Bukobawadau

Bibi harusi afariki saa kadhaa baada ya ndoa


Dar es Salaam. Mwanamke mmoja wa Ilala jijini Dar es Salaam, Mwanahamisi Saidi amefariki dunia wakati akijiandaa kwenda kwa mumewe baada ya kufunga ndoa.
Tukio hilo limesababisha sherehe ya harusi kugeuka kuwa msiba.
Tukio hilo la kuhuzunisha lilitokea Jumapili iliyopita, muda ambao bibi harusi alitakiwa kuchukuliwa na mumewe Amani Hassan kwenda nyumbani kwake.
Mwanahamisi aliaga dunia akiwa katika Hospitali ya Amana iliyoko Wilaya ya Ilala, baada ya kuugua ghafla.
Akizungumza kwa majonzi, Hassan alisema kuwa alifunga ndoa kwa taratibu za Dini ya Kiislamu Ijumaa iliyopita katika msikiti ulioko Vingunguti jijini Dar es Salaam na kupanga kwenda kumchukua mkewe siku ya Jumapili.
“Baada ya kufunga ndoa niliwaahidi ndugu wa mke wangu kuwa nitakwenda kumchukua mke wangu Jumapili kwa sababu upande wangu ulikuwa umeandaa sherehe iliyoanza Jumamosi na Jumapili ndio tulipanga kumaliza kwa kumchukua mwali wetu,” alieleza kwa masikitiko Hassan.
Alisema alipigiwa simu na mdogo wa marehemu kuwa mkewe ameugua ghafla na hana nguvu na kwamba anapaswa aende haraka akamuone.
“Nilipofika nikamkuta mwenzangu hali yake ni mbaya, hawezi kuongea na alikuwa ameshapoteza fahamu, nikafanya utaratibu wa kumpeleka Hospitali ya Amana,”aliongeza Hassan.
Alisema walipofika Amana, waliambiwa kuwa mgonjwa wao ameishiwa damu na wakati wakiwa katika harakati za kumhudumia, Mwanahamisi alizidiwa zaidi. Alisema bibi harusi alishindwa kupata pumzi, na hivyo kuwekewa mashine ya kumsaidia kupumua lakini ilipofika saa nane mchana aliaga dunia.
“Mshtuko wa taarifa zile ulinifanya nipoteze fahamu kwa muda, baada ya kuzinduka sikuwa na jinsi zaidi ya kumpigia dada yangu, ambaye ndio kama mzazi wangu kwa kuwa tupo wawili tu, wazazi wetu walishafariki.
Nilimtaarifu habari hizi za huzuni na kumuomba awaambie watu waahirishe sherehe na maandalizi yote ya kwenda Vingunguti.
Alisema wakati anatoa taarifa hizo tayari nyumbani kwao kulikuwa kumepikwa vyakula na shamshamra za muziki na ngoma zilikuwa zikiendelea.
“Yaani mpaka sasa siamini kilichotokea, tulikuwa na mipango mingi na mke wangu, hata picha za ndoa yetu bado sijazichukua najisikia uchungu sana ninapokumbuka tukio zima,” alisema Hassan.
MWANANCHI.
Next Post Previous Post
Bukobawadau