Bukobawadau

Museveni: Urais wa Muhoozi unategemea uamuzi wake na waganda


Kampala. Rais wa Uganda, Yoweri Museveni amesema hana mpango wa kumuandaa mwanawe kuwa rais wa nchi hiyo kwa kuwa Uganda si nchi iliyo chini ya utawala wa kifalme.
Kauli hiyo ya Rais Museveni imehitimisha msimamo wake kuhusu taarifa zilizokuwa zikieleza kwamba ana mpango wa kumrithisha kiti hicho mwanawe, Brigedia Muhoozi Kainerugaba mara atakapoadchia madaraka.
Akizungumza na kituo cha televisheni cha Al Jazeera, Museveni alisema “Kijana huyu ni ofisa wa jeshi ambaye wala hana mpango na siasa.” Na hata hajawahi kuonyesha kufikiria kuingia kwenye siasa kwa siku za hivi karibuni.
Katika mahojiano hayo yaliyorushwa usiku wa kuamkia juzi wakati akiwa kwenye mkutano wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa mjini New York, Museveni alisema kwamba Brigedia kainerugaba hataweza kuingia kwenye siasa “kwa kipindi kifupi kijacho.”
Kwa sasa, Brigedia Kainerugaba ni mkuu wa kikosi maalumu cha wataalamu wa jeshi wanaoilinda familia ya Rais na kuweka mifumo ya kisasa ya ulinzi nchini humo.
Alipoulizwa iwapo mwanaye huyo wa kwanza anastahili kuwa rais ajaye baada yake, alisema: “Hiwezekani kwa kuwa hana mapenzi na siasa. Pia Uganda si nchi ya kifalme hivyo hawezi kurithishwa, tunategemea uchaguzi. Haiwezekani kuhamishia urais kwake. Kiongozi yeyote wa kisasa analazimika kuchaguliwa kupitia uchaguzi unaokubalika.”
Museveni ambaye amekuwa madarakani kwa miaka 27 alisisitiza kwamba hata iwapo mwanaye huyo ataonekana kuvutiwa na kuingia kwenye siasa katika kipindi kirefu kijacho, itakuwa ni juu yake na watu wa Uganda kuhusu kuingia katika wadhifa wa urais.
Mahojiano hayo yalilenga kupata kauli ya Museveni kuhusu taarifa zilizotolewa Mei mwaka huu kwamba Breigedia Kainerugaba anaandaliwa kwa ajili ya kurithishwa nafasi ya baba yake, hivyo amekuwa akipandishwa vyeo kwa kasi jeshini ‘kwa sababu maalumu’.
Taarifa hizi zilitolewa kwa umma baada ya kunaswa kwa waraka wa aliyekuwa mkuu wa Usalama wa Taifa, Jenerali David Sejusa kwenda kwa wakuu wengine wa usalama kutoa maelekezo juu ya hatua hiyo.
Jenerali Sejusa aliandika barua kwenda kwa mkuu wa vyombo vya usalama vya serikali akitaka kujua kuhusu tuhuma kwamba baadhi ya maofisa wa serikali akiwemo yeye wamekuwa wakipinga mkakati wa kumuandaa Muhoozi hivyo kuundiwa mkakati wa kuwekwa kando.
Daili Monitor
Next Post Previous Post
Bukobawadau