SIMULIZI ZA MZEE MADIBA; SAFARI YAKE YA KWANZA ILIKUWA KWENDA DAR ES SALAAM!
Na Maggid Mjengwa,
Ndugu zangu,
JUMAMOSI hii nimepata tena wasaa wa kusimulia simulizi za Mzee Madiba. Ni Mzee wetu Nelson Mandela ambaye kwa sasa yu mahututi hospitalini.
Kwenye kitabu alichoandika Mandela mwenyewe; ‘Long Walk To Freedom’, Mzee Madiba anasimulia safari yake ya kwanza nje ya mipaka ya Afrika Kusini.
Wakati huo alikuwa mafichoni kwa vile alikuwa kiongozi mwanaharakati za mapambano ya ukombozi akiwa kwenye ANC.
Mwezi Desemba , 1961, ANC walipokea mwaliko rasmi kutoka
jumuiya ya PAFMECSA ambayo baadae ikaja kuwa Jumuiya ya Nchi Huru Za Afrika, OAU.
Mwaliko ulihusu mkutano wa mwezi Februari mwaka mwaka 1962 mjini Addis Ababa, Ethiopia.
ANC ikamteua Mandela aende kuhudhuria mkutano huo. Lakini, kwa vile alikuwa anawindwa na utawala wa makaburu na polisi wake, safari ya Mandela ilibidi ifanywe kuwa siri kubwa.
ANC iliandaa mkakati wa safari ya Addis Ababa kwa umakini mkubwa. Ikaamliwa kuwa safari ya Mandela kwenda Addis Ababa ianzie Dar es Salaam.
Sasa Mandela anafikaje Dar es Salaam?
Mpango ukawa makamanda wapiganaji watatu wa ANC wakutane kwa siri na Mandela mahali pa siri pale Soweto. Wakutane hapo wakiwa na nyaraka muhimu za kumwezesha Mandela kusafiri nje ya nchi. Wapiganaji hao ni Walter Sithulu, Ahmed Kathrada na Duma Nokwe.
Wa kwanza kufika kwenye eneo la tukio na katika muda waliokubaliana alikuwa Ahmed Kathrada. Ajabu, Mandela na Kathrada wakabaini kuwa Walter Sithulu na Duma Nokwe wanazidi kuchelewa.
Mandela na Kathrada ‘ machale yakawacheza’ kama tutatumia lugha ya mitaani. Haraka ukafanywa utaratibu wa Mandela kusafirishwa kwa gari hadi Bachuana Land. Na huko ilipangwa Mandela akapakizwe kwenye ndege ndogo ya kukodi. Ikafahamika baadae, kuwa Walter na Nokwe walitegewa mtego na makachero wa utawala wa Makaburu , na hivyo, kutiwa mbaroni wakati wakielekea kwenda kukutana na Mandela pale Soweto.
Mzee Madiba anasimulia, kuwa alikuwa na hofu kuu kwenye safari ya gari kuelekea Bachuana Land, alikuwa na hofu kuwa polisi walikuwa wakifuatilia nyendo zake na kwamba wangemkamata kabla ya kuvuka mpaka kuingia Bachauana Land ( Botswana).
Mzee Madiba anasema;
“ Tulivuka mpaka bila matatizo na tukafika mji wa Lobatse mchana huo huo. Hapo nikaikuta simu ya maandishi kutoka Dar es Salaam ikinijulisha, kuwa safari yangu ya kwenda Dar es salaam itachelewa kwa majuma mawili.” ( Nelson Mandela, Long Walk To Freedom, pg.344-345)
Naam, majuma mawili yakatimu, na alfajiri moja, ndege ndogo ikamchukua Mandela kutoka Bachuana Land kuelekea Tanganyika. Ilitakiwa itue kwanza Mbeya.
Walipokuwa kwenye anga ya Zambia, Mandela anakumbuka kumsikia rubani akiita;
“ Mbeya, Mbeya, Mbeya!”
Hakukuwa na jibu kutoka Mbeya.
Na hali ya hewa ikabadilika ghafla. Rubani alikosa mawasiliano, ndege ikawa inayumba sana. Ikafika mahali, rubani ikabidi arushe ndege chini chini akifuata barabara ya gari.
Ghafla kengele ya dharura ya hatari ilisikika ndani ya ndege. Mandela akajisemea moyoni;
“ Huu sasa ndio mwisho wetu”
Hatimaye, tukavuka hali hiyo mbaya ya hewa. Ndege ikapaa kama kawaida. Nikaiona anga iliyo ng’avu, nikaiona milima. Maishani sijapenda kusafiri sana kwenye ndege, na safari ya ndege kutoka Bachuana Land kwenda Mbeya ni moja ya safari za kutisha kuwahi kusafiri.” Anasimulia Mzee Madiba.
Mandela anazidi kusimulia;
“ Pale Mbeya tukapanga chumba kwenye moja ya Hotel za mji. Tuliwaona watu weusi kwa weupe wakiwa wamekaa sehemu moja ya kupumzikia kwenye hoteli huku wakiongea kistaarabu. Kabla ya hapo sikuwahi kuwa mahali pa wazi au kwenye baa ambapo hakukuwa na sehemu maalumu kulingana na rangi za watu.
Hapo hotelini tulikuwa tunamsubiri kiongozi mmoja wa TANU, tuliambiwa kiongozi huyo angekuja kutupokea, anaitwa Mwakangale. Hatukumjua.
Kumbe! Naye alishafika muda mrefu hotelini hapo na alikuwa akitutafuta!” Anasimulia Mzee Madiba.
Naam, kiongozi huyo wa TANU ambaye Mandela hakumjua aliitwa John Mwakangale, alikuwa ni Mkuu wa Mkoa wa Mbeya enzi hizo.
Na baada ya Mbeya, safari ya Mandela ilikuwa ni moja kwa moja kwenda Dar es Salaam. Huko Mandela akakutana kwa mara ya kwanza na Julius Nyerere, tena nyumbani kwake pale Msasani.
Nelson Mandela alipokuwa Msasani kwa Julius Nyerere alishangazwa sana na Julius. Ni yepi hayo yaliyomshangaza Nelson alipokutana na Julius pale Msasani?
Kimsingi Mandela na ANC walitaka wafike Addis Ababa kwenye mkutano walioalikwa rasmi. Ni mkutano wa PAFMESCA ambao ungeshirikisha nchi na viongozi wengi wa nchi za Afrika zilizokuwa huru wakati huo. Ilikuwa ni fursa kwa Mandela kufungua milango ya mawasiliano na viongozi mbali mbali kwa manufaa ya ANC na mapambano yao ya ukombozi kutoka ubaguzi wa rangi.
Na kabla ya kuendelea na kuiangalia safari yake ya kwenda Dar, ebu kidogo tubaki Mbeya, tuone ni jinsi gani Mandela alivyoitafakari nchi yake ya kwanza ya Kiafrika aliyoiona tangu azaliwe. Ikumbukwe,
kwenye safari yake ya Tanganyika, Mandela aliongozana na Bw. Joe Matthews, Mzungu mwanaharakati wa kupinga ubaguzi na mwanachama wa ANC.
Mandela alishangazwa sana na aliyoyaona pale Mbeya, na hususan pale kwenye hoteli waliyofikia. Na hapa Mbeya inaingia katika historia kuwa ni mji wa kwanza wa nchi huru ya Kiafrika uliopatwa kutembelewa na shujaa wa Afrika, Nelson Mandela.
Na kuna Mtanzania anayeingia pia kwenye historia, ni Bw. John Mwakangale, huyu ni Mtanzania wa kwanza, akiwa Mkuu wa Mkoa wa Mbeya na kiongozi wa TANU , ambaye ndiye aliyempokea na kuongea rasmi na Nelson Mandela alipofika Mbeya.
Na pale hotelini Mbeya Mandela alishangazwa kuona kuwa hakukuwa na ubaguzi wa rangi kama ilivyo kwao Afrika Kusini. Mandela alibaini mara moja, kuwa amefika katika nchi inayotawaliwa na Waafrika weusi. Kwamba mzungu hakuwa mtu wa kuogopewa. Na hilo linathibitishwa pale bwana mmoja Mtanganyika mweusi, alipoona Mandela na mwenzake wanashangaa shangaa, ndipo Mtanganyika yule alipokwenda sehemu ya mapokezi ya hoteli na kumwuliza mhusika, dada wa Kizungu;
“ Madam, did Mr Mwakangale inquire after these two gentlemen” Aliuliza huku akiwaonyesha Mandela na Joe Matthews. Anasimulia Mandela.
Bwana yule Mtanganyika alimwuliza dada yule mhusika kwa vile alimwona Mwakangale akifika hapo kuwaulizia wageni wake hao.
“ I am sorry, sir,’ – Samahani bwana, alisema dada yule na kisha akaendelea kusema;
“ He did, but I forgot to tell them”- kwamba ni kweli Mwakangale amewaulizia, lakini nilisahau kuwaambia. Alisema dada yule mhudumu wa kizungu.
Bwana yule Mtanganyika akamalizia kwa kumwambia mhudumu;
“ Please, be careful, madam”- Kwamba , tafadhali dada, uwe mwangalifu.
Ndipo hapo kwa maneno yake, Mandela anasimulia juu ya tukio hilo;
“ I then truly realized that, I was in a country ruled by Africans”- Kwamba ndipo kwa ukweli alipobaini, kuwa yuko kwenye nchi inayotawaliwa na Waafrika.
Na Mandela alijiona, kwa mara ya kwanza maishani mwake, kuwa yuko huru, mbali ya kwamba nyumbani kwao Afrika Kusini ni mtu anayesakwa kwa udi na uvumba na watawala.
Hatimaye safari ya kutoka Mbeya kwenda Dar es Salaam ikawadia. Mandela akawasili Dar es Salaam siku ya pili yake.
Alipofika Dar es Salaam, Mandela akakutana na Julius Nyerere nyumbani kwake Msasani. Ndio, ni Julius Nyerere, Rais kijana kwenye nchi ambayo ilikuwa na mwaka mmoja tu tangu ipate uhuru. Mandela alishangaa kuona Rais anakaa kwenye nyumba isiyo ya kifahari. Alishangaa pia kumwona Rais anayeendesha mwenyewe gari yake. Mandela anasema;
“ I recall that he drove himself in a simple car, a little Austin”- Nakumbuka aliendesha mwenyewe gari ndogo ya kawaida aina ya Austin. ( Nelson Mandela, Long Walk To Freedom, pg. 345- 346)
Naam, ni yepi mengine yalimshangaza Mandela juu ya Nyerere alipokutana naye pale Msasani? Na je, waliongea nini?
Simulizi hii itaendelea