Bukobawadau

KIINI CHA VURUGU BUNGENU CHABAINIKA

Dodoma. Maoni ya Kamati ya Bunge ya Katiba, Sheria na Utawala kuhusu Muswada wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba wa 2013 yanadaiwa kuwa yalibadilishwa dakika za mwisho na kwamba suala hilo ndicho kiini cha vurugu zilizotokea bungeni mjini Dodoma juzi.

Gazeti hili limefanikiwa kuona nakala inayodaiwa kuwa ni maoni ya awali ya kamati hiyo ambayo yalikuwa na mapendekezo yanayotaka kuwapo kwa marekebisho kadhaa kwenye muswada huo, tofauti na yale yaliyowasilishwa bungeni juzi na Mwenyekiti wa Kamati, Pindi Chana.

Jumatano na Alhamisi wiki hii kulikuwa na mvutano mkubwa bungeni kiasi cha wabunge wa upinzani kutoka vyama vitatu vya NCCR -Mageuzi, Chadema na CUF kuungana na kususia mjadala kuhusu muswada huo.

Imedokezwa kuwa mvutano mkali kuhusu muswada huo ulianza ndani ya kamati hiyo wakati wajumbe wake ambao ni wabunge wa CCM walipotumia wingi wao kubadili maoni ya awali na kuweka maoni mapya, hatua ambayo inadaiwa kuwa ilikuwa na msukumo wa Serikali nyuma yake.

Ndani ya Kamati ya Bunge ya Katiba, Sheria na Utawala, wabunge wa upinzani ambao kwa idadi yao ni wachache walishindwa kuzuia mabadiliko hayo ya “lala salama” yanayodaiwa kuwa yaliwekwa Septemba 2, mwaka huu, hivyo waliazimia kuhamasisha wabunge wote wa upinzani kupinga marekebisho hayo kutokana na sababu kuu mbili.

Sababu hizo ni kutofanyika kwa mikutano ya wazi kwa umma (public hearing) upande wa Zanzibar na hatua ya kuwapo kwa mapendekezo ya Rais kurundikiwa madaraka makubwa ya uteuzi wa wabunge kutoka asasi za kijamii watakaoingia katika Bunge la Katiba.

Habari zinasema wakati fulani Naibu Spika wa Bunge, Job Ndugai alitembelea kamati hiyo wakati ikiedelea na vikao vyake na kukuta mvutano mkali kuhusu suala la marekebisho ya sheria ya sheria hiyo na alishauri kwamba pale ambapo hawataweza kuelewana basi wasubiri uamuzi ndani ya Bunge.

Jana gazeti hili lilimtafuta Chana kupitia simu yake ya mkononi na baada ya kumweleza kuhusu madai hayo alisema: “Tafadhali sana kwa sasa niko kwenye kikao, kwanza simu yako nimeipokea kwa heshima tu, tutafutane wakati mwingine”.

Waziri wa Katiba na Sheria, Mathias Chikawe alikiri kwamba kulikuwa na mapendekezo ya kuongeza idadi ya wabunge na namna ya kuwapata, lakini Serikali iliyakataa katika hatua ya majadiliano kabla ya suala hilo kufikishwa bungeni.

Tofauti ya maoni

Nakala ya taarifa ya awali ilipendekezwa kuwa katika kuteua wajumbe 166 wa Bunge la Katiba, Rais azingatie kikamilifu mtiririko wa mapendekezo ya kila kundi lililoainishwa katika kifungu cha (1) (c).

“Na endapo Rais hatazingatia mapendekezo ya kundi mojawapo, Rais afanye mrejesho kwa taarifa kwa kundi husika juu ya sababu za kutozingatia mtiririko wa mapendekezo yaliyowasilishwa kwake,” inasema taarifa hiyo.

Taarifa hiyo inaongeza kuwa kamati hiyo ilikuwa na maoni kwamba makundi mengine ya kijamii yaongezwe katika kifungu cha 22(1) (c) cha sheria mama, ili kupanua wigo wa uwakilishi mpana katika Bunge la Katiba, hivyo kuongeza idadi ya wabunge hao kutoka idadi ya awali 166 hadi kufikia 201.

“Kamati inashauri kuwa idadi ya wajumbe iwe 201 badala ya idadi ya wajumbe 166 iliyotajwa katika sheria mama, ili kupata idadi ya wajumbe watakaounda Bunge Maalumu la Katiba,” inasomeka taarifa hiyo.

Hata hivyo, maoni hayo yanatofautiana na yale yaliyowasilishwa bungeni juzi na jana, kwani yanaonyesha kwamba kulikuwa na majadiliano na mashauriano baina ya kamati na Serikali, hivyo ilikubaliana kuwa “Rais apewe mamlaka ya kufanya uteuzi wa wajumbe Bunge la Katiba” huku idadi ya wabunge wa kuteuliwa wakibaki 166.

Kifungu hicho kiliondoa haki ya kila taasisi kuteua jina la mjumbe wake katika Bunge hilo na badala yake, ikapendekezwa kuwa Rais atapelekewa matatu ili ateue moja kati ya hayo.

Hata hivyo, jana wakati Bunge lilipoketi kama kamati kwa ajili ya kupitia vifungu vya marekebisho ya muswada huo, Serikali iliwasilisha marekebisho ya nyongeza ambayo yanazitaka asasi za kiraia ziteue majina tisa na kati ya hayo Rais anaweza kuteua jina moja na kama asiporidhika anaweza kuteua mtu kutoka nje ya orodha hiyo.

Kuhusu suala hilo Chikawe alisema: “Tangu awali ilikuwa inaonyesha wajumbe ni 166. Ni kweli Kamati ilipendekeza wajumbe hao waongezeke hadi 201 lakini pendekezo hilo halikukubaliwa, ikabakia wajumbe watakuwa 166.”

Ushiriki wa Zanzibar

Itakumbukwa kuwa Kamati ya Katiba, Sheria na Utawala ilipewa wiki nne za kuendesha vikao vyake kabla ya kuanza kwa Mkutano wa 12 wa Bunge uliomalizika jana, tofauti na kamati nyingine ambazo zilipewa wiki mbili.

Baadhi ya wabunge (hasa wa upinzani) wanasema madhumuni ya kupewa muda huo ni kama hayakutimia kwani hawakuweza kupokea maoni kutoka kwa makundi muhimu hasa ya upande wa Zanzibar kama ilivyokusudiwa.

Hata hivyo, jana Makamu wa Pili wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ), Balozi Seif Ali Idd, alilihakikishia Bunge kuwa upande wa Zanzibar ulishirikishwa katika kutoa maoni ya muswada huo.

Hatua ya Balozi Idd kutoa ufafanuzi ilitokana na mwongozo ulioombwa na Mbunge wa Sikonge, Said Nkumba(CCM) aliyeomba kwa vile Balozi Seif yuko ndani ya Bunge basi apewe fursa kufafanua utata huo.

Kauli ya Balozi Idd inapingana na ile iliyotolewa juzi jioni na Mnadhimu wa Kambi ya Upinzani Bungeni, Tundu Lissu ambaye alisema ni kosa kubwa kamati kutochukua maoni ya Wazanzibar.

Lissu alisema kulikuwa na njama tangu mwanzo za kuhakikisha kuwa Kamati ya Bunge ya Katiba, Sheria na Utawala haichukui maoni ya Wazanzibari na hilo linathibitishwa na ratiba zilizokuwa zimeandaliwa na kamati.

“Katika orodha ya wadau wote 22 waliokuwa wameorodheshwa katika kutoa maoni yao juu ya muswada huu hakukuwa na Mzanzibari hata mmoja…tulipoipitia tukasema hapana Wazanzibari wako wapi,” alisema.

Lissu alisema yeye, Mwenyekiti wa Kamati, Chana na Makamu Mwenyekiti, William Ngeleja walikwenda kumwona Katibu wa Bunge, Dk Thomas Kashililah na kumweleza azma yao ya kwenda kuzungumza na wadau wa Zanzibar.

“Katibu akatwambia kwamba yeye ana fedha za kutuwezesha kukaa Zanzibar hata wiki moja, kwa hiyo tukarudi kwenye kamati tukatengeneza ratiba mpya na tukaongeza wadau sita wa Tanganyika na Wazanzibari wanane,” alisema Lissu.

Aliwataja wadau hao kuwa ni Chuo cha Taifa Zanzibar, Chuo Kikuu cha Zanzibar, Chama cha Mawakili Zanzibar, Chama cha Wanasheria Wanawake Zanzibar, Chama cha Walemavu Zanzibar na Profesa Abdul Shariff.

Wadau wengine walikuwa ni Shirikisho la Vyama visivyo vya Kiserikali Zanzibar (Angoza) na Jumuiya ya Misikiti Zanzibar na Jumuiya ya Maimamu Zanzibar, lakini hatukuwahi kukutana nao na kupokea maoni yao.

“Tukakubaliana kuwa tutakaa Zanzibar kwa siku tatu kuanzia Julai 14 hadi Julai 16 mpaka leo hatujawahi kuambiwa kwa nini tulizuiwa kwenda Zanzibar, lakini maneno yaliyokuwa yakisikika eti kwa sababu za kiusalama,” alisema.

Lissu alisema wakati kamati yao ikiambiwa haiwezi kwenda Zanzibar kwa sababu za kiusalama, wajumbe wa Kamati ya Ulinzi ya Bunge hilo ilikuwa Pemba ikiendelea na ziara zake.
Next Post Previous Post
Bukobawadau