Bukobawadau

HII NDIYO STORY YA BOMOA BOMOA MUHIMBILI JENGO LAREGENT STORE

 Shirika la Afya Muhimbili liliingia mkataba wa pango na REGENT STORE mnamo mwaka 1987 ambapo katika mkataba huo makubaliano yalikuwa kwa REGENT STORE kujenga jengo ili litumike kuendesha biashara ya SUPERMARKET katika eneo la Hospitali kwa ajili ya mahitaji ya wagonjwa pamoja na wafanyakazi.
Mkataba huo ulikuwa wa miaka mitano yaani kuanzia mwaka 1987 hadi mwaka 1992 ambapo REGENT STORE alitakiwa kuwa ameishajenga jengo husika pamoja na kuendesha biashara ya SUPERMARKET katika hilo jengo kwa kipindi cha miaka mitano na kukabidhi jengo kwa Hospitali.
Kilichotokea:

Hata hivyo, baada ya miaka hiyo mitano kuisha, REGENT STORE hakukabidhi jengo hilo kwa Hospitali kwa mujibu wa mkataba kwa madai kuwa alikuwa hajarudisha gharama zake za ujenzi. Kutokana na madai hayo kuwa alikuwa hajarudisha gharama zake za ujenzi, Hospitali ilikubali kumwongezea muda wa miaka mitatu kuanzia 1992 hadi 1995.

Pamoja na Hospitali kumwongenzea miaka mitatu, ilipoisha miaka hiyo mitatu, REGENT STORE hakuonesha nia ya kukabidhi jengo kwa Hospitali, na badala yake aliendelea kulitumia bila ya mkataba wa aina yoyote na bila kukubali kukaa mezani
 Mgawanyo wa Mali na 1995-2000 Kama mnakumbuka katika kipindi cha mwaka 1995 hadi 2000 kulikuwa na mchakato wa kulivunja lililokuwa Shirika la Afya Muhimbili (MMC) ambalo kwa wakati huo lilijumuisha Hospitali pamoja na Chuo Kikuu cha Tiba. Zoezi ya kulivunja Shirika la afya Muhimbili lilienda sambamba na kufanya mgawanyo wa mali na madeni ya shirika hilo, na kutokana na mchakato wa mgawanyo kuendelea suala la kufuatilia kuchukua jengo lililokuwa linakaliwa na REGENT STORE lilisimama kusubiri mgawanyo ukamilike ili aliyegawiwa eneo hilo ndio afuatilie.
Baada ya mchakato huo kukamilika, Hospitali ya Taifa Muhimbili iliundwa na kupewa hadhi ya kuwa shirika la umma kwa mjibu wa Sheria ya Bunge Namba 5 ya Mwaka 2000.

Kwa bahati nzuri pia, katika mchatako huo wa kuligawa Shirika la Afya Muhimbili uliojumuisha mgawanyo wa mali na madeni, jengo hilo la SUPER MARKET ilipewa Hospitali ya Taifa Muhimbili kama inavyoonekana katika Gazeti la Serikali No. 62 ya 2007.
Hatua iliofuata: Kufuatiwa hatua hiyo, Hospitali ya Taifa Muhimbili kupitia Mwanasheria wake ilimwandikia barua ya notisi yenye Kumb. CK/GC/2005/I/II/466 ya tarehe 26, Machi 2005 ikimtaka REGENT STORE akabidhi jengo kwa Hospitali katika kipindi cha siku 14 na kwamba kushindwa kufanya hivyo kutapelekea kuchukuliwa hatua za kisheria.

Ndugu Wanahabari na Wananchi kwa Ujumla:

Baada ya kupokea barua hiyo, REGENT STORE aliamua kwenda Mahakama Kuu ya Tanzania, Kitengo cha Ardhi na kufungua kesi dhidi ya Hospitali ya Taifa Muhimbili ambayo ilisajiliwa kama Land Case No. 53 ya mwaka 2005. Katika kesi hiyo, REGENT STORE alikuwa akiomba pamoja na mambo mengine; Amri ya Mahakama kuwa notisi aliyopewa ya kuondoka katika jengo hilo ni kinyume na sheria; Aliomba Amri ya Mahakama kurekebisha mkataba ili aendelee kuwa mpangaji halali na aliomba pia Amri ya kudumu ya Mahakama kuizuia Hospitali ya Taifa Muhimbili kumwondoa REGENT STORE katika jengo hilo hadi pale mkataba utakaporekebishwa.

Mchakato wa Mahakamani:

Kesi hii imekuwa Mahakamani kwa kipindi cha miaka nane tangu mwaka 2005 na hatimaye tarehe 20 Agosti, 2013, Mahakama Kuu imetoa HUKUMU ambapo maombi yote ya REGENT STORE yametupiliwa mbali na REGENT STORE ameamuriwa kulipa gharama za kesi na kutoka katika jengo mara moja.

Utekeleza wa HUKUMU utaendelea kwa mujibu wa sheria ili Hospitali ya Taifa Muhimbili ipate matunda ya hukumu ambayo ni haki ya kuendelea kumiliki MALI YAKE.

TUNAPENDA KUTOA SHUKRANI KWA MAHAKAMA KWA KUSIKILIZA KESI HII NA KUTENDA HAKI KWA KILA UPANDE.
Next Post Previous Post
Bukobawadau