Bukobawadau

UCHAMBUZI : Vikundi hivi vina ajenda gani nyuma yake?


Tanzania kama nchi, inayo matatizo mengi ambayo yamekuwa yakiwasumbua vichwa watu wake na hata viongozi.
Matatizo hayo ni pamoja na ugumu wa maisha, ukosefu wa ajira, ongezeko la idadi ya watu mijini, kupungua kwa uzalishaji wa chakula na mengineyo mengi.
Kama nchi, Tanzania inao vijana wengi ambao hawatumiki vizuri au ipasavyo kwa shughuli zenye tija na zinazoweza kuifikisha nchi mahali inakotaka kwenda.
Vijana hao ni miongoni mwa wanachama wa vyama vya siasa – CCM, CUF, Chadema na vinginevyo ambavyo vimeandikishwa kisheria.
Kwa bahati mbaya, vyama hivi vikubwa vimeanzisha kitu ambacho hakipaswi kupuuzwa na Mtanzania yeyote, mpenda amani.
Kila kimoja kina kikundi cha vijana kilichopewa mafunzo na jukumu eti la kulinda amani kwa viongozi, mikutano na sehemu zozote zinazostahili amani na usalama.
CCM wanawaita vijana wao, Green Guard, CUF Blue Guard na Chadema wameanzisha Red Brigade.
Licha ya kujua kuwa jukumu la ulinzi na usalama ukiwemo wa viongozi na wafuasi wap ni la polisi, vyama hivi vimekusanya vijana wao watiifu waliowapa mafunzo ya ulinzi na kuwakabidhi jukumu la ulinzi.
Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe amenukuliwa akisema chama chake kimechoshwa na vitendo vya kupigwa, kujeruhiwa na kuuawa kwa viongozi na wanachama wao, na hivyo wameamua kuanza kujilinda.
Mbowe anatoa msimamo huo baada ya kumalizika kwa kikao cha dharura cha Kamati Kuu ya chama hicho na kutamka kuwa wao watatoa mafunzo ya ukakamavu kwa vijana wao, ‘Red Brigade’ na zoezi hilo litafanyika nchi nzima kwa nia ya kuimarisha ulinzi wa chama na viongozi wake.
Mbowe akabainisha kuwa Chadema imekuwa ikifanyiwa vitendo vya kikatili vya ama wafuasi wake kukatwa mapanga, kuchomwa visu na kila wanapotoa taarifa, hugeuziwa kibao kwa kukamatwa, kuteswa na kufanyiwa ukatili mwingine.
“Ili kukabiliana na vitendo vya fujo vinavyofanywa na vijana wa CCM dhidi yetu, kamati kuu imeagiza kitengo cha ulinzi kiimarishwe kwa kuhakikisha vijana wote wanapewa mafunzo maalumu ya ukakamavu katika kambi maalumu mikoani,” amekaririwa akisema.
Chadema imeweka hadharani mpango huo wakifuata nyayo za CCM na CUF, ambao walifanya hivyo kimya kwa miaka mingi.
Kwa upande wa pili, CCM kupitia Naibu Katibu Mkuu, Mwigulu Nchemba pamoja na kukiri kuwa vijana wake wamekuwa wakiwekwa kambini katika maeneo mbalimbali nchini kwa ajili ya mafunzo kwa muda mrefu, wanakana kikundi hicho kuwa na malengo ya ulinzi.
Akitetea makambi hayo
Swali la msingi ni hili linalohusu madhumuni ya kuanzishwa kwa vikundi, ni nini zaidi ya kulinda amani kama inavyoelezwa na vyama hivi?
Vikundi hivi havionekani wala kukusudiwa kulinda amani, inawezekana kuwa na ajenda zaidi ya kisiasa.
Ni dhahiri kuwa jukumu la ulinzi wa raia na mali zao ni la Serikali kupitia Jeshi la Polisi na jeshi hilo linapodaiwa limekwepa wajibu huo, ni kwa faida ya nani?
Kwa hiyo, kuibuka kwa vikundi hivi ndani ya vyama vya siasa ni dhahiri ni kinyume cha sheria ambayo imeweka wazi kuwa jukumu la ulinzi na usalama kuwa la Serikali.
Kazi au jukumu la vyama vya siasa ni pamoja na kujadili, kutafuta ufumbuzi wa matatizo ya msingi ya wananchi.
Watanzania wanayo matatizo yao mengi, yakiwemo ukosefu wa huduma bora za kijamii kama majisafi, afya na kadhalika.
Ni wazi kuwa nguvu au fedha zinazotumiwa kuwakusanya vijana na kuwagharimia mafunzo katika kambi za vyama hivyo, zingeweza kutumika kutatua matatizo lukuki yanayowakabili wananchi.
Mfano, vijana kwa umoja wao wakihamasishwa wanaweza kutumika katika kilimo, kuchimba mitaro au visima penye tatizo la maji, kutengeneza barabara, kujenga nyumba za walimu, madaktari na mambo mengine.
Katika hali ya kushangaza, wanasiasa wetu wameamua kukwepa wajibu huo na kufikiria masilahi yao, wanawaza, kubuni vitu vitakavyowagawa Watanzania ilimradi wao wabakie kileleni.
Ninaamini kila chama kinaona na kujua madhara ya uamuzi wao huo wa kuwa na vikundi hivyo visivyokubalika wala kutambulika kisheria.
Wasiwasi wangu ni kuwa pengine wanasiasa wetu wana ajenda za siri nyuma yao katika kuanzisha vikundi hivi

Joyce Mmasi ni mwandishi wa Makala za siasa wa gazeti la MWANANCHI. 0767-253436, joycemmasi@yahoo.co.uk 
Next Post Previous Post
Bukobawadau