Bukobawadau

Rais Kikwete, Kamata Wafanyabiashara wa Madawa ya Kulevya, Nchi Haitatikisika...


Siku za hivi karibu vyombo mbalimbali vya habari vya ndani na nje ya nchi vimekuwa vikiripoti juu ya matukio mbalimbali ya kukamatwa kwa watanzania katika nchi mbalimbali duniani wakisafirisha na kufanya biashara ya madwa ya kulevya. Tutakumbuka kuwa ni hivi karibuni mabinti wawili wa Kitanzania walikamatwa nchini Afrika ya Kusini wakisafirisha kiasi cha 150kg za madawa ya kulevya yenye thamani ya Shilingi 6.8 Bilioni. Hadi sasa watanzania hao wanaendelea kushikiliwa na vyombo vya dola vya nchi hiyo kwa ajili ya kuchukuliwa hatua za kisheria.

Kama hiyo haitoshi hivi karibuni pia kulisambazwa barua kwenye mitandao mbalimbali ya kijamii na JF pia barua hiyo ilikuwepo na watu mbalimbali walipata fursa ya kuitolea maoni barua ile. Katika barua hiyo iliyoandikwa na mtanzania mmoja aliyekamatwa huko Hong Kong akisafirisha madawa ya kulevya kwa niaba ya watanzania wenzake walioko katika magereza huko Hong Kong. Barua hiyo pamoja na mambo mengine imeelezea kuwa kuna kiasi cha watanzania 200 wanaoshikiliwa katika magereza ya huko Hong Kong kwa makosa ya kusafirisha madawa ya kulevya, na kwamba takribani watanzania 130 wameshahukumiwa kutumikia vifungo mbalimbali gerezani huku wengine 70 kesi zao zikiwa katika hatua mbalimbali za usikilizwaji.

Wakati bado watanzania tukiendelea kutafakari juu ya kadhia hii ya vijana wetu kuzidi kujihusisha na biashara haramu ya kusafirisha madawa ya kulevya, jana zikapatikana taarifa nyengine mbili zinazosikitisha sana na kuonyesha ni kwa kiwango gani biashara ya madawa ya kulevya ilivyoshamiri nchini na inavyozidi kushamiri. 

Ya kwanza ilikuwa ni taarifa inayobainisha idadi ya watanzania wanaoshikiliwa ama kutumikia vifungo katika nchi mbalimbali duniani kwa makosa ya kujihusisha na usafirishaji wa madawa ya kulevya. Ikaelezwa kuwa baadhi ya nchi wanakoshikiliwa watanzania hao ni kama vile Brazili-takribani watu 150, Hong Kong-takribani watu 200, China-takribani 15, Pakistani-takribani watu 16 na Afrika ya Kusini-takribani watu zaidi ya 50. Kwa kweli idadi hii ni kubwa sana na inaonyesha namna biashara hii inavyozidi kushamiri na vijana wengi wanazidi kujitumbukiza huko bila kujali madhara wanayoweza kuyapata ikiwa ni pamoja na kuhukumiwa adhabu za kifo kama inavyofanyika nchini China.

Ya pili ni tukio la vijana wawili kujisalimisha katika kongamano la amani lililkuwa limeandaliwa na kanisa la kiinjili na kipentekoste na kufanyikia kanisa la TAG Mbeya. Katika kongamanoi hilo wanafunzi wawili wa vyuo vikuu, mmoja anasoma chuo kikuu cha DSM na mwingine anasoma chuo kikuu cha St. Gasper cha Morogoro walisalimisha kilo tano za madawa ya heroine. Mbali na kujisalimisha vijana hao walitaja mawaziri wawili, Naibu waziri mmoja, wachungaji, baadhi ya wabunge watatu wa viti maalum na wabunge wastaafu wanaomiliki biashara kubwa ndani na nje ya nchi.

Tukio la wanafunzi hao kujisalimisha na kutaja wafanyabiashara wa mmadawa ya kulevya hapa nchini linatufanya wananchi tutafakari na kufikiria namna ya kukabiliana na hii biashara ya madawa ya kulevya. Na pia tukio hilo limezidi kubainisha ni watu wazito/wakubwa kiasi gani walioko nyuma ya hii biashara ya madawa ya kulevya hapa nchini.

Kufuatia hali hiyo nimelazimika kujiuliza nafasi ya serikali yetu ni ipi katika kukabiliana na biashara hii haramu ya madawa ya kulevya. Nikakumbuka kwamba hivi karibuni wakati wa maadhimisho ya siku ya kupambana na madawa ya kulevya waziri mkuu Mizengo Pinda alilitangazia Taifa kuwa sasa madawa ya kulevya ni janga la Taifa na hiyo ilikuwa inatoa picha kwakba tatizo hilo ni kubwa kiasi gani na sisi wananchi kwa umoja wetu tunatakiwa kuchukua hatua madhubuti kukabiliana na janga hilo huku serikali kwa upande wake nayo ikitakiwa kuchukua hatua madhubuti kwa upande wake kukabiliana na wafanyabiashara wakubwa wenye nguvu ya pesa na ushawishi katika jamii wanaotumia nafasi zao kuendelea kufanya biashar hii haramu inayoangamiza nguvukazi ya taifa.

Pia nikalazimika kurejea nyuma na kumtazama raisi wetu katika jitihada zake za kukabiliana na madawa ya kulevya. Nikakumbuka kuwa katika awamu yake ya kwanza aliwahi kunukuliwa akisema kuwa anayo majina ya wafanya biashara ya madawa ya kulevya lakini serikali ilikuwa inachelea kuwakamata kwakuwa kukamatwa kwa watu hao kungeifanya nchi ikayumba. Na kweli tangu wakati huo alipotoa kauli yake tumeshuhudia ongezeko la biashara hii haramu na sasa imefikia hatua watanzania wanaogopeka kila mahali wanakokwenda na hivyo imewalazimu vyombo vya dola katika nchi mbalimbali kuwafanyia upekuzi mkubwa sana tena mwingine wa kiudhalilishaji hii yote ni kutokana na hisia kwamba watanzania wengi wanaosafiri nchi za nje wanajihusisha na biashara hiyo haramu.

Hapa ndipo nimefika nikalazimika kumuandikia raisi wetu wa JMT ambaye pia ni amiri jeshi mkuu wa majeshi ya ulinzi na usalama Dkt. Kanali Jakaya Mrisho Kikwete na kumsihi kwamba sasa ni wakati muafaka kuwakamata watu wote wanaotaajwa kuhusika na biashara ya madawa ya kulevya kwakuwa kuwaogopa kwa hofu ya kwamba nchi itayumba haitusaidii chochote kama taifa bali tunashuhudia ongezeko la biashara hii haramu, kwakuwa wahusika wakuu wako huru na wanafanya biashara hii bila wasiwasi kwakuwa raisi wa nchi ameshawatangazia kuwa hawawezi kukamatwa.

Nimkumbushe raisi wangu kuwa wakati fulani kulikuwa na wimbi kubwa sana la ujambazi hapa nchini na miongoni mwa watu waliokuwa wakitajwa kuwa nyuma ya mipango yote ya ujambazi hasa katika mabenki na vyombo vingine vya fedha ni wafanyabiashara wakubwa pamoja na wakuu vyombo vya usalama lakini raisi hakuona shida kutumia nguvu yake ya kimamlaka kushuighulikia tatizo la ujambazi hadi nchi ikafika mahala ikatulia na wizi wa mabenki ukawa umekwisha kama sio kupungua sana. Kama raisi asingechukua hatua madhubuti ni dhahiri kuwa nchi ingeyumba na pengine kuparaganyika kwakuwa majambazi wangekuwa wanafanya chochote wanachotaka mahali popote na wakati wowote lakini raisi alisimama kidete na kuukomesha ujambazi.

Sasa katika hili la madawa ya kulevya ninamsihi raisi Kikwete asiwaogope wauzaji wa madawa ya kulevya, atumie mamlaka yake ya dola kuwakamata watu wote wanaojishughulisha na biashara ya madawa ya kulevya na kwa uhakika watanzania wote tutakuwa naye bega kwa bega kuhakikisha kuwa biashara hii inatokomezwa kabisa kwa ajili ya ustawi wa nchi yetu. Kwakuwa wauza madawa wamefikia hatua ambayo sasa ni dhahiri wanaiyumbisha nchi ni bora sasa wakamaatwe na kutiwa ndani ili nchi isiendelee kuyumba kwakuwa ikiendelea kuyumba itaishia kuparaganyiika kwakuwa watu hawa hawana huruma hata kidogo na nchi yetu, hawana uzalendo wowote na nchi yetu, hawana uwoga/wasiwasi wowote na nchi yetu. Ni muhimu sasa kwa pamoja kama watanzania tusimame na kuikataa katakata biashara hii na kuwafichua wote wanaojihusisha na biashara hii na serikali iwashughulikie kisawasaw.

Sitaki kuamini kwamba hawa watu wanaweza kutushinda nguvu watanzania wote kama tukiamua kupambana nao. Sitaki kuamini kwamba wakikamatwa nchi hii itayumba, sitaki kabisa kuamini hivyo. Ninamsihi kwa dhati kabisa raisi Kikwete kuwakamata watu wote wanaotajwa kujishughulisha na biashara hii bila kujali kuwa ni wanasiasa wenzake, bila kujali kama ni wafanyabiashara wanaolipa kodi kwa kiasi gani, bila kujali kama ni viongozi wa dini gani. Lazima tuweke mbele na kuyapigania maslahi ya nchi yetu na watu wake hata ikiwa ni kwa gharama kubwa kiasi gani. Tanzania kwanza!!

Naomba kuwasilisha.

MUNGU IBARIKI TANZANIA
MUNGU MBARIKI RAISI KIKWETE ANAPOKWENDA KUINUSURU NCHI NA KADHIA HII YA MADAWA YA KULEVYA.
CREDIT JF.
Next Post Previous Post
Bukobawadau