Bukobawadau

TABORA;MAKADA WA CHADEMA WAFUTIWA SHTAKA LA UGAIDI

Na Thomas Murugwa, Tabora
KWA mara nyingine Mahakama Kuu, imetupilia mbali mashtaka ya ugaidi yaliyofunguliwa dhidi ya viongozi na wananchama wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA).
Jana, Mahakama Kuu Kanda ya Tabora iliwafutia shtaka la ugaidi wanachama watano wa CHADEMA ikisema kosa lao ni la jinai na halipaswi kuitwa la ugaidi.
Katika uamuzi wake, Jaji Mfawidhi wa Mahakama hiyo, Simon Lukelelwa, aliwaonya waendesha mashtaka kuacha tabia ya kutumia maneno makali ya ugaidi katika kesi za jinai, hatua aliyosema inaogofya wageni wanaotarajia kuja Tanzania.
“Suala hili la ugaidi kwa siku za hivi karibuni limeshika kasi, linazungumzwa kwa mapana ndani na nje ya nchi, lakini inavyoonyesha mazungumzo hayo hayajaeleweka undani wa madhara yake. Nchi ikiwa imekithiri kwa ugaidi kama inavyodaiwa vitu vingi vingeathirika, uchumi, utalii na mambo mengine.
“Ni vizuri mambo haya yakapewa nafasi yake na kwa umakini mkubwa, yasije yakaleta madhara kwa nchi pasipo ulazima wowote. Hata neno ugaidi tafsiri yake haijajulikana vizuri, kila mtu anatafsiri zake. Mtu unayemuona ni gaidi, anaweza kuwa mpigania uhuru kwa mwingine,” alisema Jaji Lukelelwa.
Hii ni mara ya pili kwa Mahakama Kuu kufuta mashtaka kama hayo kwa viongozi wa CHADEMA ambapo Mei 8, mwaka huu, Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam ilimfutia mashtaka matatu ya ugaidi Mkurugenzi wa Ulinzi na Usalama wa chama hicho, Wilfred Lwakatare.
Jaji Lawrance Kaduri alitoa uamuzi huo akisema ulitokana na kukubaliana na hoja ya mawakili wa Lwakatare, Tundu Lissu, Peter Kibatara na Mabere Marando.
Makada hao wa CHADEMA waliofutiwa shtaka hilo la ugaidi jana mkoani Tabora ni Henry John Kilewo, ambaye ni Katibu wa CHADEMA Wilaya ya Kinondoni, Evodius Justinian, Oscar Kaijage, Rajabu Daniel na Seif Magesa Kabuta.
Vijana hao walipandishwa kizimbani katika mahakama ya wilaya ya Igunga na kusomewa mashtaka mawili, moja la ugaidi na lingine la jinai.
Baada ya kusomewa mashtaka hayo, mawakili wao, Peter Kibatala na Profesa Abdallah Safari walipambana kuwanusuru na mashtaka hayo.
Mawakili hao walihoji uhalali wa mashtaka hayo, wakidai kuwa hakuna vigezo vya kutosha kuonyesha kuwa kuna ugaidi, huku pia wakihoji utaratibu wa kuwafungulia mashtaka katika mahakama hiyo badala ya kule walikokamatiwa.
Hivyo, waliiomba Mahakama Kuu ama iwafutie mashtaka hayo au iamuru kila mshtakiwa arudishwe na kushtakiwa katika mahakama za mahali walikokamatiwa.
Katika uamuzi wake, Jaji Lukelelwa aliongeza kuwa sheria za makosa ya jinai zipo wazi na zinaelekeza na kufafanua makosa na mashtaka yanayoweza kufunguliwa kwa wananchi wanaokwenda kinyume cha sheria zilizotungwa.
Jaji aliamru watuhumiwa hao warejeshwe wilaya ya Igunga walikotenda makaosa yao na wafunguliwe shtaka la kufanya matendo ya kusababisha madhara makubwa mwilini kwa kuzingatia sheria ya mwenendo wa makosa ya jinai.
Aliongeza kuwa hakimu atakayesikiliza shauri hilo awape dhamana kwa kutoa masharti atakayoona yeye yanalingana na shtaka linalowakabili watuhumiwa.
Wakili wa washtakiwa hao, Peter Kibatala, akizungumza na waandishi wa habari nje ya mahakama na kumshukuru jaji kwa kupitia marejeo yao waliyoomba na kuyatolea maamuzi.
Awali wananchama hao watao wa CHADEMA kutoka mikoa mbalimbali hapa nchini walikuwa wanatuhumiwa kwa makosa mawili likiwemo la ugaidi kwamba walimteka na kummwagia tindikali raia mkazi wa mjini Igunga.
Katika shtaka la kwanza walishtakiwa chini ya Sheria ya Kuzuia Ugaidi, wakidaiwa kumteka kwa nia ya ugaidi Mussa Tesha huko Igunga, Tabora na la pili wanashtakiwa chini ya Sheria ya Kanuni za Adhabu wakidaiwa kumdhuru Tesha kwa kummwagia tindikali.
Walidaiwa kutenda makosa hayo mwaka 2011, wakati wa kampeni za uchaguzi mdogo wa Jimbo la Igunga.
Upande wa mashtaka uliongozwa na wakili wa serikali, Juma Masanja, akisaidiana na wakili mwingine wa serikali, Idelfonce Mukandara, waliodai mashtaka hayo ni halali.
Next Post Previous Post
Bukobawadau