Bukobawadau

NAPE AMSHUKIA ZITTO KABWE

*Ni kuhusu taarifa yake kuhusu ukaguzi wa mahesabu ya vyama vya siasa
*Adai Chadema ndiyo inaongoza kwa hesabu zake kutokaguliwa
*Asema CCM imekuwa ikitii kukaguliwa hata kabla ya vyama vingi nchini

NA MWANDISHI WETU
SIKU moja baada ya Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), Naibu Katibu Mkuu wa Chadema, Zitto Kabwe, kutoa taarifa zinazoshutumu kuwa vyama vya siasa nchini havijafanyiwa ukaguzi wa mahesabu kwa muda mrefu, CCM imeibuka na kuitwisha Chadema tuhuma hizo.

Imesema yenyewe (CCM) imekuwa ikiitika mwito wa sheria hiyo na kwamba hesabu zake zimekuwa zikikaguliwa kwa miaka mingi sasa, hata kabla ya kuanzishwa mfumo wa vyama vingi vya siasa hapa nchini.

Akizungumza na Waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam, Katibu wa NEC, Itikadi na Uenezi,Nape Nnauye amesema, ni sahihi kwa hesabu za vyama vya siasa kukagukiwa kwani ni kwa mujibu wa sheria, na ndiyo sababu CCM imekua ikitekeleza sheria hiyo kwa miaka mingi hata kabla ya kuanzisha mfumo wa vyama vingi vya siasa.

Nape alisema, badala yake chama kinachopaswa kutiliwa shaka kuhusu ukiukaji wa sheria hiyo, ni Chadema, chama ambacho alidai kimekuwa na tabia ya kufanya mambo mengi kinyume cha sheria kwa kisingizio cha mwavuli wa siasa.

"Chama Cha Mapinduzi kimekuwa kikiitekeleza sheria hii vizuri. Kwa mfano hesabu za CCM zilikaguliwa na wakaguzi wa nje TAC (Tanzania Audit Corporation) kuanzia mwaka wa Fedha 1977/1978 hadi mwaka 2002/2003. Kuanzia mwaka 2003/2004 hadi 2010/2011 tulikaguliwa na TAC- Associates, shirika hili linatokana na Tanzania Audit Corporation lililobinafisishwa", alisema Nape.

Alisema, 29/01/2013 CCM iliandika barua yenye kumbukumbu CMM/F. 20/80/89 kuwasilisha rasimu ya hesabu za mwaka wa fedha wa 2011/2012 ili Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Serikali (CAG) aipangie mkaguzi.

"Kufuatia barua hiyo, CAG alitupangia TAC-Associates kukagua hesabu hizo za mwaka 2011/2012. 


Kwa kawaida muda wa wakaguzi ni miaka mitatu hivyo TAC- Associates watakua wakaguzi wetu mpaka mwaka wa fedha wa 2013/2014, baada ya hapo CAG anaweza kuteua wakaguzi wengine", alisema Nape.

Nape alisema, hesabu za CCM zilizokaguliwa na wakaguzi wa nje TAC- Associates mwaka wa fedha 2009/2010 na 2010/2011 zilikwishawasilishwa kwa CAG na kwamba hesabu za mwaka wa fedha 2011/2012 bado ziko kwa wakaguzi wa nje, wakishakamilisha nazo zitawasilishwa kwenye vikao vya Chama na hatimaye kwa CAG.

Alifafanua kwamba,  hesabu hizo zikikaguliwa kwa mujibu wa utaratibu, anapelekewa CAG ambaye ndiye anazipeleka kwa Msajili wa vyama vya siasa.

Nape alisema kutokana na maelezo haya CCM haihusiki na agizo la PAC na kama kamati ya bunge ikitaka CCM ipo tayari kwenda kukutana kamati hiyo, huku CCM ikiwa na mahesabu yake yaliyokaguliwa.

"Mwito wetu kwa Zitto aanze kwa kutoa boriti kwenye jicho lake ndipo aone kibanzi kwenye jicho la mwenzake. Tunaamini kwa sababu mbalimbali zikiwemo za kuwa na vyanzo vya fedha visivyo visafi na tabia iliyokubuhu ya kupenda kukiuka kila sheria nchini wakidhani ndio staili ya kujenga chama chao, si ajabu kuwa Chadema wanaweza kuwa hawajakaguliwa kwa miaka yote hiyo. Zitto kama Naibu Katibu Mkuu wa Chama chake anapaswa kuwajibika kwa hili, yeye na Chama chake", alisema Nape na kuongeza;

"Wote tunakumbuka kelele zilizopo mtaani juu ya matumizi mabaya ya ruzuku zinazoelekezwa na Chadema na viongozi wake kutoka kwa wanachama wao, hivyo si ajabu wakawa wanakiuka sheria hii na ndio chanzo cha kelele hizo za wanachama wao".

Nape alitaka ikibainika kuwa ni kweli Chadema wamekiuka sheria hiyo muhimu, basi viongozi wa vyama husika wawajibike kwa kuwa si busara kuwa na viongozi wa kisiasa walikubuhu kwa kuvunja sheria za nchi na kujificha chiniya mwamvuli wa siasa.


"Uvunjaji wa sheria hii kwa wenzetu sio kwa bahati mbaya kwani wamezoea kutoheshimu sheria za nchi mpaka kufikia mahali pa kutangaza hadharani kuwa wanatamani nchi isitawalike. Ni muhimu kujenga utamaduni", alisema Nape. 
Next Post Previous Post
Bukobawadau