Bukobawadau

KCU (1990) Ltd: Kahawa ya magendo tishio kwa uchumi

na Justin Tumaini

‘BALIMANYAILA’ ni msemo maarufu katika sehemu zinazolima zao la kahawa mkoani Kagera ukiwa na maana ya ‘Watajua baadaye tukishaondoka.’
Msemo huu hutumiwa na walanguzi wa kahawa wanaonunua kwa magendo na huwapunja wakulima kisha kuitoreshea nchi za jirani ambako huiuza.

Kahawa ni moja ya zao la biashara hapa nchini ambalo linakadiriwa kuliingiza taifa takriban dola za Marekani sh milioni 180.
Pamoja na mchango wake huu katika uchumi wa taifa, zao hili linakabiliwa na changamoto mbalimbali na hapa nazungumzia biashara ya kahawa za magendo hususan Kagera.


Katika ziara yake ya kiserikali hivi karibuni mkoani Kagera, Rais Jakaya Kikwete aliuagiza uongozi wa Mkoa wa Kagera kuunda kikosi kazi kwa ajili ya kutafuta suluhisho la kudumu la biashara ya kahawa za magendo zinazouzwa nchi jirani.

Rais Kikwete, anatoa agizo hilo baada ya kupokea malalamiko kutoka kwa viongozi wa wilaya za Muleba, Misenyi, Bukoba na Ngara waliomweleza kuwa biashara hiyo inakua kwa kasi kubwa huku ikitishia uchumi wa nchi.

Biashara ya magendo inavyofanyika

Kwa mujibu wa Meneja Mkuu wa KCU (1990) Ltd., Vedastus Ngaiza, wakulima wa kahawa Kagera wamekuwa wakidanganywa na walanguzi wa zao hilo ambao hutumwa na wafanyabiashara kutoka nchi jirani kununua kahawa na kuwauzia kwa siri.

Meneja huyo anasema tatizo la biashara ya kahawa za magendo ambayo hufanyika gizani ni kubwa na kuongeza kuwa karibu asilimia 40 ya kahawa huingia katika soko lisilokuwa rasmi.

Anasema wafanyabiashara wa nchi jirani huwatumia vijana wa Kitanzania ambao nao huwadanganya wakulima kuwa wanawalipa bei kubwa ukilinganisha na ile inayolipwa na KCU (1990) Ltd., jambo ambalo si kweli.

Ngaiza anasema baadhi ya nchi jirani ambazo kahawa yetu hutoroshewa hazina mamlaka zinazosimamia masuala ya kahawa, hivyo soko ni huria kabisa.

“Baadhi ya nchi majirani ambazo kahawa za magendo hutoroshewa hazina mfumo wa aina yoyote kwenye masuala ya kahawa kama vyama vya ushirika, wizara na mrajisi.

“Wafanyabiashara wa kahawa wa nchi hizo wanachokifanya ni kwenda sehemu mbalimbali duniani zikiwamo nchi za Ulaya kwa ajili ya kutafuta masoko ya kahawa.

“Wanapopata oda hurudi nchini mwao kwa ajili ya kuanza kutafuta mzigo kama walivyopata oda,” anaeleza.

Anaendelea kueleza kuwa kwa vile nchi hizo hazina utaratibu kama vyama vya msingi kama ilivyo hapa nyumbani, wafanyabiashara hao hulazimika kupita kila sehemu ili kuweza kupata kiasi ambacho kitakidhi oda ambayo tayari wameshaipata.

“Hawa wanachokifanya, wanawatafuta vijana wa Kitanzania na kuwapa fedha kwa ajili ya kununulia kahawa.

“Vijana hawa hupita nyumba kwa nyumba kwa wakulima na kununua kahawa. Badala ya kutumia mizani, hutumia mabakuli pamoja na plastiki, jambo ambalo si tu ni kinyume cha utaratibu bali pia huwaibia wakulima kwa kuwapunja.

“Vijana hawa ambao ni mawakala wa wafanyabiashara hao, hutumia mbinu mbalimbali kuwadanganya wakulima ili wawauzie kahawa yao. Kwa mfano, kama KCU (1990) Ltd. wananunua kilo moja ya kahawa ya maganda kwa sh 1,000 wao watasema wananunua kwa sh 2,000,” anasema.

Anasema tofauti na KCU (1990) Ltd. ambao hutumia mizani wakati wa kununua kahawa, wao hutumia bakuli ambalo wao hudai ujazo wake ni kilo moja lakini kiuhalisia mabakuli hayo hubeba kilo mbili.

Meneja huyo anasema baada ya kukununua kwa mabakuli, walanguzi hao huenda kuwauzia kahawa hiyo kwa kilo wafanyabiashara wa nchi jirani waliowapa fedha za kukunulia kahawa kwa wakulima na hupata faida kubwa huku mkulima akibaki ameumia.
“Wakati hawa walanguzi wakiwadanganya wakulima kuwa wanaibiwa kwa kuuza kahawa zao kwenye vyama vya msingi, wakati mwingine baadhi yao baada ya kununua kutoka kwa wakulima hurudi na kuiuza kahawa hiyo kwenye vyama vya msingi kwa kupima kwenye mizani,” anaeleza.

Ngaiza anasema duniani kuna masoko makubwa mawili ya kahawa, la kwanza lipo London, Uingereza, ambalo ni soko kuu la kahawa aina ya Robusta na la pili lipo New York nchini Marekani, ambalo ni soko kuu la kahawa aina Arabica. “Masoko haya mawili ndiyo yanayotoa bei elekezi na hakuna mfanyabiashara yeyote anayeweza kulipa zaidi ya bei elekezi, “KCU kazi yake ni kutafuta soko la kahawa kwa wakulima ambao ni wanachama wake.

“Bei tunayotoa kwa wanachama wetu ni ile inayotokana na bei elekezi inayotolewa na masoko haya mawili makubwa ya kahawa duniani.

“Mfanyabiashara anayesema analipa zaidi ya bei ya soko ni muongo na ndio wanaowaibia wakulima kupitia kununua kwa mabakuli ambayo huwapunja wakulima huku wakiwadanganya kuwa wanawalipa zaidi.

“Kama watakuwa wanalipa zaidi ya bei ya soko, wao watakuwa wanakwenda kuuza wapi? Hiki ni kiinimacho ambacho watu wanapaswa kufahamu,” anafafanua.

Jitihada za kupambana na kahawa ya magendo

Kwa mujibu wa Festo Gatahya, ambaye ni Mkuu wa Kitengo cha Masoko wa KCU (1990) Ltd., anasema KCU imekuwa mstari wa mbele kushirikiana na serikali katika kupambana na biashara hiyo inayokua kwa kasi huku ikiugharimu uchumi wa nchi.
“Mwaka jana kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi tulichangia sh 500,000 kuimarisha mapambano dhidi ya kahawa za magendo ambazo nyingi hutoroshewa nchi jirani na kuinyima nchi yetu mapato,” anasema.

Anasema pamoja na jitihada wanazofanya kuwaelimisha wakulima, juu ya kuuza kahawa yao kwa vyama vya msingi ambavyo vimethitishwa kisheria kama wakala wa manunuzi ya kahawa, bado wakulima wengi wamekuwa wagumu kuelewa huku wakiamini kuwa walanguzi ndio wanaotoa bei nzuri.

“Tunawatumia wawakilishi wa wakulima ambao huja kama wajumbe wa mikutano mikuu ya KCU kwa ajili ya kuwafikishia wakulima wote wanachama ujumbe juu ya umuhimu wa kuuza kahawa yao kwa wakala waliothibitishwa na sekirali.

“ Hata hivyo, wengi wamekuwa wagumu kuelewa huku wakisema wana uhuru wa kuuza kahawa yao wanapotaka,” anasema.

Meneja wa Wakala wa Vipimo Tanzania (WMA) Mkoa wa Kagera, Salvatory Mutashobya, anakiri kuwamo kwa wafanyabiashara ambao hununua kahawa bila kutumia mizani na kuongeza kuwa zoezi la kuwakamata watu hao limekuwa gumu kutokana na usiri mkubwa katika biashara hiyo.

“Hawa wanaununua kwa magendo na wanaouza ni watu wenye tabia zinazofanana. Wote wanafahamu wanafanya biashara isiyo halali, kwa hiyo mara nyingi hufanyiwa gizani na kwa usiri mkubwa na huwa vigumu kuwabaini,” anasema.

Hata hivyo anawaasa wakulima wa kahawa Kagera kuepuka kuuza kahawa yao kwa wanunuzi wasiothibitishwa na serikali kwa kuwa watakuwa wamejiweka kwenye mtego wa kuibiwa.
Next Post Previous Post
Bukobawadau