Bukobawadau

Maruku Vanilla Tunabisha; KAGERA Siyo Maskini!

Maneno huumba kama vile imani yenye matendo izaavyo matokeo. Neno lolote lianzapo kusikika masikioni, akili ya mwanadamu hukataa kulipokea haraka haraka au mara moja. Iwapo mtu atachagua kujiweka katika nafasi ya kupokea muendelezo  na msisitizo wa neno lilelile, taratibu neno litamgeuza alikubali na kisha imani yake itajengeka kulifanya neno husika kuwa la kweli. Hufikia hatua akili ikalipokea neno na kuliandalia makazi kwenye fikra kisha taratibu huanza kujitokeza nje katika matendo ya mtu aliyelipokea. Aanzapo kulitenda, mazingira pia humruzuku kwa matokeo yanayoendana na fikra zake, mawazo yake na imani aliyonayo.  

Kila kitu katika dunia hii kiliumbwa kutoka kwenye neno. Kila kitu kilikuwa nadharia kabla ya kuwa katika hali ya uyabisi au kubadilika kimfumo. Hata vitabu vitakatifu vinalithibitisha hili kwa kumnukuu Mungu akiumuumba mwanadamu na viumbe wengine pamoja na vitu vyote kwa kusema neno—“NATUFANYE……”

Naamu! Watu wanaamini Kagera ni maskini, Tanzania ni maskini, na nchi nzima kwa ujumla ni maskini! Sisi hatuamini hivyo na tunapingana kwa kila silaha na yeyote anayetaka tumuazimishe masikio yetu ili aziroge fikra zetu kwa tungo hizi. Kwetu Kagera ni tajiri, Tanzania ni tajiri na nchi yetu kwa ujumla ni tajiri. Haya yakisemwa, wengi wanataka ishara, wanataka kuonyeshwa uko wapi utajiri huo? Kabla ya kwenda kuwaonyesha utajiri unaoonekana kwa macho ya nje, lazima turejee kwenye msingi wa hoja yetu—utajiri ni fikra! Hivyo utajiri wa kweli huko kwenye halmashauri ya kichwa cha mtu na si kwingineko. Mtu kuwa tajiri lazima kwanza awe na fikra za kitajiri. Huwezi kuwaza kimaskini, ukamudu kuishi kitajiri. Na huwezi kukubali dhana kwamba wewe ni maskini halafu ukategemea utakuwa tajiri. Fikra za Kitajiri zinaambatana na tabia zake kama zilivyo fikra za Kimaskini. Hili leo hatutaliongelea kwa urefu. Japo tutafurahi iwapo msomaji atatupa maoni yake juu ya zipi ni tabia za watu wenye fikra za kimaskini kupitia marukuvanilla@gmail.com

Ukiishakuwa na fikra za Kitajiri kichwani, unaipa roho yako msukumo na nguvu ya kuoanisha na utajiri uliokuzunguka kwa nje kwenye Eneo lako, Wilaya yako, Mkoa wako, na Nchi yako. Ni vema kuweka bayana, kuwa na fikra za utajiri pekee haitoshi. Ili kukamilisha utengamano wa fikra za utajiri ndani ya kichwa na utajiri halisi nje katika mazingira, lazima ugharamike. Hakuna mafanikio katika dunaini hii mwanadamu anapata bila kutoa sadaka. Lazima ukubali kupoteza kitu fulani katika mapambano ili ufanikiwe kingine kilicho kikubwa zaidi. Hii ndiyo gharama kubwa ya kuupata utajiri ambayo imewashinda watu wengi wenye fikra za utajiri. Badala yake hubaki kuutamani utajiri au wengine hujikuta wanapita njia za mkato zisizokubalika ili kukamilisha sadaka hii.

Tatizo linalotukabili Wana-Kagera liko ndani ya fikra zetu kuliko uhalisia ulivyo kwenye mazingira yetu. Tukiwa tunatembea juu ya ardhi yenye rutuba, tumezungukwa na ziwa na mito inayotiririsha maji, tunavuta hali ya hewa safi kabisa, tuna mipaka jirani yenye fursa lukuki, tumelaghaika kuwa sisi ni maskini na maisha yetu lazima yapatikane kwenye migomba na kahawa tu! Tuliwekwa ndani ya boksi na tunaendelea kufikiri ndani ya kingo za boksi! Hakuna mtu anawaza kama ukulima wa Tangawizi, Mjanichai,mbogamboga,  au Parachichi unaweza kumfanya amudu vema maisha kuliko migomba. Wote tumeamua kufa na Kahawa utadhani waliotuweka ndani ya boksi waliahidi kutulaani iwapo tutabadilika na kuamua kufuga Sungura, Kware, Konokono, Mbuzi au Kuku.

Wito wetu Maruku Vanilla kwa Wana-Kagera ni kubadilisha fikra zetu zetu. Kuanzia sasa tutambue kwamba kusema “mimi nimaskini” ina maanisha “wewe huna fikra”  au fikra ulizonazo ni za kimaskini. Tusiruhusu masikio yetu yawe mwenyeji wa nadharia hasi na za kimaskini. Tupigane na yeyote anayetulazimisha kusadiki kuwa sisi ni maskini. Kutambua haya ni mwanzo wa kuwa matajiri.


Imeandaliwa na Maruk Vanilla Farming & Processing Ltdchini ya mpango wao wa “Business Clinics and Mentorship Programme”
Next Post Previous Post
Bukobawadau