Bukobawadau

Bungeni sio mahali pa ibada

Na Prudence Karugendo

NAREJEA makala iliyoandikwa na Margareth Simba ikiuliza kwamba “Wabunge CHADEMA wanatafuta umaarafu?” iliyotoka katika Dira ya Mtanzania ya tarehe Agosti 4-7, 2011. Nimelazimika kuirejea makala hiyo kwa sababu nimeona, sisi, tukiwa waandishi ni lazima turekebishane pale panajitokeza upungufu au dosari ili kuufanya mhimili huu wa nne usianze kutia mashaka na kuleta wasiwasi.
Nataka niseme kwamba mazoea hujenga tabia. Watanzania tulizoeshwa kuliona bunge kama chombo cha aina yake na chenye uadhimu usiopaswa kufikiriwa wala kukadiriwa, wananchi walio wengi walibaki kuliona bunge kama bunge bila kuelewa ni namna gani wanavyohusiana na chombo hicho. Sanasana walijua kuwa wanawajibika kupiga kura na kumchagua mbunge, mbunge huyo anaenda kufanya nini kule bungeni na katika mazingira gani, hiyo haikuwa kazi yao kujua.

Wakati huo wananchi wengi walikuwa wamepofuliwa na giza la utawala wa chama kimoja cha siasa. Bunge lilikuwa na kazi moja tu kupitisha mapendekezo ya serikali bila kupinga wala kuhoji lolote. Mwanzoni mwa utawala wa kiimla wa chama kimoja wabunge waliojaribu kuhoji mapendekezo ya serikali sio tu kwamba walifukuzwa bungeni bali hata kuvuliwa uanachama na chupchupu kuvuliwa hata uraia!
Mazoea hayo ya serikali kuburuza kila ilichotaka kifanyike kwa kukipitisha tu bungeni ili kikapigwe mhuri na kuonekana kina baraka za wabunge, ndiyo yaliyowajengea wabunge tabia yenye nidhamu ya upofu inayoendelea kulisumbua bunge letu hata sasa. Tabia hiyo kwa namna fulani inajionyesha jinsi ilivyo na athari badala ya kuonekana ni kitu cha kukifurahia au kujivunia. Hiyo ni kwa sababu hakuna mtu anayeweza kujivunia upofu wala ukilema wa aina yoyote.

Tabia hiyo ya nidhamu ya upofu ilifikia wakati ikalazimisha itolewe kauli ya kwamba bungeni ni mahali patakatifu bila kuzingatia vigezo vya utakatifu! Itakuwaje bungeni pawe pahala patakatifu wakati mule ndani kuna watu wameingia kwa njia zinazokinzana na utakatifu? Wapo wanaoingia bungeni kwa kupora haki za wengine, kuna watu wanaoingia bungeni kwa kuhonga ili wakachaguliwe, kuna wengine wamepora kura za wenzao na hata wengine kufikia kupora kabisa ushindi wa wengine. Je, watu kama hao wanaolazimisha kuingia bungeni kinyume na uadilifu wanaweza wakaendesha uadilifu bungeni kiasi cha kulifanya bunge lionekane ni mahala patakatifu? Na kama dhana ni uwakilishi wa wananchi dhana hiyo kweli itakuwa imesimama mahala pake?
Na je, inawezekanaje mahala patakatifu papitishwe baadhi ya mambo yanayoonekana ni ya kuwajeruhi wanaowakilishwa bila ya wawakilishi kuona haya yoyote? Yapo mambo kama haya ya wawakilishi kujilipa mafao manono, yaliyo nje kabisa ya uwiano wa maisha ya wanaowakilishwa, wakati ikieleweka kwamba waliowatuma wabunge hao wako taabani na ndio haohao wanaobebeshwa mzigo wa kuyalipa hayo mafao manono!
Turudi kwenye hoja ya Margareth Simba. Hoja hiyo inaonyesha jinsi Simba alivyochukizwa na matendo anayoyaona ni mapya ndani ya bunge. Matendo hayo ni yale yanayoonyeshwa na wabunge wa upinzani. Hapa kuna vitu viwili, idadi kubwa ya wabunge wa upinzani ambayo haijawahi kuwepo huko nyuma, na idadi kubwa ya wabunge vijana.

Ni kwamba wabunge wa upinzani, wengi wao wakiwa ni vijana, wameingia bungeni na mishumaa ili kuleta nuru na kuliondoa giza. Mabadiliko yanayoonekana katika bunge kwa sasa yanasababishwa na nuru waliyoileta wabunge hao, haya yanaonekana ni maajabu kwa vile muda mrefu tulikuwa gizani hatuyaoni, kwa waliokuwa kwenye mwanga haya ni mambo ya kawaida kabisa. Wabunge hawa wa upinzani kidogo ni tofauti na wabunge wa chama tawala ambao lengo lao, kwa walio wengi, ni kutaka kuliendeleza giza kwa nguvu ambalo limeishaanza kuonyesha dalili za kutoweka.
Wabunge wa chama tawala wameng’ang’ania kuliendeleza giza lililoanzishwa na chama chao pale kilipoamua kiubabe kuwa chama pekee cha siasa hapa nchini. Kwahiyo hata ndani ya mwanga uliowashwa na mabadiliko ya vyama vingi vya siasa bado wabunge wa CCM wanaamini katika giza!
Tatizo linalojitokeza ni kwamba wabunge wa chama tawala walio wengi wanatokana na makada wa chama hicho waliopufuliwa na giza la muda mrefu lililosababishwa na chama chao, giza la uimla wa chama kimoja, giza ambalo kwa upande mwingine limewaathiri wananchi kwa kiasi kikubwa. Wananchi walijengewa imani kwamba bungeni ni mahali pa wabunge kukaa, kusikiliza na kupitisha kila hoja inayoletwa na serikali bila malumbano yoyote.

Tofauti na imani hiyo potofu, wabunge waliokuja na mwanga, wabunge wa upinzani, wameleta uzoefu mpya wa kwamba bungeni ni mahali pa majadiliano na ikibidi marumbano mpaka kieleweke. Huo ni mwanga, ila tatizo la mtu aliyeishi sana gizani, nusu kipofu, mwanga unamuumiza macho. Ndiyo maana baadhi ya watu wanalalamika kwamba bungeni kuna vurugu, wanashindwa kutofautisha mabishano na vurugu kwa vile hawakuyazoea. Wanauona mwanga ni mbaya kwa vile wamezoea giza.
Kwahiyo alichokisema Simba kwamba ni sinema ya bure kinatokana na tatizo la kulizoea giza, sio kweli kwamba ile ilikuwa sinema, ni kwamba mtu aliyezoea giza akiletwa kwenye mwanga kila kitu atakiona ni sinema. Tukio lile alilolijadaili Simba ni la kawaida kabisa kwa bunge lililozoea kuendeshewa kwenye mwanga, bunge lenye wabunge walio na itikadi tofauti za kisiasa.
Lakini hatahivyo pale si itikadi bali utaratibu wa kiungwana. Mnadhimu wa kambi ya upinzani, Tundu Lissu, alikuwa anatimiza jukumu lake baada ya Naibu Spika kulitumia vibaya rungu la Kanuni za Bunge kuwagongea wapinzani. Naibu Spika alimruhusu Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera Uratibu na Bunge, William Lukuvi, kuhutubia badala ya kutoa taarifa kinyume na Kanuni za Bunge.
Ndipo Mnadhimu wa Kambi ya Upinzani ikambidi afanye kazi yake ya kuomba mwongozo kwa niaba ya kambi nzima ya upinzani. Aliwasha kipaza sauti baada ya Naibu Spika kumnyima nafasi kama kanuni zinavyoelekeza. Tujiulize, kama wabunge wote wa upinzani, ambao kila mmoja anacho kijitabu cha Kanuni za Bunge, wangeamua kwa pamoja kuwasha vipaza sauti kuomba mwongozo juu ya kanuni iliyokuwa ikikiukwa na Lukuvi kwa kushirikiana na Ndugai, hali ingekuwaje pale ukumbini? Maana tayari wabunge hao walikuwa wanaumizwa na hotuba ya Lukuvi ambayo kikanuni haikuwa mahala pake.
Kwahiyo kitendo cha Lissu tayari kiliidhibiti nidhamu ya wabunge wa kambi ya upinzani na kuwafanya wasiamue wote kuwasha vipaza sauti kulalamikia kitendo cha Naibu Spika kumwachia Lukuvi kuhutubia badala ya kutoa taarifa, kama inavyotakiwa, na hivyo kuonyesha upendeleo wa dhahiri kitendo ambacho ni ukiukaji wa Kanunim za Bunge.
Kwahiyo alichokifanya Lissu, kama mwanasheria mahiri, sio kwamba kililenga kuidhibiti tu nidhamu ya wabunge wa kambi ya upinzani bali pia kumuonyesha Naibu Spika kuwa kajisahau na kutoka nje ya msitari. Ni kwa nia njema kabisa iliyokuwa imejaa weledi. Isipokuwa tatizo giza lilishatuathiri sana, Ndugai akiwa naye ni muathirika.
Lakini hata hivyo tukumbuke kwamba kanuni nyingi za bunge bado zinaandamwa sana na vinyemelea vya uimla wa chama kimoja cha siasa. Uimla huo ulikuwa tatizo baya sana mithili ya ugonjwa wa UKIMWI.
Kwa maana hiyo hatunabudi kuelewa kwamba kanuni hizo ni tofauti na kanuni zitumikazo kwenye ibada, bungeni ni mahala tofauti na kanisani au msikiti. Sehemu za ibada ni mahali ambako waamini huenda kwa ajili ya kuabudu bila kuhoji lolote katika taratibu za ibada. Hiyo ni tofauti kabisa na bungeni.
Kanuni za Bunge zimewekwa na wanadamu kulingana na matakwa ya wakati pamoja na mapenzi ya wahusika, taratibu hizo zinaweza kufuatwa lakini hazipaswi kuabudiwa. Ndiyo maana nawashangaa wanaokichukulia kitendo cha Lissu na wenzake kama kufuru!
Margareth Simba anadai wananchi waliokuwa wanamsikiliza Lukuvi, wakati Kanuni za Bunge zikiwa zimekiukwa, waliachwa hewani! Sielewi ana uhakika gani na hilo maana Lukuvi alikuwa anajaribu kukanusha mambo mbalimbali yaliyokuwa katika hotuba ya Waziri Kivuli wa Mambo ya Ndani, Godless Lema. Baadhi ya wananchi nikiwemo hata mimi, tulikuwa tunaumizwa na maelezo ya Lukuvi yaliyokuwa yamekaa kisiasa zaidi tofauti na hali halisi ya mambo ilivyokuwa.
Mfano wakati Lukuvi akikanusha kuhusu chanzo cha ajali nyingi za barabarani, akiwa amelenga kulishawishi bunge liamini kwamba pengine ajali alizokuwa akiziongelea Lema ni uzushi, ajali mbaya ilitokea mkoani Kilimanjaro na kuua makumi ya wananchi. Pengine hiyo ilikuwa hasira ya Mungu dhidi ya taarifa yenye upotoshaji iliyokuwa inatolewa na Lukuvi.

Simba anasema wananchi wanajutia maamuzi waliyoyafanya ya kupeleka watu kama Lissu bungeni! Sielewi ni wananchi wa wapi hao ambao wanaweza kuonyesha maajabu ya kiasi hicho. Maana pamoja na giza lililowasumbua kwa kipindi kirefu lakini sidhani kama wapo wananchi waliofikia kupofuka macho pamoja na akili kiasi hicho. Wananchi wamchukie mtu anayetetea uhai wao ila wamuone yule anayeeneza propaganda za kuwa hali ni salama huku wakizidi kuteketea kuwa ndiye mwema kwao!
Tuseme hata wale watu waliokufa katika najali iliyotokea wakati ule ule Lukuvi akikanusha kwamba hakuna ajali zinazotokea nao walikuwa wanampendelea Lukuvi na kumuona Lissu mbaya?
Katika uandishi kawaida huwa najitahidi sana kutoonyesha kwamba alichokiandika mwandishi mwenzangu hakifai, ila nionyeshe hapa kwamba Simba alifikia mahali akatumia maneno kama “kuropoka na wavuta bangi” akiwa amewalenga wabunge wetu! Kwakeli hapo nimekwazika. Ni kwa sababu Simba hakuyataja hayo maneno aliyoyafananisha na ya waropokaji au wavuta bangi. Bilashaka huu ni uandishi ulio nje kabisa ya uadilifu na kanuni za uandishi.

Kitu ambacho angetukumbusha Simba ni pale, kwa mfano, Kanuni za Bunge zinapotumiwa kimaajabu, mbunge wa Tarime (CCM) alitamka bungeni kuwa atawahamasisha wapiga kura wake wabebe mapanga na kwenda kuwachinja wawekezaji, Naibu Spika akasimama na kuishadidia kauli hiyo kwa furaha akisema kwamba hiyo ndiyo lugha ya watu wa Mara. Mbunge huyo aliachiwa aendelee na mchango wake.
Lakini mbunge wa Nyamagana (CHADEMA) alipotaka kutoa taarifa ya dharura juu ya hatari ya kuingizwa nchini samaki wenye mionzi ya nyukilia akafukuzwa bungeni! Sasa Simba atueleze, kuropoka kuko upande gani na matendo yanayofanana na ya wavuta bangi yako upande gani.
Nimalizie na kauli ya Lukuvi ya uchochezi unaoweza kusababisha chuki kati ya serikali na wananchi wake. Hapa inabidi tuielewe dhana ya upinzani. Upinzani si kupinga tu bali pia kuwashawishi wananchi kuichukia serikali iliyo madarakani ili baadaye ukifika wakati wananchi waiondoe serikali iliyopo kwa kura na kuwaweka wapizani. Wapinzani wasipoichonganisha serikali na wananchi upinzani utakuwa hauna maana yoyote zaidi ya kuisindikiza serikali kuelekea kusikojulikana.
Vyovyote iwavyo bungeni si mahali pa ibada tunakotakiwa kuabudu kwa kufuata tu kanuni zilizopo, bungeni ni mahali pa majadiliano, mabishano na hata marumbano mpaka kieleweke.
prudencekarugendo@yahoo.com
0784 989 512
Next Post Previous Post
Bukobawadau