Bukobawadau

UMOJA WA WANAWAKE KARAGWE: Wanawake pazeni sauti zenu

UMOJA wa Wanawake Wajane (UWK) Wilayani Karagwe umesema unyanyasaji wa kijinsia katika jamii unaweza kutokomezwa iwapo wanawake watavunja ukimya na kupaza sauti zao.
Akizungumza na waandishi wa habari jana mwenyekiti wa umoja huo, Grace Mahumbuka, alisema kuwa unyanyasaji wa kijinsia  utakoma ikiwa wanawake watavunja ukimya na kupaza sauti zao na kuripoti matukio  ya kikatili.
Alisema kuwa baadhi ya wanawake na watoto wamekuwa wakifanyiwa vitendo vya kikatili ikiwa ni pamoja na kubakwa, ukatili wa kingono, kulawitiwa, ndoa za utotoni na kutakaswa kwa wajane lakini matukio hayo yanashindwa kuripotiwa.
“Matukio ya unyanyasaji wa kijinsia  ni sawa na majanga mengine ya kitaifa, kwa wanawake wengi na baadhi ya watoto wamefanyiwa vitendo vya kikatili,” alisema.
Alisema ukatili huo wa kijinsia unahusiana zaidi na vipigo kwa wanawake kutoka waume zao na hata baadhi  kujeruhiwa, kukatwa viungo vyao vya mwili hali inayoweka rehani ubinadamu wao.
Alisema kuwa kuna umuhimu wa Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake (TAMWA) kushirikiana na Chama cha Wanasheria Wanawake Tanzania (TAWLA) kusambaza elimu vijijini ili kusaidia kupunguza matukio hayo.
Naye Diwani viti maalum (CCM) kata ya Kayanga, Joyce Mirembe aliwataka waandishi wa habari kuhakikisha hawaegemei upande wowote wanaporipoti matukio hayo.
Alisema mfumo wa kisheria uliopo unaoonekana kutokuwa na usawa huchangia wanawake kufanyiwa vitendo hivyo kushindwa kuchukua hatua za kisheria.
Next Post Previous Post
Bukobawadau