MBUNGE wa Kinondoni (CCM), Idd Azzan, amesema yupo tayari kujiuzulu ubunge, ikiwa itabainika anajihusisha biashara ya dawa za kulevya. Kauli hiyo imekuja siku chache baada ya kutajwa katika moja ya barua iliyosambazwa katika mitandao ya kijamii, baada ya mtu anayedaiwa kukamatwa China na kuwatuhumu watu kadhaa akiwamo Idd Azzan.

Akizungumza na MTANZANIA jana kuhusu sakata hilo, alisema hatua ya kuhusishwa na biashara haramu ya dawa za kulevya, ni kutotenda haki mbele ya jamii hasa wapiga kura wake na Taifa kwa ujumla.

Alisema mtu aliyendika barua ya tuhuma dhidi yake, ni wazi amedhamiria kumshushia heshima na huenda akawa ana jambo limejificha.

“Ni kweli nimeiona hiyo barua katika mtandao, inayodaiwa imeandikwa na kijana ambaye amekamatwa Hong Kong nchini China. Lakini ninajiuliza kama kweli yeye ni raia mwema, katika hili kwanini hakutaka kutaja jina lake kwenye barua hiyo.

“Hata nilipoisoma nimebaini kuwa huyo mtu ametumika na huenda kabisa hayupo nje ya nchi, kwani katika maelezo yake anataja jina la Balozi Philip Marmo kuwa amemsaidia hali ya kuwa hivi karibuni Rais Kikwete alimteua Balozi mpya Abdulrahman Shimbo na Marmo kuwa Balozi wa Shirikisho la Ujerumani.

“Kingine naona alijaribu kuandika uongo kuweza kuaminisha jamii, kwani hata hilo jila la balozi mwanzo limetajwa jina la Bernad na kukatwa kwa wino. Ninapenda kulieleza Taifa kuwa naomba vyombo vya usalama vifanye uchunguzi wa jambo hili na nikibainika ninauza dawa za kulevya nipo tayari kujiuzulu ubunge wangu.

“Kubwa haki itendeke katika kufanya uchunguzi wa jambo hili, ila ni lazima jamii na Watanzania kwa ujumla tusikubali kwa makusudi watu waichafue nchi yetu kwa chuki na fitna tu,” alisema Azzan.

Alisema kutokana na hali hiyo, anashindwa kuchukua hatua yoyote ya kufanya zaidi ya kuliandikia barua Jeshi la Polisi lifanye uchunguzi dhidi ya barua hiyo kuweza kubaini ukweli wa jambo hilo.

“Sijawahi kuuza dawa za kulevya na hata katika familia yangu hakuna mtu anayefanya biashara hiyo haramu. Kila mmoja anajua kuwa Idd nilikuwa Diwani wa Kata ya Magomeni, huku kazi yangu kubwa ikiwa ni biashara ya magari na daladala ambayo ninaendelea nayo hadi sasa mbali ya ubunge kama nilivyopewa heshima na wapiga kura wangu wa Kinondoni,” alisema Azzan.

MTANZANIA ilipomuuliza kuwa ni hatua gani ikibainika hakuna ukweli wa jambo hilo baada ya vyombo vya usalama kufanya uchunguzi, alisema atakachokifanya anamuachia Mungu.

“Ni ngumu kusema hatua gani nitachukua ikibainika hakuna ukweli, lakini nataka kusema kama yule aliyeandika barua hii angetaja jina lake ni wazi baada ya uchunguzi ningeweza kuomba ushauri kwa mwanasheria wangu hatua za kuchukua, lakini kwa kuwa hakutaja jina ni ngumu kuweza kuamua,” alisema Azzan.

Kwa mujibu wa taarifa zilitolewa kupitia mitandao, ziliripoti kukamatwa kwa Watanzania wawili nchini China wakiwa na dawa za kulevya zenye thamani ya Dola milioni 3.34 za Marekani.

Chanzo: Mtanzania.