Bukobawadau

MBUNGE BUKOBA VIJIJINI AHOJI SHULE KUKOSA MAJENGO NA KUEZEKWA KWA NYASI SHULE ZA MSINGI ZA KAMUKOLA NA RUZILA

MBUNGE wa Bukoba Vijijini, Jasson Rweikiza (CCM), ameihoji serikali ni kwanini shule za msingi za Kamukola na Ruzila hazina majengo, licha ya kuwa zimesajiliwa na kufanya mitihani ya taifa.

Alisema shule hizo hazina majengo na badala yake zina mabanda ambayo yameezekwa kwa majani, jambo ambalo ni aibu kwa serikali.

Rweikiza alitoa kauli hiyo bungeni jana alipokuwa akiuliza swali kutaka kujua serikali imechukua hatua gani kunusuru shule hizo ambazo zimesajiliwa kisheria.

Pia alitaka kuelewa kwanini serikali isiangalie uwezekano wa kuwapeleka watoto wa shule hizo katika Shule ya Msingi Kemondo na Mjule, ili kuondokana na msongamano.

Akijibu swali hilo, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Hawa Ghasia, alisema serikali inatambua umuhimu wa kuboresha mazingira ya kufundishia na kujifunza.

Aidha, alisema shule ambazo mbunge amezitaja zilianzishwa kwa lengo la kuwasaidia wananchi wa Kata ya Rukoma ambao ni jamii ya wakulima na wafugaji wa kuhamahama.

Alisema hadi sasa Shule ya Kamukole ina wanafunzi 195 na Ruzila wanafunzi 255 na shule zote zina vyumba vya madarasa vitano na upungufu wa vyumba nane.
Next Post Previous Post
Bukobawadau