Bukobawadau

Urafiki wa wapinzani na ushauri wao kwa rais Kikwete

Wenyeviti wa vyama vya Upinzani, James Mbatia-NCCR-Mageuzi (kushoto), Freeman Mbowe (Chadema) na Prof. Ibrahim Lipumba (CUF) wakizungumza na waandishi wa habari kuhusu uamuzi wao wa kuungana katika suala la Katiba. Picha na Maktaba 

Vyama vya NCCR Mageuzi, Chadema na CUF vimetangaza kuanza rasmi mikutano nchi nzima kwa lengo la kuushawishi umma kupinga kile walichokiita hujuma dhidi ya upatikanaji wa Katiba Mpya.
Jumapili, Septemba 15, vyama vikuu vitatu vya upinzani viliandika historia nyingine mpya katika tasnia ya siasa za Tanzania baada ya kuamua kushikamana kupinga Muswada wa Marekebisho ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba wa mwaka 2013.
Kauli za kupinga muswada huo ulianzia bungeni mjini Dodoma, lakini sasa umehamia nje ya Bunge na vyama hivyo vimetangaza azma ya kuanza kampeni ya kuuhamasisha umma kudai maridhiano kabla ya kuendelea na mchakato wa Katiba Mpya.
Wenyeviti wa vyama hivyo; James Mbatia (NCCR-Mageuzi), Freeman Mbowe (Chadema) na Profesa Ibrahim Lipumba (CUF) wamemtaka Rais Jakaya Kikwete kutousaini muswada huo kuwa sheria, hadi pale kutakapokuwa na maridhiano ya pande zote husika.
Wanasema mapendekezo mengi yaliyomo katika Rasimu ya Katiba iliyotolewa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba, yalipendekezwa na vyama hivyo,  hivyo havitakuwa tayari kuona maoni hayo pamoja na ya Watanzania wengi yakichakachuliwa.
Wanasema muungano wao ni mwanzo wa kuunganisha umma wa Watanzania kufanya uamuzi wa kunusuru utekaji madaraka na mamlaka ya nchi kutoka kwa wananchi.
Vyama hivyo, pia vilitangaza kuanza rasmi mikutano nchi nzima kwa lengo la kuushawishi umma kupinga kile walichokiita kuwa ni ‘hujuma dhidi ya upatikanaji wa Katiba Mpya’.
Mikutano hiyo itaanza Septemba 21 mwaka huu, kwenye Viwanja vya Jangwani, Dar es Salaam na baadaye viongozi hao watakutana na makundi mbalimbali yakiwamo asasi za kiraia, taasisi za dini, vyama vingine vya siasa, wasomi na taasisi za elimu.
Makundi mengine ni pamoja na vyama vya wafanyakazi, jumuiya za wakulima, wafugaji, wavuvi, sekta binafsi, watu wenye ulemavu, jumuiya za wanawake, vijana na wastaafu.
Tamko na madai yao
Tamko hilo la pamoja lilisomwa na Profesa Lipumba ambapo anasema wanachopigania ni kuurejesha mchakato wa Katiba Mpya mikononi mwa umma, anaongeza kuwa suala hilo kwa sasa limehodhiwa na CCM.
“Tunamshauri Rais Kikwete asisaini muswada huu, aurejeshe bungeni ufanyiwe marekebisho yenye kujenga kuaminiana na mwafaka wa kitaifa kwenye mchakato wa mabadiliko ya Katiba. Hatutakwenda kumwona, ila aurejeshe bungeni,” anasema  Lipumba na kuongeza:

“Mchakato huu unahitaji uvumilivu, staha na hekima na usitawaliwe na nia mbaya, ubabe, mabavu, kejeli na dharau hasa kutoka kwa watawala. Misingi hii ikipuuzwa mchakato mzima unaweza kutumbukiza taifa letu katika mpasuko, migogoro na hata machafuko.”
Anasema muswada ulipitishwa ukiwa na marekebisho ambayo yalifanyika kinyume na maoni ya wadau na kinyume hata na makubaliano ya awali ya Kamati ya Bunge ya Katiba, Sheria na Utawala kuhusu mamlaka ya Rais kuteua wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba.
Madai mengine ni kwamba wabunge wa CCM waliongeza baadhi ya mambo kupitia majedwali ya marekebisho, hivyo kutoa mwanya kwa Serikali inayoongozwa na chama hicho kupitia kwa Rais kuwa na mamlaka zaidi ya uteuzi wa wajumbe husika. Muswada huo ulipitishwa na wabunge wa CCM,  Septemba 6 mwaka huu, ambao walitumia wingi wao kuupitisha muswada huo katika mkutano wa 12 wa bunge ambao ulisababisha tafrani kiasi cha Mbowe na Mbunge wa Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi kutolewa nje ya ukumb wa Bunge kwa amri ya Naibu Spika, Job Ndugai.
Katika tafrani hiyo, baadhi ya wabunge wa upinzani walirushiana makonde na maofisa usalama, huku wabunge wote wa upinzani, isipokuwa Mbunge wa Vunjo (TLP), Augustine Mrema, wakiususia.
Mbowe
Yeye anasema wameamua kuweka pembeni tofauti zao kwa ajili ya kudai Katiba Mpya ya Watanzania wote, kwamba hata wanahabari wanatakiwa kuweka pembeni itikadi za vyombo vyao vya habari vinavyomilikiwa na vyama vya siasa, kuwa wakweli katika kudai Katiba Mpya.
“Waandishi wa habari msiwe  vipaza sauti  vya watawala bila kutafakari kwa kina Tanzania ya miaka 100 ijayo itakuwaje, wanahabari mnaweza kutunyima Katiba Mpya au mkatunyima kama ikitumika vibaya,” anasema.
Anaongeza kuwa  amani ya nchi inaweza kuvurugwa kama mchakato wa katiba utahodhiwa na chama kimoja cha siasa (CCM), “Ikiwa hivyo, sisi hatutakubali kuwa kondoo. Wanaohubiri amani watambue kuwa kuna misingi ya kuipata amani hiyo, amani inapatikana kunapokuwepo na haki.”
Huku akinukuu kitabu cha Mwalimu Julius Nyerere cha ‘Freedom and Unity’, anasema, “Ni rahisi mno kuliwasha taifa la watu ambao wamekwazika, taifa hili watu wamekwazika sana. Mchakato wa katiba unaweza kutibu majeraha makubwa ambayo yanalikabili taifa.”
Anasema fursa adimu ya kupata Katiba Mpya inapotezwa na bunge na CCM na anasisitiza kwamba wapinzani watatumia kila aina ya mbinu kuwaelewesha Watanzania kinachoendelea ili washiriki katika kuidai katiba iliyotokana na mawazo yao.
“Wapinzani hatutarudi nyuma na hatutakubali  nchi kurejeshwa chini ya uongozi wa katiba ya sasa. Hilo wenzangu (wenyeviti wenzangu) naomba mnielewe, Chadema hatukubali na naomba na nyinyi msikubali,  maana ndani ya CCM kuna kundi linataka kurudi katika katiba  hii tunayoilalamikia,” alisema.
Anasema katika kitabu hicho, Mwalimu Nyerere alisema, ‘Kuna siku wananchi watachagua kifo kama viongozi hawatakuwa makini’, kwamba hoja ya kutaka Amani  itaharibiwa na wale wenye dola, siyo vyama vya upinzani.
Mbatia
Kwa upande wake,  Mbatia anasema historia ya nchi inaonyesha kuwa waasisi wa kutaka sauti, kauli  na mawazo ya umma isikike katika kudai Katiba Mpya ni vyama vya upinzani. Anasema mwaka 1991 vikundi na wadau mbalimbali walikaa na kuanzisha mchakato wa Mabadiliko ya Katiba, kwamba ripoti ya tume ya Jaji Francis Nyalali iliyoundwa mwaka 1991 na ripoti ya tume ya Jaji Kisanga ya 1998 (white paper) zote zilikuja na mapendekezo ya kutaka Katiba Mpya, kupendekeza muundo wa serikali tatu na kwamba tume hizo  hazikuundwa kwa matakwa ya Serikali.
“CCM ndio nini… Wanatakiwa kujua kuwa Tanzania kwanza vyama baadaye, vyama vya siasa vilivyokuwa vikitawala nchini Kenya, Zambia vimekufa, lakini nchi hizo bado zipo.  CCM inaweza kufa, lakini Tanzania itaendelea kubakia” anasema na kuongeza;
“CCM wakisema wapinzani tunafanya vurugu wanakosea, hatuwezi kuangamiza wazo letu la kutaka Katiba Mpya, katika taifa hili Watanzania hawajawahi kuandika Katiba iliyotokana na mawazo yao.”
Anasema Katiba ni tamko la umma linalotokana na umma unataka ujiongoze namna gani, “Katiba Mpya ni tendo la maridhiano na kisiasa siyo tendo la kisheria, sisi tuna tofauti, lakini tumeziweka pembeni, tupo juu ya itikadi za vyama vya siasa.” Anasema maridhiano ya kisiasa ndio yalizaa Muungano wa Tanganyika na Zanzibar mwaka 1994 na pia yamezaa serikali ya kitaifa Zanzibar mwaka 2009 baada ya Katibu Mkuu wa CUF na Makamu wa rais wa Zanzibar, Seif Shariff Hamad na aliyekuwa rais wa Zanzibar, Aman Abeid Karume kuweka tofauti zao pembeni.
Anasema mawazo ya kutaka Katiba Mpya wanayoyasimamia sasa yapo katika rasimu ya Katiba iliyotolewa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba, hivyo ni lazima wayasimamie.
“Chama cha KANU hakipo Kenya lakini Kenya ipo, UPC ya Uganda haipo lakini Uganda. CCM inaweza kuondoka na kufutika kabisa katika historia ya nchi yetu lakini Tanzania itaendelea kuwepo” anasema.

Next Post Previous Post
Bukobawadau