Bukobawadau

Lwakatare aruhusiwa kutibiwa nje ya nchi

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu imemruhusu Mkurugenzi wa Ulinzi na Usalama wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Wilfred Lwakatare kwenda kutibiwa nje ya nchi. Kibali hicho kilitolewa jana na Hakimu Mkazi, Aloyce Katemana baada ya Wakili wa Lwakatare, Nyaronyo Kicheere kuwasilisha maombi hayo mahakamani.


Nyaronyo akiomba kibali hicho aliwasilisha nyaraka mbalimbali za matibabu kutoka kwa madaktari wa Hospitali ya Taifa Muhimbili zikionyesha mshtakiwa anasumbuliwa na matatizo ya mgongo.

Pia wakili huyo alilalamikia kitendo cha mshtakiwa wa pili, Ludovick Joseph kuzungumzia kesi magazetini huku Serikali ikikaa kimya bila kulalalamikia suala hilo.

Hakimu Katemana baada ya kukubali kutoa kibali kwa mshtakiwa Lwakatare alitoa onyo kali kwa Ludovick kwamba akiendelea kuzungumzia kesi iliyopo mahakamani katika vyombo vya habari atafutiwa dhamana.

“Mshtakiwa wa pili anaonywa na mahakama kwa kuzungumzia kesi iliyopo mahakamani katika vyombo vya habari, ikitokea amerudia kufanya hivyo dhamana yake itafutwa, atarudi rumande,”alisema Katemana.

Washtakiwa hao wanakabiliwa na mashtaka ya kula njama za kutaka kumdhuru kwa sumu Mhariri Mtendaji wa Gazeti la Mwananchi, Dennis Msacky..

Lwakatare aliachiwa huru Juni 11, mwaka huu kwa dhamana baada ya kutimiza masharti, lakini Ludovick aliendelea kusota mahabusu kwa muda kutokana na kushindwa kutimiza masharti hayo hadi alipotoka hivi karibuni.
Next Post Previous Post
Bukobawadau