Bukobawadau

Tukiamua kujirudi tunaifuta laana ya UKIMWI

NA PRUDENCE KARUGENDO

Ukimwi ni ugonjwa ambao umetoa changamoto kubwa katika sayansi ya tiba. Pamoja na wanasayansi kukosa usingizi wakitafuta namna ya kupata tiba ya ugonjwa huo tangu ulipogunduliwa kwa mara ya kwanza mwanzoni mwa miaka ya 1980, mpaka sasa bado hawajafanikiwa kupata tiba wala chanjo yake.

Tofauti na magonjwa mengine yanayotishia maisha ya wanadamu kwa kiwango sawa na ugonjwa huo ulivyo, ukimwi ni ugonjwa ambao si mwepesi kusambaa kwa njia ya kuambukizana. Kuambukizwa kwakwe ni kugumu kuliko magonjwa mengine. Hauambukizwi kwa hewa wala kugusana tu, jambo hilo linashawishi dhana ya kwamba watu wanaoambukizwa ukimwi baadhi yao ni kama wanakuwa wamekusudia kuambukizwa. Pamoja na kuonekana hivyo takwimu zinatuonyesha kuwa wapo wasioambukizwa katika mazingira yenye kila dalili za hatari ya uambukizaji wa ugonjwa huo. Mfano watu wanaofanya biashara ya kuuza ngono, malaya, machangudoa na mashoga, lakini siyo wote wanaopimwa wakakutwa wameathirika. Vilevile hata wanandoa, wapo wanaotokea mmoja akawa ameathirika lakini mwenzake akawa hajaathirika.

Kwa vile tunaona kuwa kuambukizwa kwa ukimwi ni kugumu, hivyo ni rahisi kuamini kuwa ni vyepesi kuuepuka ugonjwa huo. Lakini hatahivyo jambo la kushangaza ni kwamba bado inaonekana kuepukika kwake kunaonyesha ni kugumu vilevile! Hii ndiyo wakati mwingine inaleta ushawishi wa kuwa na imani kwamba ugonjwa huu pengine ni wa laana. Lakini hata hivyo laana yenyewe itakuwa ni ya kujitakia. Nitaeleza kwa nini.

Tunapaswa tujiulize, kwa nini mpaka sasa ugonjwa huo unashindikana kuepukika? Mathalan, ulijitokeza ugonjwa wa Bonde la Ufa siku si nyingi zilizopita ambao uambukizwaji wake ni mwepesi kuliko wa ukimwi, tuliona tahadhari zilizochukuliwa na watu wakafanikiwa kujiepusha nao. Kwa nini ukimwi unashindikana?

Kinachoonekana ni kwamba pamoja na kuelewa madhara uliyo nayo ugonjwa huo bado jamii haijakubali kuuwekea tahadhari inayolingana na ukubwa wa madhara yake. Bado ugonjwa huo unajinufaisha na namna jamii inavyoushughulikia. Kimojawapo kinachounufaisha ugonjwa huo ni aibu ambayo jamii imeamua kuufunika nayo. Ugonjwa huo unachukuliwa ni wa aibu, ambayo inapewa nafasi kubwa kuliko tahadhari ya kuyalinda maisha (uhai) dhidi ya ugonja wenyewe. Inaonekana ni heri kumlinda mtu na aibu iletwayo na ugonjwa huo kuliko tahadhari ya kuunusuru uhai wake. Ni bora kumlinda mtu anayeugua ukimwi kwa kutaja sababu nyingine za uongo za kuugua kwake ili kumuepusha na kinachodaiwa ni aibu pamoja na kumlindia heshima hata kama inaeleweka kwamba njia hiyo haitayanusuru maisha yake. Hapa hakuna lolote la maana zaidi ya kuunufaisha ukimwi kwa kuujengea mazingira ya kuendelea kujitawala huku ukiwamaliza watu.

Tuchukulie mfano, simba akiingia katika kijiji akaanza kushambulia na kuua watu, hilo ni jambo la hatari, haitakuwa aibu kumtaja mtu aliyeshambuliwa au kuuawa na simba. Ni lazima tahadhari zitachukuliwa za kujilinda na simba huyo sanjari na mikakati ya kumuwinda na kumuua. Ila kikwazo kinaweza kikajitokeza iwapo itaonekana ni aibu kuyataja madhara yaliyosababishwa na simba mhusika. Hiyo itakuwa ni faida kwa simba kwa maana ya kuendelea kuwakamata watu na kuwala kimyakimya. Swali ni je, aibu ya aina hiyo inafaa panapokuwepo na hatari ya aina hiyo?

Aibu ya kuwataja watu walioathirika au kufa kwa ukimwi linaweza likawa tatizo linalozorotesha mapambano dhidi ya ukimwi. Aibu ni tatizo linaloulinda ugonjwa wa ukimwi. Hii ni kwa sababu ukiwaondoa marais wastaafu, Mandela wa Afrika Kusini na Kaunda wa Zambia, waliotaja hadharani kuwa watoto wao wamekufa kwa ukimwi, imekuwa si kawaida kwa watu maarufu kujihusisha na athari za ukimwi. Watu wenye majina makubwa katika jamii wamekuwa wakiugua na kufa kwa dalili zote za ukimwi lakini jamii ikilazimishwa kuamini kuwa wamekufa kwa magonjwa mengine tofauti. Je, hiyo inamsaidia nani?

Wakati fulani nilifiwa na jamaa yangu kutokana na ugonjwa wa ukimwi, nilipokuwa naulizwa kafa kwa ugonjwa gani nasema ni ukimwi. Niligeuka kituko, watu wakawa wananiuliza mara mbilimbili bila kuamini masikio yao. Watu walikuwa wananishangaa kuliko wanavyoushangaa ukimwi wenyewe. Nilipewa ushauri niwe nataja magonjwa mengine kama kansa, shinikizo la damu nakadhalika, au kusema sijui ikibidi ili kulinda heshima ya marehemu ambaye hatukuweza kuulinda uhai wake.

Kinachoufanya ugonjwa huu wa ukimwi uonekane ni wa aibu ni kitu gani? Kwa nini magonjwa mengine hatarishi, kama shinikizo la damu, saratani nakadhalika, hayaonewi aibu wakati madhara yake ni yaleyale, kifo, kama ulivyo ukimwi? Kitu cha ajabu hata ugonjwa ambao chanzo chake ni uchafu wa kupindukia, kipindupindu, nao unaonekana wa maana mbele ya ukimwi! Hauonewi aibu kama inayojitokeza kwa ukimwi.

Hii inaleta picha ya kwamba pamoja na hatari inayoonyeshwa na ukimwi ni kama bado watu wanauendekeza ugonjwa huo ili usitoweke, kitu ambacho nashawishika kuamini kuwa ndicho kinachochochea aibu inayo ambatana na ugonjwa huo. Aibu ya kuonekana watu wanajihifadhia hatari dhidi ya uhai wao.

Aibu hii imegeuka kichaka kikubwa kinachooneka kulindwa hata kwa nguvu za serikali wakati mwingine kama zinavyolindwa hifadhi za taifa. Hapo ndipo inabidi tujiulize kama kweli jitihada zinazodaiwa kufanywa na serikali kupambana na ugonjwa huo zina dhamira ya kweli? Unawezaje kupambana na adui kwa lengo la kumuangamiza halafu uwe na aibu ya kuuangalia uchi wake?

Serikali inabidi iwe ya kwanza kukifyeka kichaka hiki cha aibu. Tuelezwe ni wakubwa gani wameathirika au kufa kwa ukimwi. Hawa wana uwezo, kuusambaza ukimwi kwao ni jambo rahisi kuliko wanyonge wanavyoweza. Wanyonge wakishaona mfano kutoka juu bilashaka nao wataifuata njia hiyo, tutakuwa tumekifyeka kichaka cha aibu kinachouhifadhi ukimwi. Lengo liwe ni kuunyima ukimwi mahali pa kujihifadhi.

Sisemi kwamba watu walioathirika wajulikane ili watengwe na kuwanyanyapaa, hapana, ila ni muhimu wakajulikana kusudi iwe rahisi kupaelewa walikopitia ili paweze kuepukika kama njia ya kupunguza maambukizi. Sababu kuifanya siri haisaidii lolote, sanasana kuchangia maambukizi mapya.

Namna nyingine ya kuhakikisha tunaunyima ukimwi mahali pa kujihifadhi ni kuhakikisha tunayasafisha maadili yetu kimwili na kiroho maana hili nalo ni jambo ambalo kidogo bado linatuwia gumu. Zipo njia zinazotutaka kuulinda usafi wa maadili yetu kimwili. Iwapo njia hizi zingefuatwa kikamilifu ukimwi ungekuwa hauna mahali pa kujishikiza. Kuiheshimu miili yetu na kuithamini kiasi cha kutoitoa kihorera, mtu kuwa na mwenzi moja wa kushiriki naye tendo la ngono, ambaye tena amehakikishiana naye usalama wa afya, au kutumia kondomu wakati wa kujamiiana.

Hayo ni maadili ya kuitunza miili yetu ambayo wanadamu tumejaliwa nayo kutokana na akili tulizonazo zituwezeshazo, wakati mwingine, kuitumia miili yetu kujistarehesha tofauti na wanyama wengine waitumiayo miili yao kukamilisha tu aina ya maumbile yao. Hawaitumii kufanya starehe, hivyo hawachagui wa kustarehe naye. Wanadamu tuko tofauti, tuna maadili, tunapaswa kuyatunza ili yatulinde. Hiyo ndiyo njia ya kuyalinda maadili yetu kimwili.

Njia nyingine ni ya kuyalinda maadili yetu kiroho. Njia hiyo japo kidogo inakinzana na ile ya kimwili, ikizingatiwa pia inaweza kutuepusha na ukimwi. Kanuni za njia ya njia ya kujilinda kiroho zimeambatana na amri zinazotuzuia kufanya baadhi ya mambo kama njia ya kujitakasa kiroho. Kuzini na kutamani hovyo ni kati ya mambo yanayozuiwa katika amri hizo. Watu wakikubali kuzitii amri hizo kwa kiasi kikubwa watakuwa wamejiepusha na ukimwi unaopitia katika tendo la ngono wakati wa kuzini. Hata kama mmoja wa wanandoa anamuambukiza mwenzake ni lazima ieleweke kuwa aliyeuleta atakuwa ameupata katika uzinzi.

Tatizo linajitokeza pale vyombo vya kuyasimamia maadili ya kiroho vinapoonekana kushindwa kumsaidia aliyekengeuka kiroho na kumtelekeza ili akengeuke kimwili pia. Kuzuia matumizi ya kondomu ni jia ya kuwatelekeza waliopotoka kiroho. Hapa vyombo vya imani vinaonekana kuutaka msaada wa ukimwi kuwaadhibu wakosefu, hii ni hatari.

Vyombo tulivyo navyo vinavyosimamia miongozo ya kiroho, kwa kuvitaja viwili tu vilivyoenea sana huku kwetu, makanisa na misikiti, kwa kusaidiana na wadau wengine wa kuulinda uhai, vinayo nafasi kubwa ya kuutokomeza ukimwi kama vingezitumia vyema nafasi zake.

Mfano kuuwekea mkazo mfumo wa uadilifu unaoongoza mwenendo wa imani ndani ya Uislamu na Ukristo, vilevile vikiwaangalia wanao tetereka na kuwashauri au kuwaruhusu wajilinde kimwili wakishindwa kujilinda kiroho.

Kanisa kwa mfano, linapaswa kuhakikisha yale yote yanayohubiriwa kanisani yanazingatiwa kikweli na waamini wake. Liwe na mamlaka kamili ya kulitekeleza hilo kwa waamini wake. Siyo wahubiri wanatoka kwenye madhabahu na kupitia mlango wa nyuma kwenda kujiunga na wengine kuyasigina mahubiri yao. Hili linachangiwa na ukweli kwamba tunawaona baadhi ya wahubiri wakiwa wameathirika na ukimwi wakiwa wamebaki kutegemea tu huruma ya kuonewa aibu ya kutoyataja matatizo yanayokuwa yanawasibu, kitu ambacho hakisaidii lolote.

Tumeona kuwa maambukizi ya ukimwi kwa kiasi kikubwa yanatokana na ngono horera. Kwahiyo ili kuepukana na ngono horera asasi zote zinazojihusisha na vita dhidi ya ukimwi zinasisitiza watu wote walio katika rika la kufanya ngono kuingia katika ndoa na kuwa waaminifu na waadilifu katika ndoa zao. Na kwa upande wa imani hizi mbili, Ukristo na Uislamu, ndoa ni jambo linalopewa umuhimu wa pekee.

Umuhimu huo unatiliwa mkazo zaidi na kanisa kiasi cha kufikia kudai kwamba waliooana katika imani ya Kikristo wanakuwa wameunganishwa na Mungu. Na alichokiunganisha Mungu mwanadamu hapaswi kutenganisha. Kanisa lingesimamia maelezo yake hayo kwa dhati kuhusu ndoa lingekuwa limechangia kwa kiasi kikubwa kupatikana kwa tiba ya ukimwi. Tendo la kujamiana haliepukiki, na ndoa ni njia ya kuepusha kujamiiana kihorera. Kila moja anakuwa na mwenziwe. Hiyo inaondoa kuambukizana virusi viletavyo ukimwi. Jamii isiyo na maambukizi mapya ya ukimwi tayari inakuwa imepata tiba ya ukimwi.

Lakini sasa kanisa ni kama linayumba. Wanadamu wameanza kutenganisha vilivyounganishwa na Mungu. Ndoa zinavunjika hovyo hasa kutokana na msukumo wa tamaa za kimwili huku kanisa likiangalia bila kuchukua hatua muafaka za kukabiliana na wimbi hilo hatarishi. Kanisa halichukui hatua za kumuadhibu aliyesababisha ndoa kuvunjika wala kumlinda aliyevunjiwa ndoa. Msimamo wa kanisa unabaki kwamba madamu watu hao waliapa kutenganishwa na kifo, kanisa linaendelea kuitambua ndoa husika mpaka mmoja wao anapokuwa amekufa. Kwa maana hiyo wote wawili wanalazimika kufanya ngono horera huku kanisa likiwa limewaziba na msimamo wake mwingine wa kwamba matumizi ya kondomu ni haramu. Ndoa za Kikristo zinavunjika, wanandoa wanasambaratika kanisa likiwa limewawekea pingamizi la kutooa wala kuolewa tena, na wala halitaki kusikia wakitumia kondomu. Linakuwa limewatoa kafara kwa ukimwi.

Kanisa linakuwa limesimamia kusambaa na kuenea kwa ukimwi linapowazuia waamini wake kuoa au kuolewa tena baada ya ndoa zao kuvunjika. Kanisa linao uwezo wa kuepusha janga hili kwa waamini wake kwa kuzifanyia marekebisho kidogo baadhi ya taratibu zake, ila pengine halijaona umuhimu wa kufanya hivyo. Linaona bora watu waangamie kuliko lenyewe kuachana na uhafidhina.

Hayo yote yanaweza kunifanya niamini kuwa kweli ukimwi ni laana ila ya kujitakia, tukijirudi laana hii inaweza kuisha tukaendelea kuishi bila ukimwi.

prudencekarugendo@yahoo.com

0784 989 512
Next Post Previous Post
Bukobawadau