Bukobawadau

Unyama dhidi ya Mzee Kibogoyo serikali haiuoni?

Mzee William Kibogoyo pichani.

Na Prudence Karugendo
 
MACHAFUKO yanayotokea katika jamii, hasa mapambano yanayofikia watu kutoana roho na baadaye kuonekana ni vita ya kiukoo au kikabila, ni mambo ambayo serikali inatakiwa kuhakikisha hayatokei hata mara moja. Ni kwa sababu machafuko ya aina hiyo yanaigharimu sana serikali kuyatuliza na kuirudisha jamii katika hali ya kawaida.
 
Ikizingatiwa kwamba serikali inakuwa wakati mwingine imepoteza roho za watu, wananchi, ambazo haiwezi kuzirudisha kwa gharama yoyote, miundombinu na mali huvurugika sawia huku serikali ikiendeleza wimbo wake wa amani na utulivu!
 
Ipo mifano kadhaa hapa nchini ambapo hali imechafuka sana katika baadhi ya jamii, watu wa jamii moja wakazua uhasama,  wakapigana na hata kutoana roho kutokana na mambo ambayo kama yangechukuliwa kihekima yangeweza kumalizwa bila kusababisha uhasama unaofikia hata kumwaga damu ya wananchi.
 
Hali hiyo ya uhasama ndani ya jamii huanzia kwa vitu vidogo na wakati mwingine kwa watu wachache wanaoweza kuwa kati ya mtu mmoja na mwingine.
 
Hali ya aina hiyo imeishatokea mkoani Mara ambako serikali imehangaika sana kuituliza mpaka kufikia kuunda kikosi maalumu cha askari na kulipa jina eneo hilo, hasa katika wilaya ya Tarime, kuwa ni Kanda Maalumu ya Kipolisi.
 
Umaalumu wa kanda hiyo hautokani na heri, bali ghasia zinazoachwa kiuzembe zikajitokeza.
 
La kuzingatia ni kwamba uongozi wa serikali, kuanzia ngazi ya mtaa, kijiji, kitongoji na kuendelea,  ndio unaopaswa kuwa makini kuhakikisha wananchi wanaishi kwa maelewano mazuri, bila chuki wala ugonvi baina yao.
 
Ikumbukwe kwamba ugonvi kati ya mtu na mtu unaweza kusababisha kuibuka ugonvi kati ya familia moja na nyingine, baada ya hapo ukaibuka ugonvi kati ya ukoo mmoja na mwingine,  unaoweza kusambaa na kuwa ugonvi wa kikabila.
 
Hayo yanaweza kutokea kutokana na serikali kutoyapa umuhimu mambo madogo yanayoweza kukua na kuwa makubwa kupitiliza. Maana ilisemwa kwamba hasiyeziba ufa hujenga ukuta.
 
Haya nayasema kutokana na kisa kilichompata mzee mmoja mstaafu, William Kibogoyo, wa Kishanda, Muleba, Kagera.
 
Mzee Kibogoyo, baada ya kustaafu kazi akaamua kwenda kumalizia maisha yake yaliyobaki kijijini kwake Kishanda. Amelima shamba lake zuri la migomba, mibuni na mazao mengine, kama ilivyo kawaida ya watu wa jamii ya Kihaya, wakazi wa maeneo ya Bukoba na Muleba.
 
Tatizo la wastaafu karibu wote ni moja. Ni kwamba kufanya kwao kazi nje ya vijiji walivyozaliwa au kununua mashamba, hasa wanaokuwa wametoka kufanya kazi katika maeneo ya mijini, na zaidi nje ya mikoa yao, wanaonekana ni viumbe tofauti kabisa na watu  waliokutwa vijijini. Wastaafu mara nyingi hawaonekani kama wazaliwa halisi!
 
Hawa wastaafu, wengi wao, wanakuwa wamepoteana na wenyeji wa vijijini kwao tangu enzi za shule hadi wanafanya kazi. Kwa maana hiyo unaweza kukuta mtu hajaishi na wenyeji wa kijijini kwake kwa zaidi ya miaka 40. Hivyo anapostaafu na kuamua kurudi kijijini wenyeji wanamchukulia kama kiumbe tofauti kutoka sayari nyingine. Mara nyingi wanamuanzishia maneno ya kumzushia kuwa anaringa au anawadharau watu aliowakuta kijijini.
 
Mambo ya aina hiyo ndiyo yaliyomkuta Mzee Kibogoyo. Jirani yake mmoja, kwa kutumia mtindo huo wa kwamba Kibogoyo anaringa, alianzisha vurugu makusudi kwa lengo la kukwaruzana naye akidai Kibogoyo anamchukulia sehemu ya ardhi yake.
 
Kibogoyo, kwa kutumia hekima ya shule na utu uzima, akataka mambo hayo yaishe bila kwenda mbali. Lakini jirani yake aliendelea kuyapa uzito kiasi cha kumchukulia mstaafu huyo kama adui yake mkubwa.
 
Mzee Kibogoyo anasimulia kwamba siku moja alimkuta jirani yake huyo, aliyemtangazia uadui,  akifanya shughuli shambani kwake, akampa pole ya kazi, jirani yake kusikia hivyo akamuuliza wewe unanitafuta nini? Jirani huyo akaamua kumshambulia Kibogoyo na panga alilolkuwa nalo.  Katika kujitetea Mzee Kibogoyo akajikuta amekatika kidolegumba cha mkono, kumbe panga la jirani yake lililokuwa limemlenga kichwani ndilo lililomkata kidole hicho.
 
Basi ikatokea kukuru kakara, Mzee Kibogoyo akafanikiwa kumnyang’anya jirani yake panga lake naye akamjeruhi nalo kwenye mguu.
 
Taarifa za vurumai hiyo zilifikishwa kwenye vyombo vya dola, lakini cha kushangaza aliyesakamwa zaidi ni Kibogoyo badala ya jirani yake aliyeanzisha vurugu hiyo.
 
Baada ya hapo watoto pamoja na jamaa wa jirani yake  Kibogoyo waliamua kuvamia nyumbani kwake na kufyeka karibu shamba zima la migomba ya Kibogoyo. Katika mkasa huo pia walivunja vioo vyote vya madirisha ya nyumba ya mstaafu huyo, wakiwa vilevile wanalenga kuichoma moto nyumba hiyo.
 
Kibogoyo anasema kwamba habari za matukio hayo alizipeleka kwenye vyombo husika, lakini kinachomshangaza hakuona vyombo hivyo vikichukua hatua zinazositahili dhidi ya hao walioharibu mali zake na kutishia maisha yake. Anasema wabaya wake hao wameachwa wakitamba kwamba watamshughulikia mstaafu huyo mpaka wahakikishe analihama shamba lake na huo kuwa mwisho wake wa kuonekana katika kijiji hicho.
 
Maana baada ya migomba iliyofyekwa awali kuanza kuchipua upya,  watu hao wanaosemekana ni jamaa wa jirani yake Kibogoyo aliyeanzisha uadui kati yao, walirudi na kuifyeka tena migomba bila kujali kwamba kuna serikali wala kwamba wanaweza kuchukuliwa hatua za kisheria!
 
Inasadikiwa habari za unyama huo zimeishamfikia hata mkuu wa mkoa wa Kagera, Kanali Fabian Massawe, lakini bado hakujaonekana hatua zozote za kiuongozi zinazochukuliwa kulishughulikia suala hilo tete!
 
Ninachosema ni kwamba serikali ilipaswa kuingilia kati kukomesha uonevu na unyama dhidi ya mstaafu huyo. Hiyo ndiyo kazi ya serikali. Kazi ya serikali siyo kukaa na kusubiri majanga yatokee kwanza eti ndipo ichukue hatua.
 
 
Ieleweke kwamba huyo mzee mstaafu naye anao watoto na jamaa zake, jamaa hao na watoto wake wakiishiwa uvumilivu na kuamua kulipiza kisasi kwa kujichukulia sheria mkononi, tayari amani inakuwa imevunjika. Kinachofuatia ni machafuko makali, maana inakuwa tayari imevukwa mipaka ya kifamilia na kuwa mgongano kati ya ukoo mmoja na ukoo mwingine.
 
Serikali inaweza kujikuta inalazimika kutumia nguvu na gharama kubwa kushughulikia kitu ambacho ingeweza kutumia tu nguvu ya kawaida kukituliza.
 
Sababu kwa kutokuelewa jamaa wa jirani yake Mzee Kibogoyo kwa sasa wanaweza kujiona washindi kutokana na kumfanya mzee huyo aishi kwa wasiwasi na mashaka makubwa, roho mkononi, kutokana na unyama wanaomfanyia. Lakini pindi jamaa zake Kibogoyo wakiamua nao kulipiza kisasi ushindi huo wanaojidai nao hao mahasimu wa Mzee Kibogoyo unaweza ukaonekana si lolote si chochote.
 
Siombi hali ifikie huko, ndiyo maana nasema serikali ingetumia uwezo wake kwa sasa kuhakikisha inarudisha amani kati majirani hao wawili. Hiyo ni kuzingatia kwamba moto huunguzao nyika huanzia kwenye njiti moja ya kiberiti.
 
Unyama baina ya majirani, hata kama unadharauliwa na serikali, lakini ieleweke kuwa ni tatizo linaloweza kugeuka janga la kitaifa.
0784 989 512
Next Post Previous Post
Bukobawadau