Bukobawadau

Mnakusudia Kumdungua Nani!?.

Kwa wale wanaoifahamu vyema historia ya kuanzishwa jeshi la Polisi kwenye ukanda wa Afrika Mashariki, watakubaliana na mimi kwamba dhana nzima ilitokana na hitajio la watawala wa kikoloni kuweza kukabiliana na uasi wa wazalendo waliokuwa wakiasi na kudai kutambuliwa utu wao.
Sijaribu na wala simshauri mtu yeyote kujaribu kuhusianisha dhana hiyo na utendaji wa sasa wa jeshi la Polisi kwa vile wengi wa wakosoaji wa utendaji wa jeshi la Polisi wao wenyewe si Polisi, na hata hawajawahi kuwa polisi na mara nyingine hawajawahi kuwa askari ndani ya jeshi lolote na hivyo hawaelewi changamoto anazokabiliana nazo askari katika majukumu yake ya kila siku, na mchango wa changamoto hizo katika maamuzi yake ambayo mara nyingine huibua malalamiko.
Kinachonifanya kuandika makala haya hata hivyo, ni kile kinachoonekana kwenye viunga vya mji wa Mtwara kwa sasa ambapo wafanyakazi wa makampuni ya ujenzi wa bomba la gesi kutoka Mtwara kuelekea Dar wengi wao wakiwa na asili ya Uchina, wanaonekana kutembea kwenye viunga vya mji huku wakiwa wanasindikizwa na ulinzi mkali wa polisi walio kwenye mavazi rasmi ya kijeshi na bunduki zao mikononi.
Si lengo langu kurejea kusema juu ya sakata la gesi kati ya wananchi wa Mtwara na serikali hasa kwa vile binafsi navutwa kuamini kwamba pande mbili za sakata hilo yaani serikali na wananchi wamefikia mahala fulani katika kutafuta ufumbuzi wa changamoto hizo na mahala hapo pasingehitaji kuingiliwa na kalamu za waandishi kwa lengo la kuchokoa yaliyotulia.
Hata hivyo, uwapo wa hali hii ya wafanyakazi hawa wa kigeni kupewa ulinzi mkali namna hii, unasema juu ya ukweli kwamba hali bado si shwari sana kati ya pande hizo mbili hasa kwa vile ikiwa kungekuwa na muafaka wa kweli, basi kusingekuwa na haja ya mitutu kuwasindikiza wafanyakazi hawa hadi kwenye masoko na maduka wanunuapo bidhaa. Hiyo si hoja yangu ya leo hata hivyo.
Katika makala ya leo najaribu kufanya tafakuri juu ya kitendo hiki cha wageni hawa kupewa ulinzi mkali namna hii na jeshi la polisi kina tafsiri gani katika jamii kwa kuzingatia historia ya jeshi lenyewe, nchi na hata bara zima la Afrika.
Ingawa historia ya jeshi la Polisi inarudi nyuma zaidi hadi miaka ya 1800 wakati utawala wa wakoloni wa Kijerumani kwa kutumia maakida waliweza kulinda maslahi ya utawala huo hilo likihusisha zaidi sana kudhibiti aina yoyote ya uasi ama kutotii sheria na maelekezo ya wakoloni wale, ni hadi baada ya mwaka 1914 wakati wa vita ya kwanza ya dunia, ambapo Kamanda wa Jeshi la Kijerumani, Cornel Paul Von Lettow-Vorbeck alipowaunganisha wanajeshi wake na walinzi wa kiraia wakijulikana kama askari na kuvirudisha nyuma vikosi vya Waingereza na wanajeshi wa utawala wa makaburu wa Afrika Kusini. Askari walitekeleza majukumu kadhaa kwa niaba ya utawala wa kijerumani ikiwamo kuwalinda wakoloni wale na maadui wan je na kudhibiti uasi wa ndani wa wananchi dhidi ya watawala wa kikoloni, hata hivyo bado hakukuwa na mfumo rasmi wa jeshi la polisi.
Mnamo May 1919, jeshi la polisi likaanzishwa rasmi chini ya kile kilichoitwa The Tanganyika Police Force and Prison services. Hadi miaka mitatu baada ya kuanzishwa kwake mnamo 1922, jeshi hilo lilikuwa na Makamishina zaidi ya hamsini wa kizungu, Mainspekta zaidi ya ishirini wa kiasia huku waafrika wakiwa ni zaidi ya 700 waliokuwa askari wa kawaida na maafisa wadogo tu. Vita vya pili vya dunia vilivyoshuhudia kuanguka kabisa kwa utawala wa kijerumani, vilileta pia nafuu kwa wazawa ndani ya jeshi la polisi ambapo hadi uhuru wa Tanganyika mnapo 1962, zaidi ya maafisa wa ngazi za juu 25 walikuwa wakihudumu ndani ya jeshi hilo.
Mabadiliko hayo hata hivyo hayakubadili dhana nzima ya utendaji wa polisi na hata watendaji wakuu wa jeshi hilo hawakufanya ama hawakufaulu katika juhudi za kulibadili jeshi hilo kuwa jeshi lenye mtizamo wa kuhudumia wananchi na hivyo lilibakia kuwa jeshi la kulinda watawala isipokuwa sasa likilinda watawala wazalendo badala ya wakoloni. Hii ilichangiwa na uwepo wa sheria kadha wa kadha kandamizi zilizoachwa na wakoloni wa Kiingereza na watangulizi wao Wajerumani na pia sheria nyingine zilizotungwa baada ya uhuru kwa ajiri ya kulinda utawala mchanga wa wazawa. Baadhi ya sheria hizi zimeshuhudia mabadiliko ya polepole na nyingine zingali zikitumika hata sasa na kuibua malalamiko mengi kutoka kwa wananchi na taasisi mbalimbali, na hiyo si hoja yangu leo.
Madhila ya mfumo wa utawala wa chama kimoja cha siasa ndani ya jeshi la polisi yameendelea kuwa changamoto kubwa ndani ya jeshi hilo hasa kwa vile kwa mfumo huo wa utawala, jeshi la Polisi liliendelea kuwa chombo ya watawala kulinda maslahi ya utawala na kwa sehemu wananchi ikiwa tu wananchi hao wanakubali matakwa ya watawala bila maswali.
Tume ya Jaji Francis Nyalali pamoja na mambo mengine, ilipendekeza kubadilishwa kwa sheria nyingi ambazo zilihusiana moja kwa moja ya utendaji wa polisi ikiwamo Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya jinai (The Criminal Procedure Act, 1985) Sheria ya Mgambo (The People’s Militia Laws 1973 na 1989) na hata sheria ya usalama wa taifa (The National Security Act 1970) na nyinginezo nyingi. Hata hivyo mwenendo wa ama kuzifuta au kuzibadili sheria hizi umekuwa wa polepole kwa sababu nyingi tu na hilo limekuwa likiibua malalamiko miongoni mwa wananchi hasa wenye uelewa wa masuala ya sheria, na mwendo mdogo wa mabadiliko hayo umemaanisha mwendo mdogo wa mabadiliko ya jeshi la Polisi kwa ujumla wake.
Miaka ya karibu hata hivyo, jeshi la Polisi limekuwa likifanya juhudi kubwa ya kujibadilisha katika kile kijulikanacho leo kama Polisi Jamii. Ni jambo la kawaida sasa kusikia askari polisi akisema “Nina wateja hapa nawahudumia nipigie baadaye” na hili kwa wale wanaojua lilikotoka jeshi hili, wanajua kwamba mabadiliko makubwa yametokea. Naam, kutoka siku zile ambapo hata ulipokuwa ukienda kumuulizia ndugu yako ambaye ni askari kituoni kwake, ulikuwa ukipokelewa na kauli za “Zunguka huku, kaa chini, vua mkanda…” halafu ndipo uulizwe shida yako, hadi hapa ambapo walau askari anaweza kuzungumza na hata kumzungumzia mwananchi wa kawaida kwa kumwita mteja badala ya mhalifu hata kabla ya mahakama kusoma hukumu, bila shaka haya ni mabadiliko makubwa.
Ukweli unabaki hata hivyo, kwamba mabadiliko haya ni ya sehemu ndogo sana na Jeshi hili limebaki bado katika ngazi fulani fulani kuonekana kuwa chombo cha watawala dhidi ya watawaliwa na huo ndiyo msingi wa mimi kujihoji maswali mengi baada ya kuona wafanyakazi hawa wakipewa ulinzi mkali namna hii wa Polisi tena walio kwenye sare na bunduki mikononi.
Ninazo sababu kadha zilizofanya mimi kujihoji kama hivyo mojawapo ikiwa ni ukweli kwamba kwa miaka ya hivi karibuni tumesikia na hata maeneo mengine kushuhudia jinsi ambavyo wafanyakazi wenye asili ya China wamekuwa wakiwanyanyasa wanachi na hata kuwapiga vibao, ngumi na mateke mbele ya hadhara ya watu na wananchi hawa hawawezi hata kujitetea kwa vile wageni hawa ni mabingwa wa mapigano ya bila siraha almaarufu ‘Kungfu’. Ninachojiuliza ni je! Ikiwa mmoja wao ataamua kwa kukasirishwa kidogo kumnasa kofi mke wangu mbele ya watu, nitaweza kumdhibitije mtu huyu aliyepewa hadhi ya kibalozi kwa kulindwa na siraha nzito?.
Najiuliza ikiwa tumepima uwezo wa ufahamu wa watu hawa katika kuishi na watu wenye tamaduni tofauti kabla ya kuwapa hadhi kubwa namna hii au tunangoja yatokee yale ambayo yamekuwa yakitokea kila kukicha ndipo tufikirie njia mbadala?.
Lakini hilo si kubwa sana. Lililo kubwa na la muhimu ni mnawalinda kwa nguvu kiasi hiki dhidi ya nani?. Wakati kitaaluma askari mmoja anapaswa kuhudumia watu saba, hapa nchini askari mmoja anahudumia zaidi ya watu hamsini kwa sababu ya uhaba wa askari wenyewe nab ado tuna askari wa ziada wa kutoa ulinzi maalumu kwa wageni!. Kwa sababu gani!?.
Ikiwa ni kwasababu inahofiwa kwamba wananchi wanaweza kuwashambulia wageni hawa wakati wowote kama njia ya kulipiza kisasi kwa sababu ya kutoridhishwa kwao na jinsi suala zima la uchimbaji wa urudufu wa gesi linavyoendeshwa, tunadhani matumizi ya mabavu kiasi hiki ndiyo suruhu ya uzembe wetu wa kutoa elimu kwa wananchi wetu?. Najiuliza ikiwa wananchi hawa watatokea kwa sababu nyingine yoyote hata isiyohusu mabomba ya gesi kutofautiana na wageni hawa na kuzuka ugomvi kati yao, polisi huyu atafyatua risasi na kumwaga damu ya Mtanzania mwenzake kwa ajiri ya mgeni ambaye amepewa ulinzi maalumu ili kujenga bomba la kusafirisha rasilimali ya Tanzania kutoka eneo moja kwenda lingine?.
Najiuliza ikiwa itatokea hivyo, tutakuwa sisi tumefanya tofauti gani kati yetu na vibaraka wa wakoloni waliotumika na wakoloni ikiwa ni kwa hofu ama uvivu wa kufikiri kuwanyanyasa ndugu zao wakati wa ukoloni mkongwe?.
Najiuliza ikiwa tunafahamu na kukumbuka kwamba wazee wetu walimwaga machozi jasho na damu kututoa utumwani na sisi tunakirudisha kizazi kijacho baada yetu utumwani kwa kisingizio cha maslahi mapana zaidi!?.
Najiuliza kama tunayo kweli ya kuwalaumu na hata kuwatusi wazee wetu kwamba waliingia mikataba mibovu iliyowatia utumwani na wageni kwa vile hawakujua kusoma wala kuandika ilhali sisi tujuao kusoma na kuandika twafanya makosa yale yale?. Najiuliza ikiwa kizazi baada yetu kitajivunia chochote kuhusu sisi ama tutahukumiwa nao kwa vile tulikuwa wapumbavu tuliowatia wao utmwani tena ilhali babu wa babu zao walishalipa gharama ya uhuru wao?.
Najiuliza………..wacha ninyamaze nisiseme sana kwa hasara ya kichwa change na huzuni ya vitegemezi vyangu, salaam nawasalimia. 

Na: G. J. Kamenge
kamengez@hotmail.com
+255 785 66 99 59
Next Post Previous Post
Bukobawadau