Bukobawadau

KUMBUKUMBU YA MIAKA MITATU YA KIFO CHA MAMA YETU MPENDWA MAGRETH SALVATORY KALABAMU (MAMA SANDE) 16/8/2010 – 16/8/2013

Ilikuwa saa 10.00 alfajiri, tarehe 16 Agosti 2010 ulipotutoka. Nakumbuka nilipoambiwa kuwa Bwana Amekutwaa, nilidhani ni ndoto tu. Japo uliugua ghafla (siku 10 tu) lakini ulionyesha ujasiri, uvumilivu, imani kubwa na sura ya tabasamu, sote tuliamini kuwa siku moja ungepona ukawa mzima. Mama, japo leo ni miaka mitatu tangu ututoke, bado nahisi niko ndotoni na nimeshindwa kabisa kukubaliana na ukweli kwamba haupo nasi. Mara kwa mara nakuona ndotoni, lakini ninapoamka nagundua ni ndoto tu, na hiyo inazidisha uchungu na majonzi.

Baba yetu, Mzee Salvatory Kalabamu, uliyeishi naye katika ndoa kwa miaka 41 anaendelea kukukumbuka mno. Kwani ulikuwa ni rafiki yake mkuu, mtu wake wa karibu kabisa na kila kitu kwake kama ilivyo kwetu sisi wanao; Asella (Sande), Agripina, Pendo, Shubi, Muga, Elpidius, Eutropia, Victor, Nivard na Anita tumeendelea kuwa na wakati mgumu kwa vile wewe ulitupa mapenzi makubwa na malezi bora. Tulikutania, tulicheka, tuliimba nawe, tulikusaidia kazi za nyumbani na tulijivunia kuwa na mzazi mwenye upendo kama wewe.

Japo siku zote tangu ututoke tumekuwa na wakati mgumu sana,siku hii ya leo tunapoadhimisha miaka mitatu ya kifo chako ni ngumu zaidi kwetu. Inaleta kumbukumbu zisizoelezeka na zisizostahimilika.

Kazi ya Mungu haina makosa.Tukijiuliza sana kwanini alikuchukua wakati bado tunakuhitaji sana tutakuwa tunakufuru.Tunajaribu kujifariji kwa kuamini kuwa alikuchukua kwa vile alikupenda zaidi yetu. Na tunajitahidi pia kujiridhisha kuwa huko ulipo unapata pumziko la amani na unaangaziwa mwanga wa milele ukistarehe kwa amani. Japo haupo nasi kimwili lakini siku zote tupo nawe kiroho.

Pumziko la Milele Akupe Ee Bwana na Mwanga wa Milele Akuangazie Upumzike Kwa Amani, Amen.
Agripina Kalabamu
a.k.a Mrs. Audax Barongo (Mama Alex)
Next Post Previous Post
Bukobawadau