Bukobawadau

MAISHA YA WASTARA BAADA YA KIFO CHA SAJUKI

KATI ya ndoa ambazo kila msanii anayeingia humo anatamani aishi maisha mazuri na ya kupendana, ni ya mwanadada Wastara na mumewe ambaye kwa sasa ni marehemu, Said Kilowoko ‘Sajuki.’

Ikiwa ni siku chache tangu arejee kutoka nchini Oman alipokwenda kwa ajili ya eda, baada ya kufiwa na mumewe huyo Januari 2, mwaka huu, Wastara anafunguka na kudai kwamba amekuwa akijiona mpweke tangu kutokea kwa tukio hilo, ambalo kamwe hawezi kulisahau katika maisha yake na linamfanya kila wakati kuwa katika msongo wa mawazo.

“Kwa kweli, kama ningekuwa sina watoto hawa ambao wananitegemea, ningemuomba Mungu achukue roho yangu ili nimfuate mume wangu huko aliko, maana sioni umuhimu wa kuishi wakati mbadala wangu ameshatangulia mbele ya haki,” anasema na kuongeza:

“Lakini sitaki kumkufuru Mungu, ila namuomba anipe afya niweze kuwalea wanangu ambao kwa sasa mimi ndiye baba ndiye mama.”

MAISHA YAKE BAADA YA KIFO CHA SAJUKI

Anasema, tangu mumewe afariki dunia, amekuwa hana amani moyoni na kujiona mkiwa, kwa kuwa alikuwa mtu aliyeijali familia, japokuwa amemzalia mtoto mmoja ambaye ana mwaka mmoja na nusu sasa huku wengine wawili alikuwa ametangulia kuzaa na mwanamume mwingine.

Wastara anasema anakosa amani kwa kuona wanae watatu wanapata taabu kwa pamoja, wakati awali alitengana na mumewe ambaye alizaa naye watoto hao wawili, wa kwanza akiwa na miaka 15 na wa pili miaka tisa.

“Sijawahi kuona katika maisha yangu baba ambaye anawapenda watoto wake kama ambavyo ilikuwa kwa Sajuki, ndiyo maana nasema ni pengo kubwa, kwani hata wanangu walijua huyo ni baba yao mzazi kwa jinsi ambavyo alikuwa akiwajali, mbali na huyo mdogo ambaye ni wa kwake,” anasema Wastara.

Aidha, Wastara anasema katika maisha yake na Sajuki ndani ya miaka mitano, alifarijika na kujiona mwenye amani duniani, hasa namna alivyowachukulia watoto wake kama wanae wa kuwazaa na kuwapa upendo wa hali ya juu.

“Nilikuwa nikitamani sana siku moja nimzalie mume wangu mtoto ambaye atampenda kama ambavyo alikuwa akiwapenda wa mwanaume mwenzake na Mungu akanijalia nikafanikiwa, lakini ndiyo hivyo kwa bahati mbaya Mungu hakuweza kumpa nafasi ya kukaa naye na kumuonyesha mapenzi ya dhati mwanae, jambo ambalo hadi sasa nikikaa na kumwangalia huyu mtoto naumia sana,” anasema Wastara huku akibubujikwa machozi.

Kutokana na mawazo hayo, wakati mwingine anadai kuwa huwa anajiliwaza kwa mtoto wake mkubwa na kumuoa kama ndiye baba wa familia, kutokana na aliyempenda hayupo tena duniani.

SIKU ASIYOISAHAU WAKATI SAJUKI AKIWA HAI


Wastara anasema siku ambayo hataisahau katika maisha yake wakati mumewe yungali hai ni mwaka 2009 walipopata ajali ya pikipiki na kulazimika kukatwa mguu mmoja kutokana na majeraha makubwa aliyokuwa ameyapata.

Hata hivyo anasema hilo halikumfanya Sajuki kupunguza mapenzi kwake, kwani aliendelea kumuonesha mapenzi ya hali ya juu na kuamua kufunga naye ndoa, jambo ambalo kwa wapenzi wengine inakuwa vigumu.

“Siku nyingine ambayo nayo sitaisahau ni ile tuliyokwenda kufanya shoo jijini Arusha kwa ajili ya kupata fedha za kwenda nje ya nchi kupata matibabu, ila hatukufanikiwa, kwani waliotuandalia shoo hiyo waliahirisha na kufanya ya kwao tukiwa tayari jijini humo, jambo lililomfanya mume wangu kuanza kujisikia vibaya huku kila mara akiniambia, mke wangu nakufa mimi, ila nasikitika kukuacha peke yako,” anasema Wastara aliyekuwa akitokwa machozi wakati wote.

ANASEMAJE KIFO CHA MUMEWE KUHUSISHWA NA USHIRIKINA?


Japokuwa watu wengi wamekuwa wakihusisha matatizo yake na imani za kishirikina, Wastara anasema haamini kama kuna ushirikina katika maisha yake, ila kama kuna mtu anafanya hivyo, Mungu atamlipa.

“Mimi huwa namuamini Mungu kwa kila jambo na kama watu wanahusisha matatizo ya maisha yangu na ushirikina kutoka kwa mume wangu wa kwanza, mbona nilivyoachana naye nilikaa miaka mitano sikupata tatizo lolote mpaka nikaja kuolewa na Sajuki ndiyo yatokee na nilivyokuwa mdogo nilipata tatizo la miguu na kichwa na hilo nalo tuseme ni huyo mwanamume wakati alikuwa hata hajanijua?” anahoji Wastara.

CHANGAMOTO ANAZOZIPATA KWA JAMII INAYOMZUNGUKA

Wastara anasema, tangu mumewe kufariki dunia, amekuwa akipata usumbufu kutoka kwa wanaume mbalimbali ambao anawaona kama waliomba itokee hivyo, lakini hawezi kufanya upuuzi huo na kama kweli walikuwa na mapenzi ya dhati wangemfuata mumewe alipokuwa hai.

Mbali na hilo, anawataka Watanzania kumchukulia poa, kwani wanapomshangaa wanamfanya kujiona mpweke na kumrudisha nyuma kifikra, wakati yeye anajitahidi kusahau.

“Kipindi nimepata ajali, mimi nilikuwa naumia sana, lakini marehemu mume wangu alikuwa anaumia zaidi yangu, mpaka mimi nilikuwa naanza kumtuliza yeye,” anasema.

HISTORIA YAKE KWA UFUPI

Wastara alizaliwa Septemba 27, 1983 mkoani Morogoro. Mwaka 1989 alijiunga na Shule ya Msingi Mvomero ‘A’ na kuhitimu mwaka 1995.

Msanii huyo kipenzi cha watu kwenye tasnia ya filamu, mwaka 1996 alijiunga na sekondari lakini hakufanikiwa kufika kidato cha nne kutokana na sababu zilizokuwa nje ya uwezo wake.
Next Post Previous Post
Bukobawadau