Bukobawadau

Watanzania wanateseka na Dawa za kulevya Afrika Kusini

Balozi wa Tanzania nchini Afrika ya kusini Radhia Msuya ofisini kwake Pretoria nchini Afrika Kusini.
By Albano Midelo

Idadi ya vijana wanaoingia nchini Afrika Kusini kutokea Tanzania kinyume cha sheria kwa malengo ya kutafuta maisha bora imesababisha wengi wao kujiingiza katika biashara ya dawa za kulevya baada ya kukosa kazi.
Uchunguzi uliofanywa na FikraPevu katika mitaa ya jiji la Johannesburg pekee umebaini kuwepo idadi kubwa ya vijana wa kitanzania ambao wamekuwa wanazurura na wanauza na kutumia dawa za kulevya na kujihusisha na kazi za ujambazi wa kutumia silaha kwa lengo la kujipatia kipato.
Balozi wa Tanzania nchini Afrika Kusini, Radhia Msuya amekiri kuwepo kwa vijana wengi wa kitanzania ambao wanaingia kinyume cha sheria na kwamba ofisi yake inaingia gharama kubwa ambapo kila mwezi vijana wazururaji zaidi ya 200 walioingia kinyume cha sheria wanarudishwa Tanzania.
Alibainisha kuwa vijana wengi wanaamini kuwa nchini Afrika Kusini ni kama peponi kwa kuwa kuna maisha bora hivyo wengi wanakimbilia kuja kutafuta maisha kwa kutumia njia ambazo sio halali ikiwemo kufika bila hati za kusafiria.
“Ni kweli nchini Afrika Kusini kuna maisha bora, lakini maisha hayo hayapatikani hivi hivi tu, kwa kudhani ukifika hapa unachuma pesa kutoka kwenye miti, watu hapa wanachapa kazi kwa bidii”, alisisitiza.
Alisema kutokana na vijana hao kukosa kazi za maana ambazo hazikidhi kipato, baadhi ya vijana wamejiigiza katika biashara haramu ya matumizi ya dawa za kulevya hali ambayo imesababisha wengine kuwa wakabaji.
Peter Masika ambaye ni Mkurugenzi wa kampuni ya utalii ya Monsoon Transfers and Tours ni mtanzania ambaye ameishi nchini Afrika Kusini kwa takribani miaka 15, anasema anapokuwa anazunguka katika baadhi ya mitaa Johannesburg na Pretoria amekuwa anakutana na watanzania wengi ambao wamegeuka ombamba kwa kukosa kazi ya maana.
”Wengi wananifahamu hivyo wakiona gari langu wamekuwa wanalizunguka na kuomba fedha kwa kuwa nimekuwa nawasaidia lakini wengi hivi sasa ni wahalifu, wanauza na kutumia dawa za kulevya na kujiingiza katika vitendo vya uhalifu”, alisisitiza.
Maxmillian Bushoke ni mtangazaji wa idhaa ya Kiswahili ya Channel Afrika ambaye yupo nchini Afrika Kusini tangu mwaka 1994 amekiri kuwa jamii ya watu wanaofanya biashara ya dawa za kulevya imezuka na kuwashirikisha vijana wengi wanaotoka Tanzania na Nigeria.
Kulingana na Bushoke ambaye pia ni mwanamuziki maarufu wa zamani nchini Tanzania alidai kuwa hata baadhi ya wamamuziki ambao wanaingia nchini Afrika Kusini, wanajitumbukiza katika biashara ya unga baada ya kukutana na vijana wenzao wanaotumia madawa hayo hivyo kujiletea matatizo makubwa yanayosababisha kufungwa na hata kupoteza maisha.
“Nina mfano hai uliotokea hivi karibuni kwa mtoto wetu mwanamuziki wa kizazi kipya Mangwea ambaye alifika hapa Afrika Kusini na alifanya maonesho kadhaa ya muziki kisha aliamua kwenda kuwatembelea wenzake ambao ni watumiaji wakubwa wa madawa hayo ambapo naye aliamua kubwia na yakamsababishia kifo”, alidai Bushoke.
Hata hivyo Bushoke alidai kuwa vijana wa kitanzania wanaotumia madawa ya kulevya nchini Afrika Kusini, walianza kutumia madawa hayo tangu walipokuwa Tanzania isipokuwa katika nchi ya Afrika Kusini matumizi ya madawa hayo ni makubwa zaidi kuliko Tanzania.
Bushoke alisema utafiti walioufanya katika jiji la Johannesburg mwaka huu wamebaini vijana wanaoongoza kwa matumizi ya madawa ya kulevya ni wale wanaotoka katika nchi ya Nigeria wakifuatiwa na Tanzania ambao wanatumiwa na matajiri wakubwa katika biashara hiyo haramu.
Ripoti kutoka Afrika Kusini zilibainisha kuwa wanawake wawili walikamatwa katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa OR Tambo nchini Afrika Kusini wakitokea Tanzania, wakiwa na madawa ya kulevya yenye thamani ya Rand million 42.6 kiasi ambacho ni kikubwa zaidi kuwahi kukamatwa katika mpaka wowote wa nchi hiyo.
Kwa mujibu wa taarifa iliyoripotiwa na shirika la habari la Africa Kusini SABC, wanawake hao hivi karibuni waliwasili na ndege kutoka Tanzania, walikutwa na mabegi 6 makubwa yaliyojaa madawa (crystal meth) yenye thamani ya Rand 42.6 millioni ambayo ni sawa na zaidi ya billioni 6 ya Tanzania.
Takwimu kutoka Wizara ya Mambo ya Ndani za mwaka 2005 pekee, zinaonyesha kuwa kiasi cha dawa za kulevya kilichokamatwa kilikuwa ni kilo 150,000 za bangi, kilo 1206 za mirungi, kilo 10 za heroin, kilo 78 za bangi iliyosindikwa, gramu 362 za cocaine na kilo 1.4 za dawa ya hospitali aina ya morphine na kwamba ukamataji wa dawa hizo uliambatana na kukamatwa kwa watuhumiwa 4,532 ambapo jumla ya kesi 3,368 zilifunguliwa mahakamani. 
Kwa mujibu wa ripoti ya Mwaka 2006, vyombo vya dola vilikamata kilo 91. 5 za heroin, kilo 4.13 za cocaine, kilo 37 za morphine, kilo 11 za mirungi na kilo 225,229 za bangi.
Katika nchi ya China, sheria ipo wazi kuwa mtu anapokamatwa na dawa za kulevya anahukumiwa kifo ambapo takwimu kutoka nchini China zinaonyesha kuwa katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita inadaiwa watanzania 200 walinyongwa katika nchi hiyo baada ya kukutwa na hatia ya kujihusisha na dawa za kulevya.
Wataalamu wa afya wanasema matumizi ya madawa za kulevya yana madhara mengi kwa watumiaji kama vile uharibifu wa mfumo wa fahamu ambao husababisha mtu kupata mabadiliko ya kihisia, kimtizamo na kitabia. Mabadiliko hayo humsababishia mtumiaji tabia zisizokuwa za kawaida kwa mwanadamu na hata kupungukiwa uwezo wa kufikiri vizuri.
Kwa mujibu wa wataalamu mtumiaji wa muda mrefu wa dawa za kulevya husababisha magonjwa ya akili, ini, mapafu na wakati mwingine hata kifo. Wataalamu wanasisitiza kuwa ni rahisi  kwa watumiaji wa dawa za kulevya kuambukizwa UKIMWI kutokana na kushirikiana kujidunga sindano na  kufanya ngono zembe.
Credit;FikraPEVU.

Next Post Previous Post
Bukobawadau