Bukobawadau

Muungano si kazi ya Mungu, uboreshwe


Na Msiba Pakia
KWA  muda mrefu nilikuwa sijaandika makala kuchangia mawazo yangu kwenye mwenendo wa mambo katika nchi yetu. Ni kutokana na msuguano wa shughuli za maisha, nikatoweka machoni mwa wasomaji wangu.
Lakini sasa kufuatia kuwepo kwa mchakato nyeti unaoendelea wa kuadika katiba mpya ya nchi yetu, Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, nimeona bora na mie nichangie mawazo yangu nikiwa hasa nimeulenga muungano wa nchi yetu.
Muungano wa Tanzania umekumbwa na misukosuko katika miaka ya karibuni kutokana na malalamiko  hasa yanayotokea upande mmoja wa muungano. Wazanzibari wamekuwa wakiyalalamikia baadhi ya mambo katika muungano na kuonesha kwamba hayautendei haki upande wa Zanzibar kutokana na kuonekana  yanakiuka baahi ya makubaliano ya msingi yaliyomo katika Hati ya Muungano.
Kwahiyo katika kujaribu kuuboresha muungano kupitia katika katiba mpya inayoandaliwa, yakiwa yameondolewa mambo hayo yanayoonekana kuwa kero kwa muungano,  Tume ya Rais ya Mabadiliko ya Katiba, imekuja na rasmu iliyotokana na maoni ya wananchi yaliyokusanywa na tume hiyo.
Moja ya mambo yaliyomo katika rasmu hiyo ni muundo wa serikali tatu katika Muungano wa Tanzania. Hilo ni jambo lililotokana na maoni ya Watanzania walio wengi na tume kuamua kulitendea haki jambo hilo.
Kitu cha ajabu ni kwamba rasmu iliyoletwa na tume iliyoundwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, aliye pia mwenyekiti wa chama tawala, CCM, inaonekana kupingwa kwa nguvu zote na chama hichohicho tawala! CCM inaipinga rasmu hiyo hasa kwa upande wa serikali tatu zinazotajwa kwenye rasmu hiyo. Hapo ndipo ninapotaka nijikite.
Muungano wa aina yoyote unaohusisha pande mbili haunabudi  kuyaheshimu matakwa ya pande zote mbili bila upande mmoja kuonekana unataka upewe ushawishi zaidi katika muungano husika huku upande wa pili ukibaki kunung’unika. Ndiyo maana Tume ya Mabadiliko ya Katiba ikaona bora ilete rasmu ya serikali tatu kama ilivyotolewa maoni na wananchi walio wengi, kusudi pawepo na Serikali ya Tanganyika, Serikali ya Zanzibar na Serikali ya Muungano.
Lakini Chama Cha Mapinduzi nacho kinakuja na msimamo wake kwamba liwe jua au iwe mvua ni lazima muungano ubaki na serikali mbili tu.
Sielewi msimamo huo wa CCM umelenga kumnufaisha nani. Angalia, Watanzania, ambao ndio wenye nchi, wanasema tunataka serikali tatu,  lakini chama tawala ambacho kinaonekana kunogewa na utawala, kinasema ni lazima serikali mbili tu! Kwa maana hiyo katika muungano huu chama tawala kiko tofauti na wananchi. Na kama ni hivyo kinayoyafanya ni kwa manufaa ya nani?
Sijui mtawala na mwenye nchi nani anapaswa kupewa kipaumbele katika maamuzi, hasa ikizingatiwa kwamba hii ni karne ya maridhiano, wakati ubabe wa kiimla vimebaki katika historia.
Ninaloliona hapa ni kwamba watawala hawa na chama chao wanalenga kuulinda uwepo wa chama chao kuliko wanavyofikiria kuulinda uwepo wa muungano na taifa la Tanzania kwa ujumla. Wasiwasi wao ni kwamba nje ya serikali mbili, kama ilivyo kwa sasa, chama chao kitakosa mizizi na kushindwa kuhimili changamoto zinazojitokeza kwa sasa na hivyo kuishia katika kusambaratika.
Ni wazi kwamba kwa wakati huu CCM imezidhibiti hizi serikali mbili, hata kama si kwa ushawishi, ila kwa mabavu inaweza. Itakapojitokeza serikali ya tatu hata mabavu ya CCM yatakuwa yamenywea kutokana na kukosa ngome maalumu.
Ikumbukwe kwamba CCM ndiyo inayodhibiti madaraka katika pande mbili za muungano, kwa maana ya Serikali ya Muungano na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar. Lakini CCM haina uhakika mambo yatakuwaje iwapo Katiba ya Jamhuri ya Muungano itasema kwamba muungano wa Tanzania uendeshwe kwa serikali tatu, Tanganyika, Zanzibar na Tanzania.
Hilo ni jambo linaloitia CCM tumbo joto lakini likiwa limewapa faraja wananchi wa nchi hizi mbili hasa Wazanzibari wanaojiona wamemezwa ndani ya Tanganyika.
Ni jambo la ajabu kwamba Watanganyika hawalalamiki kuhusu nchi yao, Tanganyika. Tangu baada ya muungano Watanganyika walitulia na kuiacha nchi yao isahaulike. Ni Wazanzibari tu, ambao lakini nchi yao iliendelea kuwepo ndani ya muungano, wanaolalamika kwamba muungano uliipokonya mamlaka nchi yao.
Muonekano jinsi ulivyo ni kwamba Wazanzibari wanahisi kama vile iliyokuwa Tanganyika ndiyo iliyoamua kubadili jina na kuwa Tanzania huku Zanzibar ikibaki na jina lake lakini hadhi yake ikishuka na kukalibiana na hadhi ya mkoa. Hilo ndilo tatizo kuu linalowasumbua Wazanzibari.
Wao wanasema kwamba Watanganyika hawapigi kelele kuhusu Tanganyika yao kwa sababu kila kilichokuwa chao walibaki nacho. Watanganyika walibaki na sarafu yao, Benki kuu yao, wakabaki na uhusiano wa kimataifa, wakabaki na kiti chao Umoja wa Mataifa ambako ilipelekwa taarifa tu kwamba Tanganyika imebadili jina na kuwa Tanzania huku kiti cha Zanzibar kikiyeyuka kiana, nakadhalika.
Lakini Zanzibar inaonekana kupoteza vyote ila ikibaki na jina tu ambalo inashindwa kulitumia kufanikisha malengo yake kwa vile sio nchi kamili inayotambulika kimataifa. Hili jina la nchi isiyotambulika ni sawa na kilemba cha ukoka.
Ieleweke kwamba Wazanzibari hawawezi kuendelea kukifurahia kilemba hiki cha ukoka cha kuwa na serikali yao ya mapinduzi, rais wao, Bunge lao – Baraza la Wawakilishi, kama hawayaoni yanayofanana na hayo kwa upande wa washirika wao,  Watanganyika, ili waweze kuyaangalia yaliyo ya muungano wakiwa wameyatofautisha na ya Watanganyika.
Ni dhahiri Wazanzibari wataendelea kuamini kwamba yanayoonekana yakiitwa ya muungano kumbe ndiyo ya Watanganyika. Hata serikali inayoitwa ya muungano kumbe ndiyo serikali ya Tanganyika. Hapo ndipo umuhimu wa seriakli tatu unapojitokeza kama kweli tumedhamiria kuulinda muungano wetu.
Kwa matiki hiyo, malalamiko ya Wazanzibari kwamba wanapunjwa sana ndani ya muungano hayawezi kuisha, wala hayawezi kumalizwa na kilemba cha ukoka cha kwamba Zanzibar ina serikali yake ambayo lakini inatambulika Zanzibar tu. Serikali isiyokuwa na mahusiano ya moja kwa moja na nchi nyingine za nje kwa vile siyo serikali kamili.
Tukumbuke jinsi Zanzibar ilivyokataliwa kujiunga na Jumuia ya Kimataifa ya Kiislamu, OIC, kwa kigezo kuwa siyo nchi kamili wakati Wazanzibari kwa karibu asilimia 98 walikuwa wanakubaliana na mpango huo. Sasa inawezekanaje watu hao wakadaiwa kwamba wana serikali yao ilhali wanashindwa kujiamualia wanayoyata wao kwa kisingizio kwamba hawana mamlaka kamili, mpaka wapate baraka za washirika wao, Watanganyika, kwanza?
Kwahiyo rasmu inayotaja serikali tatu inapaswa kuchukuliwa kwamba ndio muarobaini wa kero hizi za Muungano. Wazanzibari wanataka wakione kilicho chao na kukitambua na iwe haki yao kukitumia kadiri ya matakwa yao yalivyo, kuliko kuendelea kuuziwa mbuzi kwenye gunia. Vilevile wakione na kukitambua kilicho cha washirika wao, Watanganyika.  Ndipo waelewe wanachangia nini kwenye muungano bila upande mmoja kuonekana unaupunja upande wa pili.
Sielewi kwa nini CCM inaona tatizo hapa! Ila ninachoweza kukichungulia na kukielewa, ingawa kimefichwa gizani, ni kwamba CCM wanautaka muungano kwa manufaa ya chama chao, wakati Wazanzibari wanautaka muungano kwa manufaa ya taifa lao. Swali langu liko hivi:  Je, kati ya pande hizi mbili, CCM na Wazanzibari, ni upande upi unaoonekana kuupenda muungano kwa nia njema?
Izingatiwe kwamba muungano ni mali ya watu iliyotengenezwa na watu kwa manufaa ya watu. Katika muungano huu hakuna Umungu wowote uliotumika kuufanya uwepo, haya yalikuwa matakwa ya binadamu tu, tena enzi hizo.
Uliundwa kukidhi mahitaji ya kibinadamu ya wakati huo. Kwahiyo lolote linaweza kufanyika katika kuuboresha ili uendelee kukidhi matakwa ya watu kwa wakati huu tulio nao. Na katika kuuboresha tunaweza kuufanyia marekebisho ya hapa na pale bila kulazimika kuyafuata yote ya wakati ule, wakati unaanzishwa,  kwa vile sababu zilizochochea mpaka muungano huu ukapatikana zimebadilika sana kulingana na mabadiliko ya nyakati.
Sioni sababu ya watu kuendelea kuishi katika karaha kwa madai kwamba sababu zinazowafanya wakarahike haziwezi kubadilishwa kwa vile zimejifunga katika muungano kana kwamba muungano huo umeumbwa na Mungu.
Ni lazima muungano uwepo kuwanufaisha watu, kama kuna mambo yaliyopitwa na wakati na kuwafanya watu wauchoke basi yabadilishwe kwa lengo ya kuyaboresha iliyaende na wakati, au yaondolewa kabisa kusudi watu waendelee kuufurahia muungano. Vinginevyo ngalawa ivunjwe ili kila mmoja aondoke na ubao wake, kwa maana ya kuuvunja muungano. Naamini tutakuwa hatujakufuru maana muungano huu haukuumbwa na Mungu.
0718279346
Next Post Previous Post
Bukobawadau