Bukobawadau

Nchemba, hata shetani hutajwa mara nyingi

 Na Prudence Karugendo
Naibu Katibu Mkuu wa CCM Bara, Mwigulu Nchemba, kaandika kwenye mtandao wa kijamii,  kwa njia ya kutamba, akionesha kuwa kutajwatajwa kwake mara nyingi, hasa kwenye vyombo vya habari, kunadhihirisha mafanikio yake aliyoyapata mpaka sasa katika umri wake mdogo alio nao.
Mwigulu anazidi kutamba, huku akijilinganisha na Katibu Mkuu wa Chadema, Dk. Wilbrod Slaa, kwamba katika umri wake wa miaka 34 anatajwatajwa kiasi hicho, je, akija kufikia umri kama alio nao Dk. Slaa kwa sasa hali itakuwaje?
Kwa upande wangu, katika watu ambao nilikuwa najizuia kujadili mienendo yao ni pamoja na Mwigulu Nchemba. Sikutaka kujadili mwenendo wa Nchemba kwa vile unaonekana kuwa na utata mwingi ambao kuujadili pengine inabidi mtu apate kilevi kwanza.
Niwe muwazi, nimuonavyo mimi, Nchemba ni mtu ambaye hafai uongozi wa aina yoyote katika jamii, lakini ajabu wengine wanaona kinyume chake! Mtu ninayemuo hafai wengine wakamchagua awe mbunge wao. Mtu huyohuyo akapata nyadhifa mbalimbali katika chama chake, chama tawala, huku mwenyekiti wa chama hicho kitaifa akimuona anafaa zaidi kiasi cha kumpandisha chati kwa kumteua awe Naibu Katibu Mkuu!
Hayo ndiyo mambo yanayoifanya Tanzania ionekane nchi ya ajabu, nchi ambayo mtu anaweza kufanya ovu lolote na bado akashangiliwa na walewale aliowafanyia uovu. Tanzania ya maajabu.
Huko tupaache, inawezekana anapafaa kulingana na halihalisi ilivyo kwa upande wao. Maana Waswahili wanasema kwamba kila shetani na mbuyu wake. Cha kuangalia ni vituko na majigambo ya kijana huyo kada wa CCM ndani ya jamii yetu.
Kijamii, Mwigulu anaonekana kutumia nafasi aliyo nayo kuigawa jamii yetu katika makundi hasimu kwa kisingizio cha itikadi za kisiasa na kisha kuchochea uhasama kati ya kundi moja na lingine kusudi makundi hayo yachukiane. Jambo hilo analifanya bila kujali kwamba anahatarisha mustakabali wa nchi yetu ambayo yeye ni kiongozi.

Kauli na matendo yake ambavyo amekwishavionesha, kuanzia Bungeni mpaka kwenye mikutano ya hadhara, hususan  kwenye kampeni mbalimbali za kuwashawishi wananchi wakichague chama chake dhidi ya vyama vya upinzani, ni ushahidi tosha wa haya ninayoyasema hapa.
Mfano, Nchemba katengeneza kitu anachokiita ugaidi na kukivisha kwa wengine hasa anaowachukulia kama mahasimu wake kimaslahi. Katika mojawapowapo ya vituko vyake, kaapa kuanzia Bungeni kuwa anao ushahidi wa duniani na mbinguni juu ya ugaidi wa kada wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Wilfred Muganyizi Lwakatare. Lakini mpaka Lwakatare anafutiwa mashitaka hayo ya kuchonga ya ugaidi na Mahakama Kuu hatukuuona wala kuusikia ushahidi  wa Mwigulu.Wengine tukajiridhisha kuwa pengine ushahidi huo umekwamia kwenye masjala ya mbinguni alikokusema.Sasa kilichobaki kikijionesha wazi ni vita kati ya mahakama na uzushi wa Nchemba. Mahakama inaonekana kuukomalia uzushi wa Nchemba, ambapo tunajionea jinsi mahakama inavyoyatupilia mbali kila madai ya ugaidi yanayopelekwa kwake ikidaiwa kuna ushahidi uliohifadhiwa mbinguni ila mahakama inapouhitaji hauletwi.
Vihoja vingine vya Nchemba ni kama vile vya kuvaa bendera ya taifa shingoni karibu kila wakati, au kuvaa mavazi yaliyo katika mfumo wa mavazi ya kijeshi. Haieleweki kama hiyo ndiyo inayomaanisha au kuonyesha uzalendo uliotukuka. Kwamba yeye ni mzalendo kuliko wengine wote kwa kuvaa bendera ya taifa shingoni. Au kwamba yeye ni mtu anayefanya mambo kijeshi kwa kuvaa mavazi yaliyo katika mfumo wa mavazi ya makamanda wa jeshi.
Hivi hayo ndiyo mafanikio ya Nchemba anayodai yanamfanya atajwetajwe sana na kutamba kuwa kamwe hakuna atakayetokea na kuyasimamisha? Mafanikio yaliyopatikana katika umri mdogo!
Ningetaka kumkumbusha Nchemba kwa kutumia tu uzoefu wa maisha. Kama kusemwasemwa sana katika umri mdogo ndicho kinachomfanya mtu ang’are basi Samwel Doe wa Liberia aliyeupata urais katika umri wa miaka 25 angeng’ara zaidi ya Nelson Mandela aliyeupata urais katika umri wa miaka 76. Lakini je, ndivyo halihalisi ilivyo? Kuna uwezekano wowote wa kumlinganisha Samwel Doe na Mandela katika mafanikio ya kisiasa?
Sasa kwa kulizingatia hilo inawezekanaje Nchemba ajilinganishe kwa Dk. Slaa kisa kaanza kusemwasemwa katika siasa kwa umri mdogo wakati Slaa kaingia kwenye siasa ukubwani? Hapo najaribu kutegua kitendawili cha Nchemba kwamba katika umri wa miaka 34 anasemwa hivi, je, katika umri kama alio nao Slaa itakuwaje.
Naweza kubashiri kwamba si ajabu katika kufikia umri kama alio nao Dk. Slaa,  Nchemba akawa hajulikani tena kwenye siasa za nchi yetu kutokana na usemi wa kwamba ivumayo haidumu. Maana maisha yana kanuni zake ambazo si rahisi kuzibadilisha, ndiyo maana wahenga wakapata semi mbalimbali za uhakika zinazotabiri maisha kulingana na matukio yaliyopo.
Wahenga walikuwa na hekima nyingi, walisema chema chajiuza kibaya chajitembeza. Ni kweli kabisa. Ni nadra sana chema kusemwa mara kwa mara. Ila kiovu husemwa sana mara kwa mara. Nahisi kusemwa sana kwa kilicho kiovu ni katika kukumbushana namna ya kukiepuka. Chema hakina tatizo lolote.
Shetani ni muovu, swali la kujiuliza ni yupi kati yake na malaika aliye mwema anayetajwa zaidi? Kwa walio waamini kwa uwepo wa Mungu watakuwa wanaelewa kwamba ibada inaweza kuendeshwa mpaka ikaisha bila kutaja neno malaika, lakini ibada haiwezi kuendeshwa mpaka kumalizika bila kumtaja shetani. Hivi kweli shetani anaweza kuvimba kichwa na kumtambia malaika kutokana na kutajwa kwake sana hata ndani ya nyumba za ibada?
Tumeshuhudia kauli mbalimbali za hatari zinazotolewa na kada huyo wa CCM akiwa hajari zinaweza zikaiathiri kiasi gani jamii yetu. Tukiacha zile za kuwabambikia wenzake sifa mbaya ya ugaidi, tumesikia kama zile za kwamba mkiwachagua Chadema mtakufa. Kauli hiyo imetolewa katika kampeni za udiwani, Arusha. Na kweli muda mfupi baada ya kauli hiyo kukatokea vifo katika mkutano wa Chadema. Na mpaka sasa mtu huyo hajachukuliwa hatua yoyote, walau kuulizwa tu kwamba kauli yake hiyo ilikuwa na maana gani.
Zipo kauli nyingi za hatari zilizotolewa na Nchemba huku wakubwa wake wakimuangalia tu na kufurahia wakidhani anawakomoa wapinzani, hivyo wakamuachia tu bila kumkemea. Lakini inabidi ieleweke kuwa mtoto mtukutu anayechezea moto ndani ya chumba kilichohifadhi petroli ni wa kukanya kwa ukali bila kuangalia kama anacheza na ndugu wa kambo, maana lolote la kutokea linaweza kuwaangamiza watoto wote pasipo kujali ni nani asiyekuwa mtoto wa kambo.
Mtu wa aina hiyo atatoweka vipi vinywani mwa watu? Na anaposemwa ni kweli anasemwa kutokana na mafanikio yake aliyoyapata katika umri wake mdogo? Kama kweli hayo ni mafanikio yanayopaswa kutambiwa basi shetani ana kila sababu ya kumtambia malaika maana anasemwa sana zaidi yake.
0784 989 51
Next Post Previous Post
Bukobawadau