Bukobawadau

KITONGOJI CHA RWENGIR,KIJIJI CHA BUGANGO KATA KAKUNYU WAILAYA MISSENYI WAWEKWA KANDO KUPATA HUDUMA ZA JAMII

KAMA ilivyo kawaida kwa wakazi waishio mipakani, wakazi wa Kitongoji cha Rwengiri, kilichoko Kijiji cha Bugango, Kata ya Kakunyu, Wilaya ya Missenyi, Kagera utegemezi wao wa huduma za kijamii hutokana na miundombinu iliyopo katika eneo husika.

Kitongoji hicho kimepakana moja kwa moja na mpaka wa Tanzania na Uganda.

Wakati mpaka wa nchi hizi mbili uliponyooshwa mwaka 2004 uliwafanya baadhi ya jamii kutoka nchi alikozaliwa na kuhamia nchi nyingine na baadhi ya vituo vya biashara vya upande wa Tanzania vilijikuta vimepelekwa upande wa Uganda, mathalani kituo cha biashara cha Bugango, ambapo maduka mengi yalipelekwa Uganda.

Hivyo imebidi wananchi wa upande wa Tanzania kulazimika kufuata mahitaji yao ya lazima (bidhaa ya madukani) upande wa pili wa mpaka na huku wakitumia sarafu za Tanzania kwa hisani ya wafanya biashara wa Uganda.

Wafanyabiashara hao wenye maduka aidha, hubadilisha sarafu za Tanzania kwa viwango wavitakavyo kama vile sh 100 za Tanzania ni sawa na sh 60 za Uganda kama alivyoweza kueleza mkazi mmoja wa Kijiji cha Kakunyu, William Petro (29).

Petro anasema: “Mahitaji muhimu tunayapata Uganda nashukuru sijawahi kuulizwa kitambulisho,” anasema.

Mkazi wa Kitongoji cha Rwengiri, Kijiji cha Bugango aliyejitambulisha kwa jina la Kaiza, anasema wanapata matatizo mbalimbali linapokuja suala la huduma za jamii.

Anasema: “Tunayo matatizo makubwa, watoto wetu hutembea zaidi ya kilomita 30 hivi kuhudhuria masomo katika shule iliyoko Bugango (makao makuu ya kijiji).

“Baadhi ya watoto hupata hifadhi kwa jamaa zetu. Hatuna huduma za afya, wanawake hupata shida kwenda kliniki kwa kutembea umbali mrefu,” anasema.

Kaiza anasema huwa wanalazimika kufuata huduma hizo Uganda wakati mwingine unyanyapaliwa kutopata huduma, hata shule kwa watoto wetu hususan tunapofahamika kutokea upande wa pili (Tanzania) na ambao hauna huduma hizo,” anamaliza.

Maelezo zaidi ya wakazi hao ni kuwa huchota maji katika vidimbwi yaliyotuhama wakati wa mvua.

Matatizo mengine anasema ni miundombinu ya barabara ambapo wao hutegemea zaidi njia za uchochoro zinazoaminika kupitika zipo upande wa pili, mtu anapotaka kwenda au kutoka Rwengiri kutokezea katika kituo cha Bugango hutumia usafiri wa pikipiki au gari kwa kupitia barabara ya upande wa Uganda.

Uchunguzi umebaini kuwa wanafunzi waishio mpakani na hasa kwa upande wa Tanzania, watoto hao wanawekwa katika ‘mtanziko’ wa mitaala ya nchi hizi mbili, wengine wakisomea Uganda na baadhi kusomea Tanzania.

Kaimu Meneja wa Mamlaka ya Mapato wa Mkoa wa Kagera Marya Magere, alipoulizwa kuhusiana na biashara mkapani hapo anasema: “Biashara inayofanyika katika maeneo ya huko ni biashara ndogondogo, inayowasaidia wakazi wa mpakani kupata mahitaji yao kwa urahisi.

“Sioni kama kuna madhara, kwa vile hata makubaliano yaliyokwisha kufanyika ya Afrika Mashariki ni pamoja na kuondoa urasimu wa biashara ya wakazi waishio mpakani.”

Sambamba na maelezo hayo, wataalamu wa mambo ya kibenki hususan Benki ya Taifa ya Biashara (NBC) na Benki ya Makabwela NMB, matawi ya Bukoba wanasema muingiliano wa sarafu wa nchi hizi za Afrika Mashariki hauna madhara kwa vile sarafu hizo hurudi tena kwenye nchi husika.

Wataalamu hao wanazidi kueleza kuwa muda si mrefu kutakuwepo na maduka ya kubadilisha fedha sehemu za mpakani hususan katika mji mdogo wa Mtukula kwa nia ya kurahisisha huduma hiyo ya kifedha, isipokuwa hatari iliyopo kwa sasa katika kubadilishana sarafu kienyeji miongoni mwa wakazi wa mpakani ni kubadilishiwa na watu wasio rasmi.

Wanasema watu hao wasio rasmi wakiamua kutandaza fedha za kigeni hadharani bila kufuata utaratibu wa kibenki, kunaweza kudhoofisha mzunguko wa sarafu.

Kwa upande wa upatikanaji wa huduma za jamii hususan elimu kwa wakazi wa mpakani, Kimolo ambaye ni Mshauri wa Katibu Tawala wa Mkoa wa Kagera upande wa Elimu anasema: “Watoto wanaosomea Uganda hiyo ni hiari ya wazazi kuwapeleka watoto wao huko, na juu ya utofauti wa mitaala kati ya nchi hilo siwezi kulisemea kwani kila nchi ina utaratibu wake wa kimitaala.”

Kuhusu watoto wanaotembea mwendo mrefu zaidi ya kilomita 30 kutoka Kitongoji cha Rwengiri kwenda na kurudi kutoka shuleni anasema: “Sina habari nitalifanyia kazi suala hilo.”
Next Post Previous Post
Bukobawadau