa vita ileile ya kumsakama kutokana na yeye, Muhandiki, kuusakama ufisadi ndani ya KCU (1990) Ltd.. Anasema Mbogoro ni mjumbe wa Bodi ya wakurugenzi wa TANICA, kampuni tanzu ya KCU (1990) Ltd., kwahiyo naye ni sehemu ya KCU (1990) Ltd. Na ni Mbogoro yuleyule aliyeitisha kutano wa waandishi wa habari kuisafisha KCU (1990) Ltd., lakini baadaye alipobanwa na waandishi kuhusu usafi wa chama hicho cha ushirika akayakana maneno yake na kuomba radhi. Hatahivyo Mbogoro hakuita tena waandishi wa habari kuyakana maneno yake juu ya KCU (1990) Ltd. kama alivyofanya wakati anaisafisha.
Kwahiyo sasa anachokifanya Mbogoro ni kama kuendesha vita ya msituni dhidi ya wale wanaotaka kukisafisha chama hicho kikuu cha ushirika cha KCU (1990) Ltd. ili kiondokane na ufisadi unaokikabili.
Huo ndio upande wa pili ambao inaonekana Rais Kikwete hakuonyeshwa kuhusu ushirika mkoani Kagera. Nimeiamini kauli ya Baba wa Taifa, urais ni mzigo mzito sana.
prudencekarugendo@yahoo.com
0784 989 512
Next Post Previous Post
Bukobawadau