Bukobawadau

“MADIBA”KATUACHIA FUNDISHO,TUTALITEKELEZA?

Na Prudence Karugendo
SIDHANI kama kuna mtu aliyepata kufa kwa furaha kama alivyokufa mzee wetu, Nelson Rolihlahla Dalibunga Mandela “Madiba”. Hayo nayasemea kwa watu walioonja utamu wa kuongoza au kuwatawala wenzao.
Sababu toka mwanzo Mandela alithihirisha wazi kuwa uhai wake haukuwa na maana yoyote kama ungemfanya aishi kuushuhudia upotevu wa haki, unyanyasaji na ukandamizaji wa mtu mmoja kwa mtu mwingine pamoja na ubaguzi wa rangi na wa kikabila.
Hayo ni mambo ambayo, tangu ujana wake, Mandela alipigana nayo akiwa na imani kwamba ni lazima siku moja yangetokomezwa. Na hakuwahi kuyapinga mambo hayo kiuwoga, aliyapinga kiwaziwazi huku akianzisha usemi wake maarufu wa kwamba kama anayoyapinga hayaondolewi basi yeye yuko tayari hata kufa, akisema kwa kutumia kimombo “for which I am prepared to die”.
Kwahiyo tutaona kwamba Mandela tangu ujana wake, alikisimamia alichokiamini ni cha kweli na kukithamini kiasi cha kukiona kina umuhimu kuliko hata alivyouona umuhimu wa uhai wake.
Tofauti na ilivyo kwa wengi wetu, Mandela hakukiogopa kifo hata kidogo lilipokuja suala la kutenda haki. Sababu alielewa kwamba hata ukikiogopa kifo na kukiheshimu kwa namna ya pekee ni lazima utakufa tu. Sababu kifo hakikubali hongo ya aina yoyote. Hivyo aliona ni upuuzi kuyatelekeza unayoyaamini, ikiwa ni pamoja na kuutelekeza utu wako, eti kwa kukiogopa kifo.
Mfano, wakati fulani akiwa jela, anasema madaktari walimpima afya yake na kumpa ushauri kwamba aache kutumia chumvi katika chakula, yeye akawambia madaktari kuwa kutotumia chumvi ni kujitesa kwa ajili ya kuogopa kifo ambacho kamwe hakiepukiki, akasema yuko tayari kufa kuliko kujitesa, akaendelea kutumia chumvi.
Maisha yake, tangu akiwa kijana, alipambana na kitu kilichopata umaarufu duniani kote kama “apartheid”, neno la Kiafrikana lililotokana na neno la Kingereza la “apartness”, kwa maana ya kila watu wa rangi fulani kuishi kivyao bila ya kuingiliana na rangi nyingine. Tayari huo ulikuwa ubaguzi wa rangi ambapo weupe waliwekwa daraja la kwanza wakiwa na upendeleo wa kila aina. Wakati huohuo weusi waliwekwa katika daraja la mwisho lenye manyanyaso na ukandamizwaji wa kila aina, tena kumbuka, hao ndio waliokuwa kwenye ardhi yao.
Ubaguzi huo wa rangi ulianzishwa na wazungu walioitawala Afrika Kusini kufuatia kuachiwa madaraka na wazungu wenzao, Wangereza, katika kilichodaiwa kuwa ni kuipa nchi hiyo uhuru. Ndipo wazungu hao walioachiwa madaraka waliponogewa na utamu wa utawala na baadaye kuibuka na mfumo huo wa utawala ulio mchafu hata kwa shetani.
Lakini sio wazungu wote walioupenda mfumo huo wa ubaguzi wa rangi. Mfano mmojawapo ni wa mzungu aliyekubali kuishi na Mandela katika nyumba ambayo chama cha ANC kilimjengea Mandela katika kitongoji cha wazungu cha Rivonia, wakati Mandela akijifanya ni dereva wa mzungu huyo na wakati mwingine akikata nyasi kwenye bustani ya nyumba hiyo. Mzungu ndiye aliyeonekana bwanamkubwa wakati mambo yalikuwa kinyume chake!
Hayo yalifanywa kuficha Mandela asigundulike na makaburu kuwa ndiye anayeishi pale.
Fundisho lingine ni kwamba Mandela alikuwa na kila njia ya kuitoroka nchi yake kwenda kuendesha mapambano dhidi ya ukaburu toka nje, kama walivyofanya viongozi wengi wa Kiafrika walioongoza mapambano kwenye nchi zao, lakini yeye hakukubali. Aliamua kubaki nchini mwake akiendesha mapambano tokea ndani.
Itakumbukwa jinsi mipango ilivyosukwa mwanzoni mwa miaka ya 1960, ikiihusisha Tanganyika, na Mandela akaweza kutoka nje ya nchi yake kwa mara ya kwanza kuitembelea dunia. Mandela alitorokea Bechuanaland, wakati huo, Botswana kwa sasa, kwa ndege ndogo ya kukodi na kufikia Mbeya, Tanganyika, alikoshuhudia kwa mara ya kwanza mtu mweusi akimfokea mzungu na mzungu akiufyata.
Alikuwa mkuu wa mkoa wa Mbeya wakati huo, Mwakangale, akiwafokea wazungu wa Hoteli ya Mbeya, alikopangiwa kufikia Mandela.
Baada ya Mandela kuizunguka dunia kwa msaada mkubwa wa Mwalimu Nyerere, alikwenda Ethiopia kuanza mafunzo ya ukomandoo chini ya walimu wa makomandoo wa Mfalme Haile Selassie wa nchi hiyo. Lakini hatahivyo ilibidi Mandela ayakatishe mafunzo hayo na kulazimika kurudi nchini kwake kufuatia matatizo yaliyojitokeza kule.
Alipofika Dar es salaam kumuaga Mwalimu Nyerere, Mwalimu akamuuliza kwa mshangao, kwamba hivi ni kweli umeamua kurudi kule? Mandela akasema ni lazima niende.
Muda mfupi baada ya Mandela kufika nchini mwake alikamatwa, akahukumiwa na kufungwa jela maisha.
Lengo kubwa la makaburu lilikuwa ni kuzivuruga harakati zilizokuwa zikiendelea za kuupinga ubaguzi wa rangi na vilevile kulifanya jina la Mandela lisahaulike kwa watu. Itakumbukwa kwamba Mandela hakuwa kiongozi wakati huo, isipokuwa alikuwa kamanda wa Umkhonto wesizwe, kitengo cha mapambano cha umoja wa vijana wa ANC.
Kitendo cha makaburu kumfunga Mandela jela maisha, lilikuwa ni kosa la kiufundi ambalo wao hawakulijua, sababu ni kitendo hicho kilicholikuza jina la Mandela kupita hata kiwango kile walichokuwa wanakiogopa wao.
Jina la Mandela likakua na kujulikana duniani kote likiwa linatumika kama alama (nembo) ya mapambano ya kutafuta haki.
Wakati makaburu wakidhani wamelimaliza jina la Mandela papohapo wakawa wamelikuza na kuwafanya wananchi wa Afrika Kusini wamwongezee lingine la kulipamba hilo lililotaka kufutwa, wakamwita Madiba, kwa maana ya babu.
Mara kadhaa makaburu walitaka kumwachia Mandela kwa masharti lakini yeye akayakataa na kusema kwamba kama ni hivyo bora afie gerezani. Hakutaka kuona anatoka gerezani halafu anaendelea kuishi katika hali ileile iliyomsababisha aingie gerezani kwa kuipinga. Sababu kwa kufanya hivyo alikuwa anajiona hajafanya lolote na angekuwa amepoteza muda wake bure.
Alikuwa mzaliwa wa Lupa, Chunya, Mbeya, Tanzania, Frederik Williem de Klerk, mwaka 1990 akiwa rais wa Afrika Kusini, alipoona kwamba kuendelea kumbakisha Mandela “lupango” ni kwenda kinyume, sio kwa matashi ya wananchi wa Afrika Kusini peke yao, bali kwa dunia nzima. De Klerk akaamua kumwachia huru Madiba Mandela, tena bila masharti yoyote.
Nchi za kwanza Mandela kuzitembelea baada ya kutoka kifungoni ni pamoja na Tanzania, nchi aliyoiaga kabla ya kwenda kifungoni. Ila wakati wa ziara yake hiyo ya kwanza tangu atoke kifungoni, hakupenda kuongelea lolote juu ya maisha yake ya jela, alikuwa akikataa kuyaongelea kwa kutumia usemi wa kwamba yaliyopita si ndwele, akisema kwa kimombo “let the bygones be bygones”.
Hiyo ni wazi kwamba Madiba hakuwa na kinyongo na mtu yeyote. Isipokuwa alionyesha upendo usiosahaulika kwa kuukumbuka mchango wa Tanzania katika harakati za ukombozi wa nchi yake. Akiwa katika Uwanja wa Taifa, ambao kwa sasa ni Uwanja wa Uhuru, alitamka maneno yafuatayo; “Tunawashukuru, tunawahusudu, tunawaheshimu na juu ya yote tunawapenda sana”. Maneno hayo aliwaambia Watanzania.
Baada ya Uchaguzi mkuu wa mwaka 1994, uliowashirikisha kwa mara ya kwanza wananchi wote wa Afrika Kusini, bila ubaguzi, pamoja na chama chake cha ANC kupata kile ambacho hapa nchini kinaitwa ushindi wa kishindo, Mandela alikazania kuunda serikali ya umoja wa kitaifa. Aliamini kuwa ile ni nchi yao wote akiwa amejitofautisha na viongozi wengine wa Kiafrika wanaodai kwamba ushindi ni ushindi hata kama ni kwa tofauti ya kura moja!
Maajabu mengine ya Mandela ni kwamba, akiwa rais alisafiri nje ya nchi yake wakati makamu wake akiwa nje vilevile, hivyo ikabidi Mandela amwachie nchi Waziri wa Mambo ya Ndani, Gatsha Mongosuthu Buthelezi, mtu aliyekuwa kibaraka mkubwa wa makaburu na mvurugaji namba moja wa harakati za wazalendo za kuutafuta usawa nchini mle.
Hatahivyo, pamoja na ukweli kwamba Mandela alijua kuwa anapendwa na wananchi kuliko mtu mwingine yeyote nchini mwake, hakutaka kuongeza kipindi cha pili cha uongozi. Alisema kwamba kimoja kilimtosha ili na wengine waongoze. Hiyo ni tofauti na tunavyowashuhudia baadhi ya viongozi wa Kiafrika wanaoyang’ang’ania madaraka na kutaka kuhakikisha wanafia madarakani!
Akiwa tayari ni Baba wa Taifa, Mandela alikubali mtoto wa rafiki yake kipenzi, Thabo Mbeki, mtoto wa Govan Mbeki waliyesota wote jela, aondolewe kimizengwe kwenye urais wakati Baba wa Taifa hilo la Afrika Kusini, alikuwa na kila uwezo wa kuinusuru hali hiyo. Aliamini kuwa nchi ni mali ya wananchi na si mali yake binafsi inayoweza kuendeshwa kwa msukumo wa urafiki binafsi kati yake na watu wengine.
Hivyo tunapopiga kelele tukiusema na kuusifu uzuri wa Mandela, hasa wakati wa tamasha la kifo chake, tunapaswa tujiulize kwamba aliyotuachia kama fundisho ni kweli tunayazingatia? Je, kama ni mazuri kwa kiasi tunachokionyesha, tuko tayari kuyafuata na kuyatekeleza?
Kama hatuwezi, ujasiri wa kuushangilia uzuri na uadhimu wa Mandela tunaupata wapi? Utayashangiliaje mambo ambayo moyoni unayaona ya ovyo? Sababu kama hatuwezi kuyafuata na kuyatekeleza aliyotuachia basi ni ya ovyo. Maana Mandela alikuwa binadamu kama sisi, hana chochote alichokifanya chenye nguvu za Kimungu, ambacho sisi kama binadamu hatukiwezi. Ni suala la uamuzi na utashi tu basi.
James Kiemi wa Isamilo, Mwanza, anasema, “Sipendi sana kuingia kwenye mtego huu, lakini itoshe tu kusema kuwa bila Nyerere Mandela asingekuwa hivi alivyo kwa sasa. Angekufa kimyakimya kama wapigania uhuru wengine wote na kusahaulika. Hata hivyo Mandela alikuwa na dhamani ya kipekee duniani, uvumilivu wa kupindukia, msimamo thabiti kabisa na kusamehe kusiko na mipaka”.
Nimalize kwa kusema kwamba Madiba, kwa upande wake, kafa kwa furaha kubwa maana aliyoyapigania akiwa ameiweka rehani roho yake kayatimiza karibu yote! Tangulia Madiba.
prudencekarugendo@yahoo.com
0784 989 512
Next Post Previous Post
Bukobawadau