RAI YA JENERALI ULIMWENGU ;Zipo kanuni za kuleta maendeleo,Kati ya hizo, siyo omba-omba wala kupiga watu wako
NIMEKAA kimya kwa muda kidogo katika kipindi hiki cha mfululizo wa wageni waliokuja nchini mwetu wakiwa na kauli nyingi na tamu kuhusu nia zao za kushirikiana nasi katika nyanja kadhaa.
Kwa kile tulichoweza kukiona hadharani, sisi ambao hatukuingia katika majadiliano ya faragha, ziara hizi zimekuwa za kufana kwa jinsi ambavyo Watanzania walivyojitokeza kuwapokea wageni hao wazito na jinsi wageni nao walivyoonekana kufurahia kuwapo kwao hapa miongoni mwetu.
Hata hivyo maswali kadhaa yamekuwa yakiulizwa kuhusiana na manufaa yatakayotokana na ziara hizi, na si busara hata kidogo kuyapuuza maswali haya. Ni halali kabisa kutaka kujua iwapo heka heka zilizotokea, baadhi zikiwa ni kero kwa wananchi na wakazi wa Jiji la Dar es Salaam, zitazaa faida zinazoeleweka na zinazopimika.
Hili linaweza kuwa suala tata katika mazingira yetu. Kwa sababu za malezi ya hovyo, wananchi wengi wamefanywa kuamini kwamba mandeleo yao yatatokana na misaada na ufadhili wa mataifa ya nje, hasa mataifa ya watu wenye ngozi nyeupe.
Huu ni unyonge tuliojivisha taratibu hadi sasa tumelemaza akili zetu kiasi kwamba hatuthamini uwezo wetu wa kujifanyia mambo yetu wenyewe na kujiletea maendeleo pasipo kupata misaada kutoka kwa Wazungu. Tumejondoa thamani, tumejirahisisha, tumejidhalilisha.
Ishara zote zinaelekea kuthibitisha hali hii ya kujivisha unyonge wakati nchi yetu inazo rasilimali za kutosha kutuinua kama tungeweza kujiheshimu kidogo tu kwa kutambua kwamba uwezo wa kujiendeleza umo miongoni mwetu na siyo kutoka kwa watu wengine.
Tukitaka kuwa wakweli hatuna budi kukubali kwamba, pamoja na mambo mengine mengi, jambo kuu linalodumaza ni akili finyu zinazotuswaga kuelekea utegemezi mkubwa zaidi, hasa katika fikra kuhusu maendeleo.
Kila mara tunaletewa rasimu zinazotokana na mipango iliyofanikishwa na wenzetu wa ughaibuni ambao miongo mitano tulishabihiana nao kwa hali zetu za kiuchumi na kijamii. Hizi ni nchi kama Malaysia, Korea ya Kusini, na nchi kadhaa za Amerika ya Kusini.
Maendeleo huwa hayaigwi kwa kuhaulisha mipango ya nchi moja na kuipeleka nchi nyingine kuitekeleza vivyo hivyo ilivyotekelezwa katika nchi ilikonakiliwa. Yapo mambo mengi yanayosababisha maendeleo ambayo yanatokana na hali ya nchi na watu wake, hali ya hewa na tabia-nchi, utamaduni wa watu wake na uthibiti wa uongozi wa taifa.
Ni kutwanga maji ndani ya kinu kama tutaamini kwamba tunaweza kuchukua walichofanya Malaysia wakafanikiwa na kupandikiza katika nchi yetu bila kuangalia mazingira ya Malaysia wakati wa kipindi chote walipokuwa wakitekeleza mipango yao hiyo.
Nasikia miito inayotolewa leo hii kuhusu “Big Results Now,” nami najiuliza “Where will Big Results come from without Big Ideas, which are born of Big Thinking by Big Men and Women?” Petty thinking never produced big results anywhere. Yatatoka wapi matokeo makubwa kama hatuna tafakuri kubwa, mawazo mapana?
Nimekuwa nikisema tena na tena, na sijachoka kuyarejea hayo ninayoyasema kwa sababu sijachoka, kwamba tunao uwezo mkubwa kama Taifa kwa maana ya rasilimali watu na maliasili lakini tunajiangusha na kuangushana kwa kutojenga uongozi madhubuti wa kuipeleka nchi yetu mbele kwa kasi inayohitajika.
Kwa jinsi hii, tangu aondoke Mwalimu Julius Nyerere nadiriki kusema kwamba (pamoja na makosa yake ambayo siogopi kuyajadili) tumekosa uongozi wa aina ninayoijadili hapa. Tumekuwa na watawala wa aina tofauti tofauti, mara nyingi wakijitahidi kuendeleza walichokikuta bila kuwa na uthubutu wa kufikiri kwa ukubwa wa muono mpana na wa mbali.
Tumekosa kile kinachoitwa kimombo, transformative leadership, na badala yake tumekuwa ni jamii ya “yale yale” kama ilivyotabiriwa muongo mmoja uliopita na kile kijitabu cha “Tutafika,” na hali hii haitatupeka kokote katika siku za karibuni. Tutaendelea kuziruhusu nchi zisizo na rasilimali kama zetu zitupiku, huku tukisubiri Marekani na Wachina waje kutuendeleza.
Hatutaendelea abadan! Na kila tukigundua kwamba hatuendelei tutachukua hatua za kujidanganya kwa kukataa ukweli kwamba tumekwama. Tutatamba kwa kuonyesha vitu vidogo vidogo (vitu vya kawaida kabisa kwa serikali kufanya) na kuvinadi kama “matokeo makubwa” kwa sababu hatukubali kujipima na wenzetu waliofanya mambo kabambe bila kuwa na rasilimali kama zetu.
Ikishindikana kuwashawishi wananchi kwamba wameendelea wakati wanaona hali zao hazina ahueni, na hasa wakidai kwamba umasikini wao unatokana na watawala wao kuwafukarisha na kutowajali, tunaamuru kwamba “wapigwe tu.” Wapigwe mpaka watakapotambua kwamba wameendelea, ama hadi watakapokubali kwamba masikini hana haki ya kulalamika?
Ufumbuzi wa matatizo yetu kwa “kupiga” unaanza kurejea kama utamaduni wetu katika hangaiko la kutafuta majibu mepesi kwa matatizo mazito na ya muda mrefu. Watoto wakifeli darasani, piga. Walimu wakiwa watoro, mkuu wa wilaya ansema “Piga”! Tushangae tu kwa nini yule mkuu wa wilaya aliyewapiga walimu watoro alifukuzwa kazi. Angelifaa kuwa mshauri mkuu wa Serikali katika Idara Kuu ya Kupiga.
Nashauri tena: Twende, tutembee duniani, si kwa ajili ya kufanya “shopping” tu, bali tukajifunze, kutoka nchi zisizo na kitu, na ambazo wananchi wake ni mafukara wa kutupa, lakini zinajenga miundombinu hata Wazungu wanashangaa, kwa mfano Uhabeshi. Tusione haya kujifunza kutoka kwa waliotuzidi kwa umasikini.
Aidha, kama tunataka kupiga, twende katika nchi nyingine tukajifunze jinsi ya kuwachunguza, kuwakamata, kuwashitaki na kuwafunga wote wanaobainika kuwa wala rushwa, ambao hasa ndio wanatakiwa kupigwa, na kupigwa kweli kweli.
Kama kweli tunataka kupiga, haya na twendeni tukapige, na tupige kweli kweli. Tuanze kwa kuwa na sherehe ya bakora kwa wote waliohusikana EPA, Twin Towers, Kiwira, Buzwagi, Deep Green, Mwananchi Gold na wengine katika mikataba yote yenye uvundo
Na tujue kwamba kama vile ambavyo ghala linalosimamiwa na panya haliwezi kutunza nafaka, vivyo hivyo utawala uliojaa rushwa, ubadhirifu na kutojali hauwezi kuleta maendeleo, hata kama wakuu watawapiga wananchi wao mpaka wapigaji wachoke kuliko wanaopigwa.