Bukobawadau

WIVU WA MAPENZI WASABABISHA MAUAJI YA KUTISHA DAR, MFANYABIASHARA WA MWANZA AUA DADA WA MPENZI WAKE, AJERUHI WENGINE NA KUJIPIGA RISASI NA KUFA PAPO HAPO

 Majeruhi wa tukio la mauaji ya wivu wa mapenzi, Francis Shumila, akiwa chumba cha dharura Taasisi ya Mifupa (MOI), Dar es Salaam leo asubuhi, muda mfupi baada ya kufikishwa toka eneo la tukio Klabu ya Wazee Amana Ilala,alikoshambuliwa na mfanyabiashara wa jiji la Mwanza, Gabriel Munis aliyetaka kumuua anayedaiwa kuwa mpenzi wake Christina Alfred,lakini akamuua dada ya mpenzi wake huyo, kujeruhi watu watatu na kisha kujiua kwa kujipiga risasi.
Gari namba T 537 CJY aliyokuwa amepanda mpenzi wake huyo  pamoja na jamaa zake inavyoonekana baada ya kushambuliwa na risasi.
Kumradhi kwa picha hii. Huyu ndiye bwana Gabriel Munis 
baada ya kujiua.(Imeandaliwa na www.mwaibale.blogspot.com)

Na Dotto Mwaibale

SAKATA la mauaji yanayotokana na wivu wa mapenzi limeendelea kulisakama Jiji la Dar es Salaam ambapo sasa  mfanyabiashara Gabriel Munis (30-35) amemwua kwa risasi mdogo wa mpenzi wake, kisha kujimaliza mwenyewe.

Mfanyabiashara huyo wa mkoani Mwanza, alifikia hatua ya kujiua kwa kile kinachodaiwa kuwa alikuwa akidhani watu aliowamiminia risasi wote walikuwa wamefariki dunia.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ilala, Kamishna Msaidizi (ACP), Marietha Minangi akizungumza na wanahabari Dar es Salaam leo mchana, alisema tukio hilo lilitokea jana saa 1:00 asubuhi eneo la Klabu ya Wazee Amana karibu na Hospitali ya Amana.

Kamanda Minangi alifafanua kuwa jana asubuhi Chritina ambaye ndiye alikuwa mpenzi wa Gabriel alikuwa ndani ya gari pamoja na mama yake mzazi Helena Eliezer, mdogo wake Alfa (34) (ambaye ni marehemu sasa) na dereva Francis walikuwa wanatoka ndani ya geti la nyumba waliyokuwa wakiishi.

Alibainisha kuwa baada ya kutokeza nje ya geti hilo ndipo walimkuta marehemu ambaye ghafla alianza kuwamiminia risasi  iliyompata Francis begani na kichwani huku Christina ikimpata mguuni sanjari na mama yake huku na kumpiga mdogo wake ambaye alifariki dunia papo hapo.

Kamanda Minangi alisema baadaye marehemu alijipiga  risasi na kufariki papo hapo.

Alisema miili ya Alfa na Gabriel imehifadhiwa katika Hospitali ya Amana ambapo majeruhi hao hao wawili walikimbizwa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH).

Alisema Christina alitibiwa katiak Hospitali ya Amana na kuruhusiwa huku mama yake na dereva walikimbizwa katika Hospitali Muhimbili huku Francis hali yake ikidaiwa kuwa mbaya.

Mmoja wa ofisa wa jeshi la polisi ambaye hakupenda kutaja jina lake kwa kuwa si msemaji alisema Munis alikutwa na magazini mbili na aliwafyatulia lisasi 14 na kuwa inaonesha kabla ya tukio hilo huenda kulikuwa na mtu aliyekuwa akiwasiliana naye.

Alisema walioshambuliwa katika tukio hilo ni familia moja inayodaiwa ilikuwa ikimsindikiza Christina aliyekuwa akienda nchini Cyprus.

"Habari ambazo hatuna uhakika nazo zinadai kuwa Christina alikuwa akienda uwanja wa ndege kwa safari ya kwenda katika nchi hiyo" alisema ofisa huyo.

Tukio hilo linakuja ikiwa ni mwezi mmoja baada ya tukio jingine kama hilo kutokea eneo la Kibamba Dar es Salaam mwezi uliopita.

Katika tukio hilo Anthery Mushi alimpiga risasi mama mazazi wa mpenzi wake Ufoo Saro Mtangazaji wa Kituo cha televisheni cha ITV kisha kumjeruhi Ufoo na kujiua mwenyewe akidhani alikuwa ameshawaua wote.
Next Post Previous Post
Bukobawadau