Bukobawadau

Membe : Hizi ndizo sababu za ujio wa Rais Barrack Obama


Dar es Salaam. Wakati Tanzania imejiandaa kupokea ugeni mkubwa kimataifa kwa siku mbuli kuanzia leo, kumekuwa na maswali mengi ambayo wananchi pamoja na wachambuzi wa masuala ya siasa za kimataifa wamekuwa wakijiuliza juu ya ujio wa Rais Obama wa Marekani katika ardhi ya Tanzania.
Miongoni mwa maswali hayo ni pamoja na anakuja Tanzania kufanya nini? Kwa nini hatembelei Kenya ambako ndiko hasa asili yake? Pamoja na wale ambao wamekuwa na wasiwasi juu ya rasilimali za nchi hasa gesi. Katika mahojiano maalumu na gazeti hili, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe anafafanua zaidi kuhusu ziara hiyo , umuhimu na manufaa yake.
Urafiki wa Tanzania na Marekani
Waziri Membe anasema nchi hizi mbili zimekuwa na urafiki wa karibu sana katika kipindi cha muongo mmoja na nusu (miaka 15) ushirikiano baina ya nchi hizi mbili umeongezeka. Anasema urafiki huo ulianza kuimarika baada ya kulipuliwa kwa ubalozi wa Marekani nchini mwaka 1998.
Anakumbuka baada ya kutokea mlipuko katika ubalozi huo jijini Dar es Salaam, Tanzania ilishirikiana kwa karibu na Marekani katika kuhakisha kwamba watuhumiwa wanasakwa, kukamatwa na kushtakiwa, huku katika mataifa mengine haikufanyika hivyo.
Anasema kitendo hicho kiliongeza ‘uaminifu’ kwa  Serikali ya Marekani ambayo katika kipindi hicho iliongozwa na Bill Clinton. Ukarimu wa Watanzania ukaifanya nchi yao ipendwe  na utawala wa George W. Bush na sasa Obama.
Demokrasia na Utawala Bora
Katika hilo, Membe anasema Tanzania kwa kiwango kikubwa imekuwa inatekeleza misingi ya utawala bora, uhuru wa kupata habari, haki za binadamu. Anasema hata kama kumekuwa na malalamiko juu ya suala la utekelezaji wa haki za binadamu na utawala bora nchini bado Tanzania iko katika nafasi nzuri zaidi katika takwimu kidunia ukilinganisha na nchi nyingine barani Afrika.
“Ni kweli kwamba tumekuwa tunafanya vizuri katika kigezo cha demokrasia na utawala bora ukilinganisha na nchi nyingine Afrika….katika ‘Peace Index’ (kiwango cha Amani) tunashika nafasi ya 53 duniani , Kenya wapo nafasi ya 135, Rwanda 136 na Burundi 144,” anasema Membe.
Nafasi ya Tanzania Ukanda wa Maziwa Makuu, Kimataifa
Akizungumzia nafasi ya Tanzania katika kutatua migogoro, Membe anasema nchi imekuwa kinara katika utatuzi wa migogoro katika nchi jirani, mfano ,Kenya, Zimbabwe, Comoro  pamoja na Madagascar.
Next Post Previous Post
Bukobawadau