Bukobawadau

Hofu yatanda Kamati Kuu Chadema

Mwenyekiti wa Chadema Freeman Mbowe (katikati) akiwa na walinzi wake akiwasili katika Jengo la Ubungo Plaza, Dar es Salaam, jana kushiriki kikao cha Kamati Kuu ya chama hicho. Picha na Michael Jamson

Dar es Salaam. Hali ya wasiwasi iligubika eneo  kinapofanyika kikao cha Kamati Kuu ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kilichoanza Dar es Salaam jana.
Ulinzi mkali wa walinzi wa Chadema (Blue Guard), uliimarishwa katika ukumbi wa Ubungo Plaza kinapofanyika kikao hicho ambacho kinatarajiwa kumalizika leo, huku kukiwa na maagizo yaliyoashiria kuwapo kwa mambo mazito.
Maazimio ya kikao hicho yanasubiriwa kwa hamu na wafuatiliaji wa mambo ya siasa nchini kwani kinafanyika katika kipindi ambacho chama hicho kikuu cha upinzani nchini kinapita katika misukosuko na hasa ya malumbano baina ya makamanda wake wa juu.
Maelekezo ya ulinzi
Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe aliwasili ukumbini hapo saa 5.20 asubuhi na baada ya kuingia, wapiga picha waliruhusiwa kuingia kuchukua kumbukumbu ya tukio hilo kwa dakika moja tu.
Waandishi wa habari hawakutakiwa kuingia na badala yake walielezwa kuwa wangepewa taarifa baadaye.
Wakati wapiga picha wakiwa ndani, mmoja wa wajumbe wa mkutano huo alitoka na kutoa maelekezo kwa walinzi wa Chadema akiwataka kuwa makini kutekeleza kazi yao watakapopewa amri ya kumwondoa mjumbe yeyote mkutanoni.
“Kama mkipewa amri ya kuondoa mtu ingieni na mtekeleze amri hiyo mara moja,” alisisitiza mjumbe huyo na kuingia ndani haraka. Walinzi hao zaidi ya 10, walipokea maelekezo hayo kwa kutikisa kichwa kuashiria kukubaliana na amri hiyo.
Kikao kufunguliwa
Kikao hicho ambacho kilifunguliwa dakika nane baada ya Mbowe kuwasili, kilipangwa kujadili mambo matatu jana.
Mmoja wa wajumbe wa mkutano huo ambaye hakutaka kutajwa jina lake alisema kingepitia taarifa za vikao viwili vya Kamati Kuu vilivyopita.
Suala jingine ambalo lilipangwa kujadiliwa jana ni ushiriki wa Chadema katika uchaguzi mdogo wa Mjumbe wa Baraza la Wawakilishi Jimbo la Kiembesamaki, Zanzibar na kupitia taarifa ya fedha
Leo moto
Ajenda zinazotarajiwa kujadiliwa leo ni pamoja na ripoti ya utekelezaji wa Kampeni ya ‘Movement For Change’ (M4C) na hali ya siasa.
Ajenda hiyo inatazamiwa kugusa matukio ya hivi karibuni ndani ya chama hicho. Hayo ni pamoja na malumbano kati ya Naibu Katibu Mkuu, Zitto Kabwe na Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema kuhusiana na masuala ya posho, kusimamishwa kwa Mwenyekiti wa Chadema wa Mkoa wa Arusha, Samson Mwigamba, kuvunjwa kwa uongozi wa Mkoa wa Mara na pia kuondolewa kikaoni kwa Mbunge wa Maswa Magharibi, John Shibuda.
Zitto na Lema waliingia katika vita ya maneno mwanzoni mwa Novemba kuhusiana na masuala ya posho ya vikao.
Vita hiyo ilianzishwa na Lema katika kikao cha wabunge wiki iliyopita aliposema kuwa Zitto anafanya unafiki kukataa posho.
Lema alimtuhumu Mbunge huyo wa Kigoma Kaskazini kwamba anakataa posho za vikao bungeni, lakini anapokea posho nyingi kutoka mashirika mbalimbali ya kijamii nchini.
Lema aliweka tuhuma hizo kwenye Mtandao wa Jamii Forum huku akisema suala hilo halihitaji vikao vya chama kulijadili isipokuwa vyombo vya habari na hususan, mitandao ya kijamii kwani hata Zitto hutumia mitandao hiyo.
Akijibu hoja hizo, Zitto alisema tangu siku nyingi alikwishapiga marufuku kwenye Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) kupokea posho kutoka taasisi au mashirika yanayosimamiwa na kamati hiyo.
Alisema tangu alipokuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Mashirika ya Umma (POAC), alipiga marufuku posho na pia aliwahi kuwashtaki Taasisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa (Takukuru) wabunge wanaochukua posho kutoka taasisi za Serikali.
Zitto pia alipata msukosuko mwingine baada ya kusambazwa ripoti inayoitwa ‘Taarifa ya Siri ya Chadema’ iliyomtuhumu kuwa alikuwa anashirikiana na CCM na viongozi wa Idara ya Usalama wa Taifa kuhujumu chama hicho.
Ripoti hiyo inayodaiwa kuwa iliandaliwa na Idara ya Upelelezi ya Chadema, ilieleza kuwa Zitto alikuwa akipokea fedha kutoka kwa maofisa wa usalama na kuzisambaza kwa makada wengine wa chama hicho ili wafanye kazi ya kukihujumu. Hata hivyo, Chadema kupitia kwa Mnyika ilitoa taarifa kupinga vikali suala hilo.

.
Next Post Previous Post
Bukobawadau