Dar es salaam kama kinyonga inabadilika sura kulingana na mahitaji ya wakati
Na Prudence Karugendo
KINYONGA ni mdudu aliyejaliwa uwezo wa kujibadilisha rangi kulingana na mahali alipo, akiwa katika sehemu iliyo na kijani kibichi atabadili rangi yake iwe ya kijani kibichi, akiwa kwenye sehemu ya kahawia atabadili rangi naye awe kahawia nakadhalika. Maumbile hayo ya kinyonga ndiyo yanayomwezesha, katika mwendo wake wa kusuasua, kujipatia riziki kirahisi kwa kuyavizia mawindo yake akiwa amejifananisha na mahali alipo hivyo kukosa kugundulika kiwepesi na kile anachokuwa anakiwinda. Huyo ni kinyonga mdudu asiye na kasi katika mambo yake.
Tofauti na kinyonga, wanadamu tumejaliwa uwezo wa kila aina, tunaweza kuwa na kasi tukitaka, tuna maarifa pamoja na akili za kutuwezesha kutengeneza mbinu mbalimbali za kukabiliana na maisha tuliyomo bila ulazima wa kujibadili ili tufanane na mahali tulipo. Hiyo inamaanisha kwamba wanadamu tunao uwezo wa kupata riziki bila kujibadili maumbile yetu wala kuubadili mwonekano wa mazingira yetu.
Ukweli huo unatusuta Watanzania ambao muda wote tumejikita katika kuyabadili mazingira yetu, bila kujali ni uharibifu kiasi gani tunausababisha, kwa tamaa ya kupata riziki pasipo kutumia uwezo wa akili zetu tulizojaaliwa nazo.
Tamaa ya kupata riziki kwa njia ya mkato, mbali na kutufanya tuyaharibu mazingira yetu, pia inatufanya kuiharibu historia yetu na hivyo kutufanya tupasahau tulikotoka. Tunabaki kuvizia riziki kwa kulazimisha kufanana na mahali tulipo kama afanyavyo kinyonga.
Kwa hapa nataka niuangalie uzembe huo tulio nao kwa kulitumia Jiji la Dar es salaam. Jiji la Dar es salaam limekuwa likibadilika sura kila baada ya muda mfupi na kuelekea kupoteza kabisa sura yake ya asili kitu kitakacholifanya lisiweze kuwa na historia inayojionyesha.
Limekuwa jambo la kawaida sasa kwa Jiji la Dar es salaam kubadilika sura na rangi katika kipindi cha mwezi mmoja kiasi kwamba, hata kwa mtu aliyelizoea jiji hilo anaweza kupotea njia iwapo atakuwa nje ya jiji kwa kipindi kisichozidi mwezi mmoja.
Maana mtu anatoka akiiacha sehemu fulani ni eneo la wazi lakini anarudi baada ya mwezi mmoja anakuta katika sehemu hiyo tayari kuna mnara wa jengo unaokaribia mawinguni! Au sehemu nyingine kunabomolewa jengo muhimu la kihistoria na kujengwa mnara kwa madai ya kwamba minara ndio ujenzi wa kisasa bila kujali kwamba usasa inabidi utokane na historia ya sehemu husika. Tunabomoa historia kutengeneza usasa, kituko cha aina yake!
Kwa upande mwingine wapo watu wanaoyaona mabadiliko hayo yaliyolikumba Jiji la Dar es salaam kama sehemu ya maendeleo bila kuelewa kwamba mabadiliko hayo yanasukumwa na na tamaa ya kujipatia riziki kwa kujibadilisha rangi kama kinyonga. Kinyonga atajibadilisha rangi atapata riziki yake lakini atabaki ni kinyonga. Kwahiyo kubadilika rangi kwa kinyonga kamwe hakuwezi kuitwa maendeleo.
Ninachoweza kukiita maendeleo ni huduma za kijamii zinazotokana na kodi za wananchi. Kwa hali yoyote ile siwezi kuiona minara inayoota kama uyoga jijini Dar es salaam, hasa ile iliyoota kwenye maeneo yetu ya kihistoria, kama maendeleo. Maendeleo gani yasiyomnufaisha kwa namna yoyote mwananchi mlipa kodi? Mwananchi wa kawaida ananufaikaje na minara hiyo?
Kinachohitajika kwa mwananchi na kuonekana ni maendeleo akiwa katika jiji lake ni miundombinu bora itakayomrahisishia mawasiliano na shughuli zake. Mfano jiji liwe na vyoo vya umma vilivyotokana na jasho lake, kwa maana ya kodi anayoilipa kila wakati, wala siyo vyoo vya kulipia vinavyojengwa kwa mtindo wa kufa kufaana. Kwa nini mwananchi alipe kodi halafu alipie huduma ya choo wakati kodi yake ndiyo inayotakiwa kumhakikishia miundombinu salama zikiwemo huduma za vyoo?
Mwananchi anahitaji busitani nzuri anakoweza kukaa na kupumzika baada ya mizunguko mingi ndani ya jiji nakadhalika. Lakini kitu hicho hapa Dar ni kama anasa isiyo na umuhimu wowote, watu wanazunguka wakiiangalia minara tu bila mahali pa kupumzikia.
Simtarajii mwananchi aliyechoka na kukosa mahali pa kupumzikia kwa vile maeneo mengi yaliyopaswa kuwa busitani za kupumzikia yamejengwa minara, mwananchi anayepatwa na haja ndogo au kubwa lakini asipate pa kujisitiri, aione minara hiyo inayoota kama uyoga kuwa ni maendeleo. Maendeleo kwa lipi?
Duniani kote miji yote iliyoendelea na kusitarabika inakuwa na mionekano inayojulikana. Picha fulani ikionyeshwa mara moja mtu anasema hapa ni London, New York, Paris nakadhalika. Hiyo inatokea hata kwa mtu ambaye hajawahi kuitembelea miji hiyo isipokuwa kuziangalia tu alama za miji hiyo zisizobadilika. Unakuta miji hiyo inazo amala au majengo ambayo hayajabadilika kwa kipindi cha zaidi ya miaka 100. Ni miji inayotunza historia yake. Hilo ni jambo ambalo Dar es salaam haitakaa iwe nalo hata ikipita miaka 2000 kama mwenendo huu wa sasa utadumu.
Mfano, wakati London ya miaka 50 iliyopita ndiyo London ileile ya leo, tunaweza kuona kwamba Dar es salaam ya mwaka 1985 ni tofauti sana na Dar es salaam ya sasa. Mambo mengi yamebadilika na mengine kupotea kabisa ikiwemo historia iliyokuwa ikijieleza wakati ule kubadilika na nyingine kufutika na kupotea kabisa. Hivi kweli mabadiliko ya aina hiyo ndiyo tunayoweza kuyaita maendeleo? Maendeleo yanayofuta historia?
Ninavyoamini mimi ni kwamba maendeleo yanatakiwa yawe ni kuendeleza sehemu ambazo hazijaendelezwa, lakini siyo kubadili au kufuta maendeleo ambayo tayari yapo. Huko si kuendeleza bali kuharibu maendeleo.
Mji unaweza kuendelezwa kwa kuyatumia maeneo ambayo yanakuwa bado hayajaendelezwa na kuachwa jinsi yalivyo maeneo ambayo yaliendelezwa awali huku historia ikiwa imetunzwa. Maendeleo ya aina hiyo yana mvuto wa aina yake, na ndiyo yanayoipa mvuto wa pekee miji ya Bamako na Zanzibar.
Ikumbukwe kwamba historia huandikwa na matukio ya nyakati. Lakini ikitokea tukio moja linalifuta tukio lingine, kwa maana ya tukio la nyuma kulituta tukio lililotangulia kamwe hatuwezi kupata historia isipokuwa kitu kinachojibadilibadili sura na rangi mithili ya kinyonga.
Nchi yetu imepitia katika vipindi mbalimbali ambavyo inabidi viwe katika historia, kimaandishi na kimwonekano. Tulianza tukijitawala kijadi, mara ukaja utumwa, mara ukaja ukoloni, tukatawaliwa na Wajerumani na baadaye Wangereza. Baadaye tukapa uhuru wetu, tukajitawala. Kisha likaja Azimio la Arusha na sasa tumo ndani ya ufisadi.
Kwahiyo tutakuwa hatuitendei kaki historia iwapo tutaruhusu matukio ya nyuma kuyafuta yaliyotangulia. Mfano kuuacha ufisadi ulifute Azimio la Arusha, hata kama halifanyi kazi kwa sasa, lakini mabaki yake kuonekana ni muhimu sana kihistoria.
Tunakumbuka kuna majengo yaliyotaifishwa baada ya Azimio la Arusha. Majengo hayo yaliwekwa chini ya kilichoitwa Msajili wa Majumba kabla ya kuunganishwa kwenye Shirika la Nyumba la Taifa. Mengi ya majengo hayo yanatunza historia kwa kutukumbusha Azimio la Arusha.
Lakini kwa sasa baadhi ya majengo hayo yanabomolewa kwa kasi kubwa kupisha minara ambayo nayo ni lazima inatuweka kwenye kipindi kingine cha historia. Bilashaka minara hii itabaki ikitukumbusha kipindi ambacho nchi yetu ilikuwa ikipita kwenye wimbi kubwa la ufisadi. Ndiyo, hiyo nayo ni historia. Lakini historia ya ufisadi haikupaswa kuifuta historia ya moyo wa uzalendo ambapo serikali iliona umuhimu wa kutaifisha mali binafsi na kuzifanya mali za umma.
Kwahiyo wanaoona umuhimu wa kutengeneza historia mpya kwa njia ya maendeleo wangefanya hivyo bila kuiathiri historia iliyokuwepo, hiyo ni kwa vile historia ni kitu endelevu ambacho hakikatiki na kuanza upya. Tukio moja linapolifuta tukio lingine mtiririko wa historia unakuwa umepotea. Na kwa mtindo huo wa matukio kuyafuta matukio mengine kinachoitwa maendeleo kitakuwa kinaelea kwa vile kitakuwa hakiko kwenye msingi wa historia.
Nimalizie kwa kusema kwamba haya mabadiliko yanayojionyesha katika Jiji la Dar es salaam binafsi siyafurahii hata kidogo, sababu ni mabadiliko ya kinyonga. Kinyonga kujibadili rangi kufanana na mahali alipo si kwa kupapenda mahali pale bali kwa kuvizia mawindo yake. Kwahiyo hata haya mabadiliko ya Jiji la Dar es salaam siamini hata kidogo kama yanasukumwa na moyo wa kweli wa wahusika wa kulipenda jiji letu, isipokuwa ninachokiona ni mbinu zilezile za kinyonga za kuyavizia mawindo yanayonaswa kirahisi katika mabadiliko hayo.
0784 989 512